NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
HATIMAE
mahakama maalum ya kupambana na makosa ya udhalilishaji Mkoa wa kusini Pemba, imemswekwa
chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 10, mshitakiwa Khamis Juma Chumu ‘soda’ (76) mkaazi wa Mtoni Chake Chake, baada
ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 13.
Hakimu wa mahakama hiyo Muumini
Ali Juma, alisema kati ya adhabu hiyo, mshtakiwa atatumikia chuo cha mafunzo
miaka 10 kwa kosa la ubakaji wa
mtoto huyo.
Akisoma hukumu hiyo, alisema
upande wa mashtaka ulifanikiwa kuwasilisha mashahidi watano kwenye kesi hiyo,
akiwemo mtoto mwenyewe, ambae alitosha kwa kiwango kikubwa, ushahidi wake
kuishawishi mahakama.
Alisema, mtoto ndio shahidi
mkuu anayepaswa kuihakikishia mahakama kuwa, alibakwa na kutorosha ama laa, na
sio mtu mwengine yeyote.
Hakimu huyo akiendelea
kusoma hukumu hiyo alisema, wakati mtoto huyo wa miaka 13 anatoa ushahidi wake
mahakamani hapo, akiongozwa na wakili wa serikali Ali Amour Makame, alieleza
kwa kina, namna alivyobakwa na mzee ‘soda’.
Alisema katika ushahidi wake
kuwa, kwanza aliitwa ndani ya babu huyo, kwa lengo la kumtuma dukani, ingawa
kumbe dhamira ilikuwa ni kumbaka.
Mtoto huyo alisema, alitii
agizo la kwenda ndani ya nyumba anayoishi mzee huyo, kwani ni mtu aliyemzoea na
hakuwa na wasi wasi wowote.
‘’Alinibaka juu ya kitanda
anacholala na kisha alivaa taula baada ya kuniabaka babu Khamis soda
(mshitakiwa),’’ndivyo hakimu alivyonukuu sehemu ya ushahidi mkuu wa mtoto huyo.
Hata hivyo Hakimu Muumini
Ali Juma, alisema hata ushahidi wa askari mpelelezi wa kituo cha Polisi Madungu
Chake chake, ulikuja kuunga mkono ushahidi wa mtoto huyo, na haukuacha chembe
cha shaka.
Katika hatua nyingine Hakimu huyo alisema,
ushahidi wa upande wa utetezi, haukuvuruga wala kutia doa ushahidi
uliowasilishwa wa upande wa mashtaka.
Kabla ya hukumu hiyo, wakili
wa utetezi Abied Mussa Omar, aliomba mahakama hiyo kuzingatia umri wa mzee
huyo, na kumpunguzia adhabu.
Alisema mzee huyo, anafaa
kupunguziwa adhabu kwanza umri wake, pili bado anayofamilia kubwa inayomtegemea,
ili kuiendeleza kihuduma.
Ingawa upande wa mashataka
uliokuwa ukiongozwa na wakili wa serikali Ali Amour Makame, aliiomba mahakama
hiyo kutoa adhabu kali, kwa mshtakiwa huyo.
‘’Makosa haya kwa watoto
sasa yamekuwa janga, ndani ya jamii, hivyo sasa tayari kila upande
umeshatekeleza wajibu wake, ni kazi ya mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa
sheria,’’aliomba.
Awali ilibainika mahakamani
hapo kuwa, mtuhumiwa huyo Khamis Juma Chumu ‘soda’ (76) mkaazi wa Mtoni
wilaya ya Chake chake, alimtorosha mtoto wa kike miaka 13, wakati akienda kuchota
maji mferejini, na kumpeleka nyumbani kwake.
Kufanya hivyo ni kosa,
kinyume na kifungu 113 (1) (a) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018,
sheria ya Zanzibar.
Kosa la pili ni la ubakaji, ambalo
alilifanya Mei 15, mwaka huu, ambapo alimmbaka mtoto huyo ndani ya nyumba
anayoishi majira ya saa 4:15 asubuhi, eneo la Mtoni wilaya ya Chake chake.
Kufanya hivyo ni kinyume, na
kifungu 108 (1), (2) (e) na kifungu cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu nambari 6
ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment