NA
HANIFA SALIM, PEMBA::
“HALI ya
maisha yangu ilikua ni ngumu mno, na wakati mwengine ili kutimiza mahitaji, ilimlazimu
muume wangu kuuza kuni,’’.
Ni maneno ya mama mmoja mwenye familia ya watoto watano Amina Juma
Salum (40) mkaazi wa kijiji cha Kwawema kilichopo shehia ya Mgogoni wilaya ya
Micheweni Pemba.
KABLA YA
KUJIAJIRI
Hali ya maisha yake ilikua ngumu kabla ya kuingia katika uanzishaji wa
mradi mbali mbali, na hapo ndio mume wake ilimlazimika kutafuta kuni auze, ili
kupata chakula walau kwa siku moja.
Shida hata kwa watoto wake kupata elimu, walipokua wanakwenda skuli
sare zao zilikua ni chafu, zimechanika na hata michango ya skuli ilikua inawashinda.
“Ninapotokezewa na misiba au harusi nilikua najisikia vibaya mno,
kwani nilishindwa kushirikiana na wenzangu katika michango ya kifedha, hadi
pale ninaposuka makuti na kuuza ndipo huchangi”, anakumbuka.
Maisha hayo yalikua ni ya takribani miaka 17 na ndipo ulipoanza mradi
wa kunusuru kaya maskini ambapo alipata fursa ya kujiunga na mradi huo, ambao
ulikua chanzo cha mbadilisha kimaisha yake.
Anasema hakufikiria akiwa macho wala kupitikiwa na ndoto, kuwa iko siku
atasahau machungu ya maisha, naye kuisha kama wengine.
‘’Watoto wangu hawaifahamu siku waliovaa nguo mpya hasa sikukuu,
walikuwa ni kuvaa mitumba ya bei ya chini na viatu vilivyochoka,’’anakumbuka.
Ingawa ndoto zake na hasa kwa kushirikiana na mume wake, alikuwa na
ndoto za kufanya mradi wowote ili kuwaokoa watoto wao na hasa kuwapatia haki
yao ya elimu.
‘’Nilisema peke yangu siku moja kuwa, kama mimi ni maskini na je
watoto wangu nao waishi kwenye maisha kama haya, nikasema hapana lazima
nipambane,’’anasema.
MWANGA
WA MAISHA YAKE ULIVOANZIA
Anasema, baada ya kufanyiwa udahili juu ya hali yake ya umaskini na
kisha aliingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini chini ya Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii Tanzania TASAF.
Kwa mara ya kwanza alipata
shilingi 42000 kama rukuzu kutoka TASAF alizitumia na nyengine kuziweka hakiba,
ambayo kila mwezi ziliongezeka kutokana na uwekaji wake.
“Nilitoa shilingi 10,000 nilimpa mume wangu, kwa ajili ya kununulia chakula,
tulikula vizuri kwa siku hiyo, wanangu pia niliwapa pesa ya kutumia skuli kila
mmoja shilingi 500 jambo ambalo lilikua ni ajabu kwao,’’ anasema.
Baada ya hapo anasema, alizaa wazo la kufuga kuku, mradi ambao
alibaini utawatoa kimaisha, na kuwaondoshea umasikini ambao walikua nao hapo
awali.
Mbali na kuwaza wazo hilo, aliamua kujishughulisha na kilimo cha migomba,
mihogo, minanasi na mboga mboga za aina mbali mbali, ili kuwa na uhakika wa
fedha ndogo ndogo.
Anafahamisha, walianza kufanya
matufali wao wenyewe ambayo walijengea banda dogo la kufugia kuku, kisha wakaomba
mabati ambayo yalishatumika kwa ajili ya kuezekea.
KUANZA
KWA MRADI
Alinunua kuku mmoja mmoja kulingana na pesa ambayo alikua akiipata
kupitia TASAF kila mwezi, waliongezeka kwa kuzaliana hadi kufika kuku 100,
kutoa 10 wa awali.
“Hapo nyuma sikua na utaratibu wa kuwanunulia wanangu nguo kinapofika
kipindi cha sikukuu, lakini baada ya kuanza mradi huu, kila inapofika mwezi wa Ramadhani
tunauza kuku wetu kwa ajili ya kukidhi mahitaji,’’ anasema.
Alianza mradi huo ambao ulikua ni kwa kuku 10 na hadi sasa ana wastani
wa kuku 100 wa kienyeji, bado anaendelea na biashara hiyo, kwa kushirikiana na
mume wake.
Anasema, kwa sasa ana uwezo hata wa kununua pikipiki (Bodaboda) kwa
pesa za kuku, anaofuga ikiwa atatamani kubadilisha maisha yake, kwa namna
nyengine.
Kwa sasa hivi amepiga hatua kubwa za kimaisha hadi kufikia kusomesha
mtoto wake katika skuli za binafsi, kupitia mradi huo wa kuku, jambo ambalo
mwanzoni hakulifikiria kwenye maisha yake.
“Naweza hata kuwaita ndugu zangu katika familia, kushirikiana nao
katika kujenga mambo mbali mbali, kusaidia familia yangu kwa kifedha na hata
mawazo,’’ anaeleza.
Kama akitakiwa kutoa maombi kwa wafadhili wengine au serikali ni
kuomba fedha hata za mkopo, ili kutanua banda kwa ajili ya mifugo yake ya kuku.
‘’Ndoto zangu za kuwa na maisha mazuri zimeshaanza kuona bandari na
kweli nimeamini zie kauli za viongozi kuwa tujiajiri, kwangu zimeshazaa
mafanikioa,’’anasema.
Anawashangaa wanawake wenzake, wanaoendeleza nafasi ya ugolkipa kwenye
ndoa, akisema sasa wanaume wa aina hiyo wameshaondoka duniani,’’anafafanua.
Hapa anakusudia kuwataka wanawake na hasa waliomo kwenye ndoa,
kuhakikisha wanakuwa na miradi japo midogo ambayo, itasaidia katika huduma za
kila siku.
Kwake anasema ijapokuwa TASAF ilikumkuta njiani kuelekea kujiajiria,
lakini haisahu ilivyomsukuma mbele na sasa kuwa mwanamke wa aina ya pekee
katika familia yao.
MALENGO
YA BAADAE
Malengo yake ya baadae anasema,
endapo hatopata msaada, anatamani kukuza mradi wa ufugaji wa kuku wa kienyejia,
ili aweze kuajiri wengine kijijini hapo.
Jengine sasa anatamani kuwasafirisha mwenyewe kuku wake kutoka Pemba
hadi Unguja, ili atakaporudi abeba mradi kama wa nguo.
‘’Kama mipango na mikakati yangu itafikiwa hapo baade, nataka niwe
mfugaji maarufu na mwenye wateja hata wan je ya nchi, kama sisi tunavyokea kuku
wa peduwi,’’anasema.
SOKO
Kwake soko la kuku na mayai ya kienyeji yake kama kusukuma mlevi
kwenye bonde, hana shaka wala wasi wasi nalo, maana akitangaaza tu wateja
wanajaa.
‘’Katika mifugo ambayo haina shaka ya wateja ni kuku wa kienyeji na
mayai, yake maana hata mimi kama nahitaji shilingi 100,000 ya haraka nikisema
tu, wameshanununuliwa,’’anasema.
Tena achia mbali wale wateja wetu kama wenye hoteli au wanaosafirisha
nje ya Pemba, yaani kwa wateja wapo kama mvua.
Kwa sasa soko lake ni eneo la miji ya Wete, Konde na Micheweni ambapo
ukiwapeleka maeneo hayo baada ya saa moja, unarudi na fedha.
MUME
WAKE
Seif Salum Hamad ni mume na baba wa familia hiyo ya watoto watano
anasema, mke wake amekua ni mshauri wake mkubwa na ndie aliyemfunua akili.
Anasema, mafanikio yote ambayo wanayapata ni mashirikiano na
masikilizano ambayo wanayo baina yake na mke wake, ndio sababu kubwa
iliyopelekea kufikia hapo.
“Katika shughuli zetu za kuendesha maisha tunasaidiana kwenye kilimo
na hata ufugaji wa kuku, huduma pia pale ambapo mimi napungukiwa kihuduma,
anasaidia ili muradi siku zinakwenda”, anasema.
Kipindi cha sikukuu hakua na uwezo wa kuwanunulia watoto angalau nguo
moja tena mpya, lakini baada ya kufanya shughuli hizo amekua ni muume mbele za watu.
Anaona sasa ndoa yake imepata mapana na kurejesha upya, mapenzi,
mahaba, masikilizano, uaminifu na kujiamini hasa katika hudumza za kila siku,
achia mbali matibabu.
‘’Sasa kupitia mke wangu nimeamini kuwa, wanawake wakiamua ni wachumi,
watafutaji, wawekaji akiba na wanaojali familia,’’anasema kwa furaha.
Anasema kwa sasa anajiamini kwa kuwa kila shilingi 100, inayotumika
katika huduma za lazima pamoja na ada ya mtoto wao anayesoma skuli binafi, basi
shilingi 70 ni za mke wake.
‘’Mimi sasa najiamini kama ntapata safari ya kikazi hadi mwezi mmoja,
mke wangu anauwezo wa kuiendesha familia n ahata wageni wakitokezea,’’anasema.
Malengo yake ni kuwasomesha watoto wake hadi kufika vyuo vikuu na
kuendesha maisha yao kwa shughuli nyengine kama vile kujenga nyumba kubwa ya
kisasa.
Anawashauri wanaume wenzake washirikiane na wake zao ili wabuni miradi
mbali mbali itakayowaondoshea umasikini na kuwaendeshea maisha yao ya kila
siku.
MAJIRANI
Omar Haji Khamis na Fatma Hija Othman wanasema, familia hiyo imeibuka
ghafla na leo kuwa mfano wa kuigwa kijijini kwao kimaendeleo.
‘’Kwa hakika jembe na ufugaji kama ukidhamiria haumtupi mtu, maana
mfano wa hayo ni Amina na Mume wake, walianza kama utani kufuga kuku 10, leo
wanahesabu 100,’’anasema Omar.
Kwa sasa inapofika kipindi cha sikukuu au mtu anapohitaji kuku,
imekuwa rahisi wao kufika kwa Amina na kununua kwa ajili ya kukamilisha
mahitaji.
SHEHA
Sheha wa shehia ya Mgogoni Said Hamad Khamis anasema, shehia hiyo ina
wakaazi 4,326 ambao wanajishughulisha na shughuli mbali mbali za kijamii na
kiuchumi.
Kwake jambo la kujivunia ni kuona baadhi ya wananchi akiwemo Amina Juma, wanafanya shughuli zao za
kijamii na kiuchumi ambazo zinawasaidia katika maisha yao ya kila siku.
‘’Kwa ninavyomfami Amina Juma Salum na mume wake, leo nikisikia
wanaisha kwenye maisha mazuri kwa sababu ya ufugaji na kilimo, hii ni furaha
maana wameyatekeleza kwa vitendo maagizo ya serikali,’’anasema.
“Katika shehia yangu ni mwanamke ninae muamini kati ya wale ambao
wanajishughulisha na harakati mbali mbali ili kuhakikisha wanapata maendeleo”,
anasema.
Anaiomba serikali iendelee kuongeza nguvu kwa wanawake ambao
wanajighulisha na kazi mbali mbali ikiwemo ujasiriamali, kilimo na ufugaji ili
waweze kuondokana na utegemezi na hali ngumu za kimaisha.
WANAHARAKATI
Afisa miradi kutoka TAMWA Pemba Asha Mussa Omar, anaseme wamekuwa
wakitoa elimu kwa wanawake, ili kubuni miradi ya kujiendesha kimaisha, badala
ya kutegemea familia kwa kila kitu.
Hassina Issa Shehe wa Mchanga mdogo, anasema miradi wanayoifanya
wanawake, imekuja kuimarisha ndoa na mahusiano mema kwa familia.
TASAF
Mratibu wa TASAF Pemba Mussa Said, anasema
wapo walengwa 14, 280 kwa Pemba ambao wanaendelea kupata fedha za kunusuriwa na
umaskini.
Walengwa
hao wapo kwenye shehia 78, ikiwemo ya Mgogoni, ambapo tayari shilingi bilioni
14. 4 zimeshwafikia.
‘’Mtu
kama Amina Juma ndio hasa malengo ya TASAF ya kumtoa mwananchi katika unyonge,
na kumleta kwenye taa, ili nae aishi maisha mazuri,’’anasema Mratibu.
“TASAF
inaorodha ya zaidi ya walengwa 50,000 kutoka wastani wa walengwa 15 kila
shehia, kati ya shehia 78, ambao wamenzisha miradi ya kujikwamua.
Mratibu
Mussa anabainisha kuwa, kwa mwaka 2014/2015 walengwa hao wa kunusuru kaya
maskini, waliibua miradi ya kijamii 41, idadi iliongozeka mwaka uliofuata kwa kufikia
miradi 84.
MWISHO.
Comments
Post a Comment