IMEANDIKWA NA ZUHURA
JUMA, PEMBA
MWANAMKE
mmoja aliejulikana na jina la Tahiya Mbarouk Ali mwenye umri wa miaka 22 mkaazi
wa Kifundi Konde amefariki dunia baada ya kuanguka kwenye pikipiki katika eneo
la Konde Vilima Vitatu Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa, dada huyo kabla ya
kufikwa na umauti, alikuwa amepakiwa kwenye pikipiki na mume wake akitokea
Konde kwenda Wete na walipofika Vilima Vitatu alianguka na kuumia kichwa.
Walisema kuwa, sababu ya ajali hiyo ni kutokana na baibui la dada
huyo kuingia kwenye pikipiki hilo na kusababisha kuanguka, ambapo aliangukia
kichwa na kufariki.
Jirani wa dada huyo Saada Said alieleza kuwa, aliondoka
nyumbani kwake kwenda kazini Wete, ambapo alimwambia mume wake ampeleke, kwani
alikuwa ameshachelewa.
‘’Kwa kweli ni mitihani kwa sababu hivi karibuni mumewe alimgonga
mwanafunzi na kufariki na leo ameshapata ajali nyengine na mke wake
amefariki’’, alihadithia dada huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis alisema
ajali hiyo imetokea Juni 27 mwaka huu saa 1:30 mkaazi wa Kifundi Wilaya ya
Micheweni, ambapo dereva wa pikipiki mwenye namba za usajili DFPA 8083
iliyokuwa ikiedeshwa na Khalfan Salim Said mwenye umri wa miaka 37 akiwa
amempakia mke wake walianguka, baada ya nguo ya mama huyo kuingia kwenye spoki
ya pikipiki.
‘’Nguo hiyo ilipoingia kwenye spoki, pikipiki ilikukosa
mueleke na kusababisha kuanguaka na mwanamke huyo kufariki dunia, baada ya
ajali hiyo alikimbizwa katika hospitali ya Wete ambapo daktari alisema kuwa,
marehemu alianguka kwenye sakafu ya barabara na kuumia kichwa na hicho kikawa
ni chanzo cha kifo chake’’, alisema Kmanda huyo.
Aliwataka akinamama wanapopanda katika pikipiki au bodaboda
wahakikishe wanakunja vizuri nguo zao ili kuepusha hatari zinazoweza
kujitokeza.
MWISHO.
Comments
Post a Comment