NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
WANAUME katika wilaya ya Micheweni
mkoa wa kaskazini Pemba, wameonywa tabia ya kupiga wake zao, hasa wenye
ujauzito, kwani wanaweza kusababisha madhara kadhaa ikiwemo ulemavu kwa watoto
tarajiwa.
Kauli hiyo
imetolewa na wanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu kisiwani Pemba, wakati
wakizungumza na mwandishi habari hizi, baada ya kumaliza ziara ya kuishajihisha
jamii, utekelezaji wa haki za watu, wenye ulemavu.
Walisema
wakati mwengine, watoto huanza kuupata ulemavu tokea wakiwa tumboni mwa wazazi
wao, inayosabishwa na madharaka mengi, ikiwemo vipigo.
Mwanaharakati
Aisha Hilai Hassan alisema, baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwageuza ngoma wake
zao, kwa kuwashushia vipigo hata kama wanaujauzito.
Alisema,
katika wilaya walizozipitia, wamegundua kuwa Micheweni kuna malalamiko mengi,
ambayo wanawake waliwaeleza wakati walipokuwa, wanazungumza nao.
‘’Inawezekana
wanaume wanadhani kila aina ya ulemavu mtoto huzaliwa nao kwa asili yake, kumbe
upo mwengine husababishwa kwa wanawake, kupigwa wakiwa wajawazito,’’alisema.
Nae Mwanaidi
Iliyasa Hassan alisema, wakati wanawake wanazungumza nao, walisema wapo ambao
sio kuzaa mtoto mwenye ulemavu pekee, wengine wameharibu pia ujauzito.
‘’Mwanamke
anakuambia anapigwa wakati mwengine kwa kuchelewa kupika, au kuongeza ama
kupunguza chumvi kwenye chakula huku akiwa na ujauzito,’’alifafanua.
Mmoja kati
ya wanawake ambae alizaa mtoto mwenye ulemavu wa akili, akidai ilitokana na
kipigo mkaazi wa Shumba mjini, alisema kesi hiyo aliifikisha kituo cha Polisi
Micheweni.
Alisema,
alipigwa na mume wake kwa sababu ya kuchelewa kurudi kwa mama wake mkwe, huku
akiwa na ujauzito wa miezi minne, na hadi leo mtoto wake anaulemavu wa akili.
‘’Madaktari
walisema sio rahisi kuwa ningeweza kujifungua salama, ingawa nilifanikiwa
hivyo, lakini hadi sasa mtoto anamiaka 11 anaonekana na ulemavu wa
akili,’’alieleza.
Kwa upande
wake Mwanakhamis Yakouti Juma, aliwataka wanawake wenzake, ni vyema kuisamehe
ndoa, lakini wanapopigwa wapeleke taarifa vituo vya sheria.
‘’Wapo
wanawake wanapigwa, na kisha hukaa kimnya na wakati wa kujifungua hupata shida
hadi wengine kupoteza mtoto au kuzaa akiwa na ulemavu,’’alisema.
Mkuu wa
wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, amekuwa akirejea kauli yake ya kuwataka
wanawake kutoa taarifa wanaponyanyaswa ama kudhalilishwa.
‘’Kama
mwanamke unapata madhila na kisha unakaa kimnya, itakuwa huipendi afya yako,
njooni hata ofisini kwangu mtoe taarifa,’’alisema.
Mjumbe wa kamati tendaji ya Jumuiya ya
wanawake wenye ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’ Hidaya Mjaka Ali, alisema pamoja na
kwamba ulemavu ni kudura ya Muumba, lakini kama yupo anayechangia, lazima
sheria ichukue mkondo wake.
Mjumbe wa
baraza la taifa la watu wenye Ulemavu Zanzibar Mashavu Juma Mabrouk, amewataka
wanawake kisiwani Pemba, wanaopata madhila kuhakikisha wanatoa taarifa maeneo
husika.
Taarifa ya
kihalifu Jeshi la Polisi Tanzania ya mwaka 2020, imeibua wanawake 636 waliopigwa
na watu mbali mbali, na wengine 1,963 waliojeruhiwa katika matukio mbali mbali
nchini kote.
Mwisho
Comments
Post a Comment