NA HAJI NASSOR, PEMBA::
MAHAKAMA maalum ya kupamba na makosa ya
ukatili na udhalilishaji mkoa wa kusini Pemba, imesema kesi za udhalilishaji
zinazowahusu watoto wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 17, ndio pekee
zinazowatesa wao na ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, kwa kule kukataa kutoa
ushahidi.
Kauli hiyo,
imetolewa na Hakimu wa mahakama hiyo Muumini Ali Juma, wakati akitoa ufafanuzi
wa baadhi ya masuali yalioulizwa na wananchi, kwenye kongamano la kuelekea siku
16 za kupinga ukatili, lililofanyika Kiwanda cha Makonyo Wawi.
Alisema, mara
matukio hayo yanapotekezea kwenye jamii, wazazi wao huwa na ari, kasi na hamu
ya kuyafikisha mbele ya vyombo vya sheria, ingawa baada ya muda, hawaonekani
mahakamani.
Alisema, na
hasa kesi za aina hiyo zinazowaweka njia panda ni zile zinazowakabili watoto
wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17, ambao kimatendo ni watu wazima.
‘’Hao
wanaobahatika kufika mahakamani, basi wakati wa kutoa ushahidi hueleza kuwa,
wale watuhumiwa waliodai kuwabaka hawawajui, na kuiacha njia panda mahakama na
upande wa mashtaka,’’alisema.
Aidha Hakimu
huyo alisema, suala la kufika mahakamani kutoa ushahidi, ni njia moja muhimu na ya haraka
katika kuyapunguza ama kuyaondoa matendo hayo.
Akifungua kongamano
hilo, Msaidizi Kamishna wa Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba Cyprian Mushi,
alisema kila mmoja akitekeleza wajibu wake, matendo hayo yatakoma.
‘’Kwa mfano
kama leo hii, asasi za kiraia zimeungana katika kuitisha kongamano hili, ambalo
kila mmoja atatoa maoni yake, na huwenda sulhu ya pamoja, ikapatikana,’’alieleza.
Mwenyikiti
wa kamati ya kuelekea siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji Nassor Bilali
Ali, alisema lazima jamii ikae chini na kufikiria upya, suala la kuwa na malezi
ya ushirikiano.
Alieleza kuwa,
kama yapo mambo jamii wanashirikiana mfano harusi, msiba na hivyo hivyo
utamaduni huo uhamishiwe kwenye malezi ya pamoja.
Mwakilishi kutoka wizara ya Jinsia, Wazee, Maendeleo ya wanawake na watoto Pemba, Omar Mohamed Ali, alisema wizara pekee ni vigumu, kumaliza vitendo hivyo.
‘’Sisi tupo
kama kutoa miongozo, sera na maelekezo kwenye mapambano dhidi ya udhalilishaji,
sasa lazima na wengine tushirikiane katika kuona, hili linafikia pahala pazuri,’’alieleza.
Mapema akiwasilisha
utafiti wa kihabari wa mapambano dhidi ya udhalilishaji kwa watu wa karibu, uliofanywa na Chama
cha waandishi wa habari wanawake Tanzania ‘TAMWA-Zanzibar’ mwanaharakati Safia
Saleh Sultan, alisema utafiti umegundua kuwa wapo baba wazazi 13, waliowabaka
watoto wao wa kuwazaa.
Aidha utafiti
huo umeibua, baba walezi 25, Unguja wakiwa 13 na na Pemba 12, ambao nao wamewabaka
watoto wao walezi, na kutumia nafasi yao vibaya.
Hata hivyo
mwanaharakati huyo alisema kuwa, wapo waalimu wa madrasa 20, Unguja na Pemba,
waliotuhumiwa kuwadhalilishaji wanafunzi wao.
Wakichangia kwenye
kongamano hilo, washiriki hao akiwemo sheikh Abdalla Nassor Mauli, alilipongeza
Jeshi la Polisi, kwa kubadilika katika utendaji wao wa kazi.
Nae Fatma
Maulid Kassim kutoka kituo cha mkono kwa mkono wilaya ya Chake chake,
alipendekeza kuwa, kama wapo wazazi, walezi na watu wengine wanakataa kutoa
ushahidi, sheria ichukue nafasi yake.
‘’Hiwezekani
serikali na wanaharakati hawalali usiku na mchana katika mapambano ya ukatili
na udhalilishaji, kisha mwengine anaejua kila jambo, ashindwe kuvisaidia vyombo
vya sheria,’’alieleza.
Nae mjumbe
wa sheha kutoka shehia ya Vitongoji Fatma Mohamed Ali na mwenzake Rizik Hamad
Ali, walisema kama kuna madaktari au watendaji wa Jeshi la Polisi, wanavizisha
kesi hizo, wachukuliwe hatua.
Hata hivyo
mjumbe wa kamati hiyo Khalfan Amour Mohamed, alisema mporoko wa maadili, rushwa
muhali na wazazi kukubali kuzimaliza kesi hizo nje ya mahaka, yanachangia
kuendelea kuweko.
Kongamano
hilo, ni sehemu ya shamra shamra za kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku 16
za kupinga ukatili na udhalilishaji, ambapo makongamano kama hayo yamefanyika
wilaya zote za Pemba.
Mwisho
Comments
Post a Comment