TAMWA, Internews waungana kutaka sheria
mpya ya habari Zanzibar
NA HAJI NASSOR, PEMBA::-
‘’BILA ya kuathiri
sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo
yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari kupitia chombo chochote bila ya
kujali mipaka ya nchi’’.
‘’Tena pia mtu huyo ana uhuru wa
mawasiliano yake kutoingiliwa kati, na rai anayo haki ya kupewa taarifa wakati
wote kuhusu matukio ya nchini na duniani kote, ambayo ni muhumi kwa maisha yake’’.
Ndivyo
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inavyoelekeza kifungu cha 18 juu ya
upatikanaji na utoaji wa habari kwa raia, tena bila ya kujali mipaka ya nchi.
Mwanasheria
wa kujitegemea Khalfan Amour Mohamed, anasema suala la kupata habari, au kutoa
ni haki ya kikatiba, ambayo inatofautiana na haki nyingine.
‘’Ukitaka
kuzigawa haki hizi, basi zipo haki za kikatiba na haki nyingine zilizotengenezewa
sheria yake mbali mbali, mfano haki ya elimu,’’anafafanua.
Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwajali wananchi wake, haikuishia tu ndani ya Katiba
kifungu cha 18 ya upatikanaji wa habari, bali kwa kutambua umuhimu huo,
ilianzisha sheria maalum.
Ikumbukwe
kuwa, miundombinu ya kupashana habari ni Magazeti, redio na tv, ingawa na kwa
sasa kumeibuka mitandao ya kijamii.
Kwa Zanzibar,
vyombo vya habari vya magazeti vinasimamiwa na sheria ya Magazeti, Vitabu, na
Mawakala wa Habari nambari 5 ya mwaka 1988.
Igawa kwa
redio na tv na hata sasa uwepo wa vyombo vya habari mtandaoni, vyenyewe
vinasimamiwa na sheria ya Tume ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997.
SHERIA YA MAGAZETI,
VITABU NA MAWAKALA WA HABARI NO 5, 1988
Sheria hii
yenye vifungu 81 na sehem 10, sasa inatimiza miaka 34, tokea kutungwa kwake, na
kwa maana nyingine, vipo vifungu zaidi ya 40 ambavyo vyengine vinahitaji
kufutwa.
Vyengine
vikihitajika kufanyiwa marekebisho na vyengine vilivyobeba maneno makali kama ‘uwezo
wa waziri, waandishi kudhibitiwa na kufanya uchochezi’.
Kwenye
sheria hii ambayo kwa sasa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar kwa ufadhili wa Shirika la Internews, wanaharakishwa kufutwa,
vipo vifungu kadhaa mabavyo vimepitwa na wakati na kuwa na sheria mpya.
VIFUNGU KANDAMIZI KWA UHURU WA HABARI
ZANZIBAR
Moja ya
kifungu ambacho kwa sasa wadau wanataka kifutwe, ni cha 39 ambapo chenyewe
kinaeleza ‘sharti la kukusanya na kutoa habari na vifaa vya habari’.
Kifungu
kimeanza vizuri, kuwa hakuna mtu
atakayepewa kibali cha maandishi cha kukusanya habari, isipokuwa awe (i) mwandishi
wa habari wa ndani au (ii) mwandishi huria wa habari.
Lakini
kifungu cha (3) kikatoa haki kwa mkono wa kulia na kupokonya kwa mkono wa
kushoto, kwa muathirika wa kibali hicho (mwandishi wa habari) kwamba anaweza
kukata rufaa.
‘’Muathirika anweza
kukata rufaa ya kuzuialiwa, kukataliwa, kufutwa kwa kibali chake moja kwa moja
wa Waziri wa habari ndani ya wakati,’’kinafafanua kifungu.
Kifungu cha
(4) ambacho kinapokonya haki hiyo, kinaeleza kuwa ‘kila uamuzi wa waziri kuhusiana
na rufaa ya mwandishi wa habari, utakuwa ni wa mwisho na hautafanyiwa mapitio
(haukatiwi rufaa) na mhakamani’.
Kwamba iwapo
waziri amemkatilia mwandishi wa habari kumkosesha kibali, kukifuta, kukizuia au
kukikataa uamuzi wake huo utakuwa wa mwisho.
Lakini hata mazonge mengine ya sheria hii yapo kwenye kifungu cha 40, kinachoelezea uwezo wa waziri wa Habari wa kufuta kibali kilichotolewa na Mkurugenzi.
Kwamba
mwandishi wa habari ameshaomba kibali kwa Mkurugenzi, ameshalipa ada
itakayopangwa, lakini sheria inampa uwezo Waziri kukifuta kibali hicho.
‘Waziri
anaweza kufuta kibali kilichotolewa na Mkurugenzi ikiwa kwa maoni yake tu,
ufutaji huo utakuwa ni kwa maslahi ya umma au ni kwa maslahi ya usalama na
utangamano wa taifa’
Kwamba
sheria hii, imempa uwezo wa kupitiliza Waziri, na kwamba anaweza, kufuta kibali
kwa maoni yake tu, akihisi kukifuta huko, kwa faida kwa taifa.
WADAU WA HABARI WANASEMAJE?
Mdhamini wa
Baraza la Habari Tanzania MCT-Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema sheria hiyo
imeshapitwa na wakati na moja ya vifungu vibaya ni cha 39 na 40.
‘’Haiwezekani
suala la haki ya kikatiba ya kupata na kutoa habari, apewe uwezo wa kupindukia
waziri, juu ya kuona nani apewe au asipewe kibali,’’anasema.
Mchambuzi wa
sheria za habari Zanzibar Hawra Shamte anasema, kwenye nchi ya utawala wa sheria
na demokrasia kama ilivyo Zanzibar, sheria hiyo vifungu vyake kadhaa
vinapingana na katiba ya nchi.
‘’Iweje kuwe
na sharti la kukusanya habari, tena moja ya sharti hilo uwe na kibali ambacho
hakitolewi na kamati wala bodi anatoa mtu mmoja,’’anaelezea.
Anasema
maajabu mengine ambayo yamo kwenye sheria hiyo ni kifungu cha 40, ambacho
kimempa uwezo mkubwa waziri, juu ya kukubali ama kukataa kutoa kibali.
‘’Kinachoonesha
udhaifu kuwa, hata mwandishi akikataliwa na waziri kuwa hawezi kuomba kibali,
hapo ndio mwisho wa kulalamika,’’anafafanu.
Kwamba
uamuzi wa waziri hauwezi kukatiwa rufaa katika mahakama yoyote na hata
mwandishi hawezi kumshtaki waziri huyo wa kiongozi wa nchi aliyemteua.
Aliyekuwa
mkuu wa Chuo cha uandishi wa habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar ‘ZJMMC’ Dk.
Saleh Yussuf Mnemo, anasema ujio wa mapinduzi ya habari ya kidigitali, suala la
kibali halipo.
‘’Wanachotakiwa
mamlaka ni kufuatilia utendaji wa kazi wa waandishi wa habari na watoa taarifa,
lakini sio kuwabana na kuwawekea sheria ngumu,’’anasema.
Katibu mkuu
wa klabu ya waandishi wa habari Pemba ‘PPC’ Ali Mbarouk Omar, anasema vifungu ambavyo
vinampa uwezo waziri, ni dhahiri vinapingana na katiba.
‘’Muda wa
kuwa na sheria unaotaja cheo cha mtu umepita, maana unaweza kuwakosesha
wananchi kupata habari, kwa kule waziri, kumchukia mwandishi wa habari tu,’’anasema.
Mhariri
mtendaji wa shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar, Ali Haji Mwadini anasema,
ukuaji wa maendeleo ya taifa lolote hutegemea mno, uwepo wa waandishi huru wa
habari.
‘’Kama bado
kuna sheria inaelekeza kuwa waziri anaweza, mkurugenzi akiona, kwa maoni
yake au akihisi hiyo sio demokrasia,’’anasema.
WAANDISHI WA HABARI WANASEMAJE?
Abid Juma
Suleiman, mwandishi wa habari wa shirika la Magazeti Pemba, anasema sheria hiyo
ya Magazeti, Vitabu na Mawakala wa Habari nambari 5 ya mwaka 1988, imekuwa
kikwazo kwao.
‘’Ilishawahi
kuwakumba waandishi wa habari wa vyombo binasfi kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Chambani Mkoani Pemba, kwa kukoseshwa vibali,’’anasema.
Mwandishi wa
habari wa kituo cha tv na redio cha Zenj fm Is-haka Mohamed Rubea, anasema
sheria hiyo hasa kwenye upatikanaji wa kibali, imekuwa shida.
Mwandishi wa
redio Jamii Mkoani Said Omar Said, anasema sheria yenye vifungu kandamizi,
huwaumizi zaidi waandishi wa vituo binafsi.
NINI KIFANYIKE?
Mkurugenzi
wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzur Issa Ali, anasema ujio wa sheria mpya ya habari,
vifungu vinavyompa uwezo mkubwa waziri vifutwe.
‘’Lakini
napendekeza kama habari ni haki ya kikatiba, sharti la kutoa kibali lisiwemo
mikononi mwa mtu, bali iwe ni bodi ya ushauri wa habari,’’anapendekeza.
Mchambuzi wa
sheria za habari Zanzibar Hawra Shamte, anasema maneno kama ‘uwezo
wa Mkurugenzi, Waziri, akiona inafaa, akihisi, kwa maoni yake’ kwenye
sheria mpya ya habari yasitumike.
‘’Sote
tunakubali kuwa kila mmoja anamapungufu yake, sasa kama waziri wa habari,
akipewa uwezo mkubwa wa kukubali au kukataa kibali, itafika wakati Zanzibar
kusiwe na waandishi wa habari,’’anaeleza.
Mratibu wa uchechemuzi
wa upatikanaji wa sheria ya habari Zanzibar kutoka TAMWA-Zanzibar Muhammed
Khamis, anasema, wakati umefika Zanzibar kuwa na sheria rafiki.
‘’Ndio maana
TAMWA-Zanzibar kwa kushirikiana na wafadhili wetu shirika la Internews, tunaomradi
wa miezi minne, ili kuwawezesha waandishi kusukuma upatikanaji wa sheria mpya
habari Zanzibar,’’anasema.
Mwandishi wa
kituo cha redio cha Sauti ya Istqama Salim Ali Msellem na mwenzake wa tv ya
mtandaoni jicho letu Amina Ahmed, wanasema rufaa ya kukataliwa, kufutiwa kibali
isiishie kwa Waziri kama ilivyo sasa.
‘’Suala la
habari ni la kikatiba, basi ieleze wazi kuwa waziri akifuta, akikataa kutoa
kibali muathirika, sheria ielekezea hadi afike mahakamani,’’anasema.
WANANCHI WA KAWAIDA
Asha Ali
Haji mwenye ulemavu wa viungo wa Mtambile, anasema, waandishi wanapowekewe vikwazo
kwenye kukusanya, kutafuta na kuandika habari waathirika ni wao wa chini.
Hemed Haji
Omar wa Wambaa Mkoani anasema, sheria kandamizi kwa waandishi wa habari ni ukiukwaji
wa haki za binadamu.
Mwisho
Comments
Post a Comment