NA HAJI
NASSOR, PEMBA
KITUO cha
Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ kimesikitishwa na kitendo cha baadhi ya baba
wazazi, walezi na waalimu wa madrassa, kuwafanyia vitendo vya ukatili na
udhalilishaji watoto walio na mamlaka nao.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kituo hicho Harusi Miraji Mpatani,
kwenye maelezo yake yaliotolewa na Mratibu wa kituo hicho Pemba Safia Salehe
Sultan, kwenye kongamano la kuelekea siku 16 za kupinga ukatili, lililofanyika
Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake.
Mkurugenzi huyo alisema, katika utafiti wa miezi tisa, uliofanywa
na Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, watu 182
walifanyia usaili ili kupata taarifa hizo.
Alisema, kati ya watu hao
wanawake 115 na wanaume walifikiwa 67 kutoka kisiwa cha Unguja na Pemba, ambapo
moja ya malengo ya utafiti huo ni kufichua kesi zilizo jificha kutokana na
muhali na mkwamo katika ngazi za chini mpaka kufikia muafaka wa kesi husika.
Alieleza kuwa, ameshtushwa na kubainika
kwa baba wazazi 13, waliowafanyia ubakaji watoto wao wa kuwazaa, ambapo kati ya
hao tisa (9) Unguja na watatu (3) wakiripotiwa kisiwani Pemba.
Mkurugenzi Harusi alieleza kuwa, jengine
ambalo ZLSC katika siku hizi 16 za kupinga ukatili linawasikilitisha ni kuwepo
kwa akina baba walezi na kambo 25, Unguja wakiwepo 13 na Pemba 12 waliowaba
watoto wao wa kuwalea.
‘’Elimu inatolewa na serikali na hasa
tasisi ZLSC, ZFELA na TAMWA na nyingine, lakini sasa ninapoona matokea ya
utafiti huu wa miezi tisa uliofanywa na wenzetu TAMWA, inauma sana,’’alisema
Mkurugenzi.
Katika hatua
nyingine Mkurugenzi huyo wa ZLSC ameendelea kuitahadharisha jamii, kuwatumia
wanganga wa tiba za asili ambao, kwani baadhi yao hukosa uaminifu
wakati wanapoendesha tiba zao.
‘’Hata kwenye utafiti huu, jumla ya matukio
10 ya udhalilishaji yaliripotiwa kufanywa na waganga wa kienyeji, ambapo Unguja
yalikuwa sita (6) na Pemba manne (4), wakifanyiwa watoto,’’alieleza.
Aidha Mkurugenzi huyo wa
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC Harusi Miraji Mpatani, amewatadharisha
wasaidizi wa sharia waliomo majimboni, kutojiingiza kwenye sulhu ya kesi hizo.
Mratibu wa ZLSC Pemba Safia Saleh Sultan, alisema
Kituo kitaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kufika mahakamani kutoa ushahidi,
ili jamii ionea faida.
‘’Mahakama inawategemea wananchi
waliosikia, kuona au kuambiwa jambo wafike mahakamani kutoa ushahidi, sasa kama
bado wanakimbia, hakuna kesi itakayotiwa hatiani,’’alieleza.
Hata hivyo Mratibu huyo, aliendelea
kuisisitiza jamii kuzitumia siku 16 za ukatili, ili kujua wajibu wao hasa
yanapotokezea matendo hayo, ndani ya jamii husika.
Kwenye kongamano hilo Hakimu wa mahakama maalum ya kupambana na
udhalilishaji Muumii Ali Juma, alisema wakati umefika sasa kwa jamii kufanya
uamuzi wa kuyatokomeza matendo hayo.
Akifungua kongamano hilo, Msaidizi Kamishna wa Jeshi la Polisi mkoa
wa kusini Pemba Cyprian Mushi, alisema kila mmoja akitekeleza wajibu wake,
matendo hayo yatakoma.
Mwenyikiti wa kamati ya kuelekea siku 16 za kupinga ukatili na
udhalilishaji Nassor Bilali Ali, alisema lazima jamii ikae chini na kufikiria
upya, suala la kuwa na malezi ya ushirikiano.
Alieleza kuwa, kama yapo mambo jamii wanashirikiana mfano harusi,
msiba na hivyo hivyo utamaduni huo uhamishiwe kwenye malezi ya pamoja.
Wakichangia kwenye kongamano hilo, washiriki hao akiwemo sheikh
Abdalla Nassor Mauli, alilipongeza Jeshi la Polisi, kwa kubadilika katika
utendaji wao wa kazi.
Nae Fatma Maulid Kassim kutoka kituo cha mkono kwa mkono wilaya ya
Chake chake, alipendekeza kuwa, kama wapo wazazi, walezi na watu wengine
wanakataa kutoa ushahidi, sheria ichukue nafasi yake.
‘’Hiwezekani serikali na wanaharakati hawalali usiku na mchana
katika mapambano ya ukatili na udhalilishaji, kisha mwengine anaejua kila
jambo, ashindwe kuvisaidia vyombo vya sheria,’’alieleza.
Kongamano hilo, ni sehemu ya shamra shamra za kuelekea kilele cha
maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, ambapo makongamano
kama hayo yamefanyika wilaya zote za Pemba.
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ambacho
kimeanzishwa mwaka 1992, malengo yake makuu ni pamoja na kutoa msaada wa
kisheria, kwa wazanzibar bila malipo, ushauri, na elimu ya kisheria kwa watu
hasa maskini.
Mwisho
Comments
Post a Comment