NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WATEJA
wanaotumia mashine ya kutolea fedha kwa njia ya kielektroniki ‘ATM-Machine’ ya Benki ya watu wa
Zanzibar PBZ, kituo cha Mtambile wilaya ya Mkoani Pemba, wameomba kuwekewa
kinga maalum, ili wasionekane na kila mtu, wanapofanya muamala.
Walisema kwa sasa, licha ya kuwepo kwa mashine hiyo, ambayo
imewapunguzia mafasa ya zaidi ya kilimita 10 kwenda Mkoani, lakini haja ya
kujengwa kwa kinga, inahitajika.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema mashine
hiyo iko wazi na kila mmoja, anaweza kuona wakati mteja anapofanya muamala.
Himid Hija Mjaka wa Mwambe, alisema kukosekana kwa kinga
(kibanda) kwenye mashine hiyo ya ‘ATM’ imekuwa ikiwawiya vigumu, wengine
kutumia huduma eneo hilo.
‘’Ukitoa fedha kila mmoja anakuona mubashara ‘live’
hivyo unaweza kuwashawishi wahalifu, mana wanaona kila kitu
unachokifanya,’’alisema.
Nae Asha Abdalla Abdi wa Kangani, alisema juzi alitaka kufanya
muamala wa kutoa fedha, lakini kutokana na kuwepo kwa vijana wengi, alishindwa.
‘’Unajua mashine hii iko pazuri, maana kati kati baina ya sisi
watu wa Mwambe, Kigope, Wambaa, Kangani na Mtambile, lakini kwa sasa iko wazi,
vijana wanakuangalia unapoingia kibandani,’’alifafanua.
Kwa upande wake Mwajuma Haji Hassan wa Mizingani na Fatma
Mbarouk Haji wa Mtambile walisema, ni vyema kwa uongozi wa PBZ, ukaharakisha
ujenzi wa kinga kwenye kibanda chao.
‘’PBZ ijenge kitu mfano kama kioo au mlango, ambao hautoruhusu
aliyeko nje kumuona aliyeko ndani, nini anafanya, ili isiwe sababu ya
kufuatiliwa,’’alieleza.
Kwa upande Meneja wa PBZ tawi la Chake chake Mohamed Shehe,
alikiri kukosekana kwa kinga hiyo, na kusema mpango wa kujenga upo.
Alisema, walichokifanya ni kuharakisha uwepo wa huduma hiyo
kwa hatua za awali, na kisha shughuli nyingine zitafuta ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa kinga hiyo.
Alieleza kuwa, pamoja ujenzi wa kinga hiyo, lakini chengine
kitakachofuata ni kuweka alama ya utambuzi wa mashine, matangaazo na maelekezo
mengine.
‘’Tulichokifanya ni kuwapatia wananchi huduma za haraka, na
ujenzi wa mambo mengine yatafuata hatua kwa hatua,’’alieleza.
Benki ya watu wa Zanzibar ‘PBZ’ kisiwani Pemba, kwa sasa inazo
mashine nane (8) za kielektroniki za kutokea fedha, zikiwa katika maeneo ya
Chake chake, Mkoani, Micheweni, Wete na Mtambile.
Mwisho
Comments
Post a Comment