NA HAJI NASSOR, PEMBA::
MAHAKIMU,
waendesha mashtaka katika mahakama maalum ya kupmabana na ukatili na
udhalilishaji kisiwani Pemba, wameiomba jamii kuacha kuwalaumu, pale kesi za
aina hiyo, zinapofutwa au mtuhumiwa kuachiwa huru.
Walisema, wao yapofanyika matendo hayo huwa hawapo eneo
la tukio, hivyo hawajui kinachoendelea, na ndio maana wanategemeo wao
kuwaeleza, lakini kama hawafiki mahakamani kutoa ushahidi, na kesi kufutwa,
wasiangushiwe lawama.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kuelekea mwaka
mpya wa mahakama 2023, walisema jamii ndio ambayo inategemewa mno, na mahakimu
na waendesha mashataka, katika kufikia haki ya kweli.
Walieleza kuwa, wao wapo kuwasubiri wananchi kufika
mahakamani kuto ushahidi, hivyo kama wanakataa wito wa mahakama, kitakachofuata
ni mtuhumiwa kuachiwa huru.
Hakimu wa mahakama maalum ya kupambana na udhalilishaji
mkoa wa kusini Pemba, Muumini Ali Juma, alisema kama jamii inajua namna wao
wanavyokabiliana na wakati mgumu, ni kuwaonea huruma.
Alieleza kuwa, wao wanasubiri kuelezwa jinsi ubakaji au
ulawiti ulivyotokea na kisha kuupima ushahidi, kabla ya mahakama, kufikia
uamuzi wa kutoa hukumu.
‘’Wananchi wanatolewa wito wa mahakama ili waje
mahakamani tushirikiane, katika kufikia haki, lakini chakushangaaza hawaji,
sasa tuendelee kumshikilia mtuhumiwa hadi lini,’’alihoji.
Katika hatua nyingine, Hakimu huyo alisema, ili kila
kesi ili ifikiwe kutolewa uamuzi wenye tija, ni kuhakikisha suala la kufika
mahakamani kutoa ushahidi, lifanyike.
Kwa upande wake
Mwanasheria wa serikali Ali Amour Makame, alisema wazazi na walezi wamekuwa na
hamu ya kukutana na vyombo vya sheria, mara watoto wao wanapodhalilishwa,
ingawa baadae huvikimbia.
Alisema wanazo kesi kadhaa wazazi wamekuwa wakipokea
wito wa mahakama, lakini bila ya sababu za msingi huamua, kutodhuhuria
mahakamani.
‘’Ni kweli, hata sisi waendesha mashataka wakati
mwengine ndio tunaongoza katika kuiharakisha mahakama kuziondoa au kuwaachia
huru watuhumiwa, kwa vile mashahidi muhimu hawafiki mahakamani,’’alieleza.
Alieleza kuwa, wengine wanaofika mahakamani kwa
makusudi huwakana watuhumiwa, ambao awali waliwataja wakati wanahojiwa vituo
vya Polisi, kuwa ndio waliodhalilisha.
‘’Zipo sababu nyingi, moja wapo ni rushwa muhali, wengine
hasa kwa kesi za watoto wa miaka 16 hadi 17 ni kuzifanyia sulhu, ili kukimbia
adhabu,’’alieleza.
Aidha wakili huyo alisema, hata mwishoni mwa mwaka
jana, mahakama maalum ya kupambana na makosa ya udhalilishaji ya mkoa kusini
Pemba, ilimuachia huru daktari Hassan Said Mohamed miaka (38)
wa hospitali ya Chake chake, baada ya mtoto wa aliyedai kubakwa mara tatu,
kumkana daktari huyo mahakamani.
Aidha wakili wa utetezi, Massoud
Mohamd Said, katika shauri la kuingilia kinyume na maumbile, aliiomba mahakama
maalum ya kupambana na makosa ya udhalilishaji, kuliondosha shtaka hilo,
kutokana na upande wa mashataka, kushindwa kuwasilisha mashahidi.
Hata hivyo mahakama hiyo pia, mwezi
August mwaka jana ilimuachia huru mtuhumiwa mwengine wa kosa ka ubakaji, baada
ya shahidi nambari
moja (mtoto wa miaka 13), aliyedai kubakwa, kushindwa kufika mahakamani kutoa
ushahidi, licha kuitwa na mahkama mara saba.
Kwa
upande wake Naibu Mrajisi mahakama kuu kanda ya Pemba Faraji Shomari Juma, amesema mahakama itahakikisha sasa, inawapatia
nauli zao mashahidi wanaofika mahakamani, ili kusiwe na mkwamo wa kesi, hasa za
udhalilishaji..
Mwisho
Comments
Post a Comment