NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
WATUMISHI
wa umma kisiwani Pemba, wametakiwa kutumia lugha laini, zenye mvuto, shirikishi
na zenye heshima wakati wanapowahudumia wananchi wanaofika kwenye tasisi hizo
kudai huduma.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Chuo cha Utawala wa Umma ‘IPA’
tawi la Pemba Juma Haji Juma, wakati akizungumza na watumishi wa baraza la mji
Chake chake, wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na wa wizara
ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, kwenye mafunzo ya sehemu ya uthibitisho wa kazini,
yaliofanyika ukumbi wa Baraza la mji Chake chake.
Alisema, moja ya msingi mkuu kwa watumishi wa umma,
wakati wanapowahudumia wananchi, ni matumizi ya lugha sahihi na zenye ushawishi
wa kupokea na kutoa huduma.
Alisema, wapokea huduma huwa wanahitaji kusikilizwa, kushauriwa,
kufafanuliwa na wakati mwengine kuelezwa jambo lilipofikia, ambapo mchakato
wote huo, matumizi ya lugha nzuri ni jambo la kuzingatia.
‘’Niwakumbushe watumishi wenzangu wa umma kuwa, suala la
kutumia lugha isiyorafiki kwenye maeneo yetu ya kazi, haijengi bali inabomoa,
lazima tutumie lugha za mvuto, zenye heshima na nidhamu, na hayo ndio maadili
mema,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa IPA tawi la Pemba,
aliwasisitiza watumishi hao, kuwa makini kwenye mafunzo, ambayo ni sehemu ya
uthibitisho wa kazi, baada ya ajira.
Akifungua mafunzo hayo, Afisa Utumishi wa Baraza la mji
wa Chake chake Abdalla Salim Abdalla, aliwaeleze watumishi hao kuwa, wanawajibu
wa kuzisoma na kuzijua sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Alisema, mara mtumishi anapoajiriwa haraka sana,
anatakiwa kuzitafuta na kuzisoma sheria zinazomuongoza, ili kujua haki na
wajibu wake kazini.
‘’Kama wenzetu wa IPA wakishirikiana na wizara zetu,
imeamua kuwakusanya na kuwapa elimu hii, ni jambo jema, na sasa ni wajibu wenu
muwe makini wakati wakufunzi wanawafundisha,’’alieleza.
Katika hatua nyinge, Afisa huyo Utumishi wa Baraza la mji
wa Chake chake Abdalla Salim Abdalla, alisema mtumishi wa umma lazima aelewe
kuwa, anaiwakilisha serikali kuu kwenye utendaji wake.
Hata hivyo amesema, mtumishi asipoweka mbele maslahi ya
tasisi yake na kuangalia zaidi mashali binafsi, anaweza kuzalisha changamoto
zisizo za lazima.
Akiwasilisha mada ya utekelezaji wa program ya utumishi
wa umma, mkufunzi kutoka ‘IPA’ Abubakar Nuhu, alisema ina lengo la kuleta
ufanisi, sehemu za kazi.
Alisema program hiyo, ipo kwa mujibu wa sheria na kanuni
za utumishi wa umma, hivyo ni wajibu kwa kila mtumisha na kwa nafasi yake,
kufanya juhudi za kuhakikisha inaleta ufanisi.
Hata hivyo mkufunzi huyo, amewataka watumishia hao,
kuzilinda nyaraka za ofisi zao, kwani ndio roho ya kila tasisi na kinyume chake,
ni kutoa siri za serikali.
Kwa upande wake mkufunzi Khamis Nassor Salim,
akiwasilisha mada ya uzalendo na umuhimu wake kwa taifa, alisema ni jambo
ambalo, linatakiwa kuwa ndani ya moyo wa mtumishi mwenyewe.
‘’Hili suala la uzalendo, linakwenda sambamba na imani na
huruma zaidi, sasa hapa tunasomeshana lakini kila mmoja atajipima mwenyewe,
kama yuko chini kiuzalendo azidishe, kwani ni chachu ya kufikia maendeleo ya
kweli.
Katika mafunzo hayo ya siku tatu, mada 10 zitawasilishwa
ikiwa ni pamoja na rushwa na athari zake, huduma za ZSSF, uzalendo, sheria na
kanuni za utumishi wa umma, afya na usalama kazini na maadili ya utumishi wa
umma.
Mwisho
Comments
Post a Comment