NA HAJI NASSOR, PEMBA
WATU
wenye ulemavu uziwi kisiwani Pemba, wameomba kuwekewa wakalimani wa lugha ya
alama, kila aina ya kipindi au taarifa yoyote, inayohusu elimu ya Ukimwi, ili
iwe rahisi kwao kufuatilia kwa ukaribu.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi, kuelekea siku ya Ukimwi duniani Disemba 1, walisema bado elimu ya
kujikinga na vurusi vya ukimwi kwa kundi lao, hijawafikia vizuri.
Walisema, tume za Ukimwi ile
ya Zanzibar na ya Tanzania bara, hazijaweka kipaumbele juu ya kuweka wakalimani
wanaporushwa vipindi, juu ya masuala ya Ukimwi.
Mmoja kati ya viziwi hao,
Omar Khamis Juma wa Ole, alisema wanakosa elimu kubwa ya kujikinga ama
mapambano ya virusi vipya ya Ukimwi, kutokana na kuachwa nyuma.
Alieleza kuwa, ijapokuwa
kupitia shirika la Utangaazaji Zanzibar ‘ZBC’ kuna baadhi ya vipindi kunawekwa
wakalimani, lakini bado sio vipindi vyote.
‘’Tunataka kila kipindi,
hutuba, tangaazo au wito unaogusa suala la Ukimwi, VVU, unyanyapaa au dawa za
kufubaza maisha ARVs basi, kuweko na makalimani ili, kupata elimu hiyo kwa
upana,’’alieleza.
Khadija Mcha Haji wa Kangagani
wilaya ya Wete, alisema hata kwenye makongamano, mikutano na hata kilele cha
maadhimisho ya siku ya Ukimwi, hakujazingatiwa uwepo wa mkalimani.
‘’Elimu ya Ukimwi, sisi
viziwi kwetu ni shida mno, maana hakuna wakalimani wa lugha yetu ya amala, sasa
inakuwa vigumu, kuwa na taarifa kwa upana,’’alieleza.
Nae mtoto mweye uziwi Sara
Issa Khamis wa Machomane Chake chake, alisema kwa wao wanaoishi kando ya mji,
wamekuwa hata mara moja moja, hukosa kuona ukalimani wa elimu ya Ukimwi.
Hivi karibuni akizungumza
kuelekea siku ya wakalimani, Katibu Mkuu wa jumuia ya wakalimani wa lugha ya
alama Zanzibar ’JUWALAZA’ Kheir Mohamed Siamai, aliitaka jamii, kujiunga na
jumuiya hiyo, ili kujifunza lugha ya alama, ili kukidhi haki ya mawasiliano,
kwa watu wenye ulemavu wa uziwi.
Alisema, bado jamii haijaona
umuhimu, wa kujifunza lugha ya alama, na kuwasaidia viziwi katika mawalisiliano,
hasa juu ya kujikinga na maradhi, kadhaa ukiwemo Ukimwi.
Alifahamisha kuwa, kundi la
viziwi katika jamii ni sawa na kundi jengine lolote, ambalo linahaki ya
kuwasiliana baina yao na kundi jengine, ingawa wao ni kwa kutumia lugha ya
alama.
‘’Mawasiliano ya viziwa ni
maalum, hivyo kila mmoja ana haki ya kuhakikisha anawasiliana nao, ili kutumiza
utu na ubinadamu, lakini jambo la kwanza ni kujifunza lugha ya
alama,’’alieleza.
Kwa upande wake Mjumbe wa
Jumuiya hiyo kisiwani Pemba, Asha Suleiman alisema, bado lazima mkazo uwekwe na
serikali katika kuona kundi hilo, linapata elimu ya masuala mbali mbali ukiwemo
Ukimwi na njia za kujiepusha.
Afisa Mdhamini wizara ya
Makamu wa Kwanza rais Pemba Ahmed Abubakar Mohamed, amesema marekebisho yajayo
ya sheria ya watu wenye ulemavu, yanatarajiwa kulazimisha uwepo wa wakalimani
kwa vipindi vyote.
Mkataba wa kimataifa wa haki
za watu wenye ulemavu Ibara ya 21 (b) inaeleza kuwezesha matumizi ya lugha ya
alama, maandishi ya braille kuongoza na kuweka mawasiliano mbadala kwa njia
nyingine na mfumo wa mawasiliano watakaoamua.
Aidha sheria nambari 9 ya
mwaka 2016 ya haki na fursa ya watu wenye ulemavu Zanzibar kifungu cha 15, ni
lazima mawasiliano kwa watu wenye ulemavu utolewe kwa njia mbali mbali, ikiwemo
la nukta nundu na lugha ya alama.
mwisho
Comments
Post a Comment