IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
JAMII
imetakiwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi zima la ufundishaji
na ujifunzaji kuanzia kwenye ngazi ya familia kwa kuwasaidia watoto na
kumtengenezea mwanafunzi mazingira rafiki ya kujifunza kwa urahisi.
Hayo yameelezwa na Meneja Mwandamizi wa Uratibu na Programu katika
mradi wa Boresha Elimu ya Sekondari Zanzibar, John Masenza katika mafunzo ya
kuwajengea uwezo walimu wa Hesabati, Sayansi na Kiengereza.
Alisema kuwa, ikiwa jamii itashiriki kikamilifu katika ufundishaji
na ujifunzaji itasaidia wanafunzi kupata maarifa kwa urahisi hususani katika
masomo ya Hesabati, Sayansi na Kiengereza ambayo kwa sehemu kubwa yameonekana
kuwa na changamoto kwa elimu ya Sekondari.
“Mradi huu tunautekeleza Zanzibar na tunakududia kuwafikia
walengwa 220,000 wakiwemo walimu, wanafunzi, kamati za skuli, wakaguzi na wadau
wengine wa vituo vya walimu kwenye HUB”, alisema Meneja huyo.
Alisema kuwa, katika kufanikisha malengo ya mradi wanakusudia
kuboresha uwezo wa walimu wa Sekondari katika kutekeleza mtaala unaolenga kwenye
ujuzi, uwezo na umahiri wa wanafunzi unaosaidia zoezi la ufundishaji na
ujifunzaji, ambao unatakiwa umlenge mwanafunzi zaidi.
Aidha alieleza kuwa, mradi unakusudia kuimarisha mifumo na
mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kuvijengea uwezo vituo vya walimu na
kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kufuatilia maendeleo au ubora wa elimu
kwenye skuli zinazoizunguka jamii.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Afisa Mdhamini Wizara ya
Elimu na Mafunzio ya Amali Pemba, Kaimu Mratibu Idara ya Mafunzo ya Ualimu WEMA
Mzee Ali Abdalla alisema, alilipongeza sana Shirika la good Neighbors kwa kutoa
mafunzo hayo, yenye lengo la kuboresha elimu ya Sekondari Zanzibar.
Alisema kuwa, kwa dunia ya leo mfumo wa elimu unaotakiwa ni wa
ujifunzaji kwa kuzingatia yanayofundishwa darasani yaendane na uhalisia katika
maisha, ili watakapomaliza kidato cha nne waweze kujua pakuanzia kutokana na
mbinu pamoja na ujuzi ambao wamefunzwa wakiwa skuli kwa miaka minne.
“Tunataka ufundishaji huu umguse kila mwanafunzi kwa kutumia
mbinu mbali mbali na ujuzi ili kufikia malengo, mtaala wa sasa tunapendekeza
kumfikia mwanafunzi na tunampa elimu ili aweze kuja kuakisi katika maisha ya
kawaida”, alisema.
Kwa upande wao walimu waliopata mafunzo (resources trainers)
hayo walisema kuwa, kupitia mafunzo hayo wanaamini kwamba wanafunzi
watabadilika na kuongeza ufahamu pamohja na kiwango cha ufaulu kwa masomo hayo.
Mwalimu wa skuli ya Sekondari Madungu Chake Chake Hasanati
Said Suleiman alisema, amejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kubaini kuwa
mwanafunzi anaweza kujifunza kwenye njia tofauti, mbali na ile waliyoizoea.
“Kuna hii teknolojia ya kujifunza lakini hatuitumii, kwa hiyo
katika mafunzo haya nimepata kujua kuwa teknologia ni kitu muhimu katika
kuwafunza watoto wetu”, alisema mwalimu huyo.
Aliishauri Wizara ya Elimu kujaza vifaa bora kwenye vyumba vya
maabara ambavyo vitawasaidia wanafunzi kufanya kwa vitendo sambamba na kujengwa
HUB mbali na skuli, ili kuepusha usumbufu kwa wanafunzi wakati wanapoendelea na
masomo.
Mwalimu wa skuli ya Sekondari Msuka Seif Juma Said alisema
kuwa, mafunzo hayo yatakuwa na tija kwa walengwa wote, kwani kupitia yeye
atafikisha ujumbe huo ambao hapo awali haukuwepo katika skuli hiyo.
“Mafunzo haya yana tofauti kubwa na yale tunayofundisha
kawaida, kwa sababu tuliamini kuwa mwalimu ndio anajua kila kitu na mwanafunzi
hakuwa na nafasi yeyote kwenye ufundishaji, lakini kumbe mwanafunzi ana mengi
anayoyafahamu na alipaswa atawale kwa asilimia 100”, alifafanua.
Mhadhiri wa chuo cha elimu kutoka UDOM Dk. Francis William ambae
alikuwa mkufunzi wa masomo ya hesabati alisema kuwa, lengo ni kuhakikisha
walimu wanajenga uwezo na umahiri mkubwa katika kuhakikisha wanafuata mtaala
ambao unahitaji walimu wanavyosaidia wanafunzi kujifunza, waweze kujenga mahiri
kwenye maeneo ya maarifa, stadi na mielekeo, ili kile wanachojifunza wakitumie
katika maisha yao ya baadae.
“Tumekuwa hapa kwa siku sita za kufundisha na tunatengeneza
resources trainers hivyo tutakuwa na wataalamu ambao wamebobea katika masomo
haya ya sayansi, hesabati na kiengereza”, alisema.
Mradi huo wa miaka minne unatekelezwa na Shirika la Good Neighbors
Tanzania chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Korea (Koica) ambao
unakusudia kuwafikia walengwa 220,000.
MWISHO.
Comments
Post a Comment