NA ZUHURA JUMA, PEMBA
SERIKALI
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imepanga kufanya sensa ya watu na makaazi,
ifikapo Agosti 23, mwaka huu wa 2022.
Sensa hufanyika kila baada ya miaka 10, na ya mwisho ni ile
iliyofanyika mwaka 2012, ambapo hii ya mwaka 2022 itakuwa ni ya sita kufanyika.
Zilizowahi kufanyika ni zile za mwaka 1967 kisha mmwaka 1978,
1988, 2002 na ile ya mwisho 2012.
Maana
ya Sensa ya Watu na makaazi
Ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathmini, kuchapisha
na kusambaza takwimu za kidemografia.
Lakini pia ni kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na
makaazi yao katika nchi kwa kipindi maalum.
Wapo wanaosema kuwa sensa ni zoezi maalumu lenye lengo la
kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahala wanapoishi na
hata hali yao ya elimu.
Takwimu hizo za msingi, ndizo zinazoanisha mahitaji halisi ya
wananchi yakiwemo makundi maalum, yenye mahitaji maalumu, kwa mfano watu wenye
ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee.
Watu
wenye ulemavu na sensa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Wilaya ya Chake Chake (ZANAB) Suleiman Mansour anasema, watanufaika
kwa sababu ni agizo la Serikali lenye lengo la kujenga.
Anasema, Serikali ni chombo ambacho kinahudumia watu wake kwa
idadi waliyonayo, hivyo wao watakaposhiriki zoezi hilo itajulikana idadi yao na
kuweza kutafutiwa mahitaji yao yanayotosheleza.
“Sisi ni watu wenye mahitaji maalum, Serikali ndio yenye
dhamana kwa watu kama sisi, hivyo bila kujua idadi yetu halisi watafanya kitu
kwa usahihi,’’anasema.
Anaamini serikali inapojua idadi ya watu, ni sawa na kujua
mahitaji ya binadamu, kwa hiyo ikiwa wazazi na walezi watawaficha watu wenye
ulemavu, watawakosesha haki zao za msingi.
Said Omar Said ambae ni Mwenyekiti wa Viziwi wilaya ya Chake
Chake anasema, sensa itasaidia watu wenye ulemavu, moja ni kujua idadi yao kamaili.
“Tutajulikana ni watu wangapi wenye ulemavu na tunahitaji kitu
gani, hivyo itakuwa ni rahisi kutatuliwa changamoto zinazotukabili”, anasema.
Anaishauri jamii kushirikiana pamoja, katika kuhakikisha
wanakuwa mstari wa mbele kushiriki zoezi la sensa kwa lengo la kufanikisha,
kwani ni muhimu katika maisha yao.
Sahia Seif Salum wa Jumuiya ya wasioona ‘ZANAB’ Chake Chake
anasema, sensa itawasaidia hata mgawanyo wa rasilimali elimu na afya.
Kubwa anasema ili kufanikisha hilo, sasa ni jukumu la wazazi
na walezi kuwafichua watu wenye ulemavu wakati utakapofika.
“Watu wenye ulemavu watakapojitokeza kwenye zoezi la sensa ya
watu na makaazi, sasa changamoto zetu ni kuzinyooshea njia
kumalizika,’’anasema.
Hafsa Yussuf Abdul-rahman mkaazi wa Kifumbikai Wete ambae ni
kiziwi anasema, watakapohesabiwa wanaamini kwamba changamoto zao nyingi
zitatatuka.
‘’Nasoma chuo cha Mwalimu Nyerere Chake Chake lakini sioni
huduma hata moja zinazotuwezesha sisi viziwi, nimezoea kumuangalia mwalimu
mdomoni tu, hivyo naamini hii sensa itakuja na suluhgisho,’’anaeleza.
Mratibu wa Baraza la Taifa la Watu wenye ulemavu Pemba Mashavu
Juma Mabrouk anasema, hana shaka bali senda itakuja na matokeo bora kwa watu
wenye ulemavu.
“Lengo ni kupata idadi
ya watu katika nchi na kuweza kuandaa na kupanga mikakati thabiti ya maendeleo,
hivyo watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii”, anasema.
Anazidi kuanisha faida ya sensa kwa kundi hilo, ni kuwa na
idadi kamili, kujua mahitaji yao ya msingi, aina ya ulemavu wao.
Kupitia sensa Serikali itajua kwamba wanahitaji vitimwendo vingapi
au kuna wasomi wangapi na hivyo hata katika masuala ya ajira wanaamini kwamba watapata
fursa ya kuajiriwa kutokana na idadi ya wasomi waliopo.
Mratibu huyo anaeleza kuwa, sensa itapunguza changamoto kwa
watu wenye ulemavu kwa sababu wataingizwa katika mpango wa maendeleo ya nchi,
jambo ambalo litasaidia kutapata mahitaji yao.
“Ikiwa watu wenye ulemavu watafichwa, hawatojulikana idadi yao
na wala hakutojulikana kwamba wana uhitaji wa vitu gani na gani, hivyo wanaweza
kukosa haki zao za msingi”, anaeleza Mratibu huyo.
Aziza Alawi Mussa ambae ni Mjumbe wa Shirikisho la Jumuia za
watu wenye Ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’
Pemba, anasema, walipewa taarifa katika Jumuiya yao, juu ya uwepo wa zeozi
hilo.
Kwa ngazi ya awali
tayari viongozi wao kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Jumuiya za watu
wenye ulemavu, wameingia kwenye maeneo ya kamati za wilaya mpaka mkoa na tayari
zimeshafanya kikao cha awali.
Anataja athari inayoweza kujitokeza iwapo watu hao hawakupata
fursa ya kuhesabiwa kuwa ni, Serikali haitakuwa na takwimu sahihi za kupanga
mipango yake ya kila siku.
Khalfan Amour Mohamed kutoka Jumuiya ya Watu wenye ulemavu wa
akili Zanzibar ‘ZAPDD’ anasema, sensa
inaweza kuwasaidia watu wenye ulemavu katika nyanja tofauti.
‘’Kwa watu wenye ulemavu ni kwamba, baada ya zoezi hilo serikali
itajua kuwa, katika nchi kuna watu wangapi wenye ulemavu na kujua aina ya
mahitaji yao,’’anasema.
Yeye anaona itakapofanyika
sense, Serikali itajua na itajipanga kuweza kuleta yale mahitaji maalumu ambayo
yamekuwa yakililiwa kwa siku nyingi na watu wenye ulemavu wa akili.
Jumuiya yao imejipanga kuhakikisha wanatoa elimu ya kuhamasisha,
watakutana na viongozi wa matawi ya Jumuiya zao ambapo kwa Pemba ni 30, ili
kuwaelimisha na wao wachukue juhudi ya kuwahamasisha wazazi na walezi.
Raya Mohamed Nassor mwenye ulemavu wa viungo anasema, ni
muhimu kwa watu wenye ulemavu kuhesabiwa kwani Serikali itaona kwamba wapo na
wanahitaji kutatuliwa changamoto zinazowakabili kwa mujibu wa idadi yao.
Halima Bakar Ali ambae ni mkaazi wa Wete anasema kuwa, sensa
ni muhimu sana kwa wananchi, kwani inaisaidia Serikali kupata taarifa za msingi
ambazo zitapelekea kuchapuza maendeleo katika nchi.
Ali Omar Ali mkaazi wa Ole Wilaya ya Chake Chake anasema, kuna
watu wenye ulemavu wengi ambao hawajajiunga na jumuiya zinazoshughulikia watu
hao, hivyo idadi yao halisi haijulikani.
‘’Watakapohesabiwa itajulikana kuna watu wa aina hiyo wangapi,
wanaosoma na wasiosoma wanagapi na ndipo Serikali itakapojua kunatakiwa kitu
gani cha kuwasaidia na idadi yake’’, anaeleza Ali.
Mkurugezi wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar
Ussi Khamis Debe amewasisitiza watu wenye ulemavu kuchangamkia zoezi hilo.
‘’Hakuna mahali ambapo sasa kuna taarifa rasmi juu ya idadi na
mahitaji ya watu wenye ulemavu, lakini ujio wa sense hii yam waka 2022, itakuwa
ndio suluhisho,’’anasema.
“Nitoe wito kwa wazazi na walezi pamoja na watu wenye ulemavu
kujitokeza kuhesabiwa na wasione kwamba ni mkosi au nuhsi hapana, hiyo ni
mitazamo potofu”, anaeleza.
Mkurugenzi huyo anasema, watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii
na ni sehemu ya wananchi wa Zanzibar, hivyo ni vyema wakajitokeza, wahesabiwa.
Sensa ni muhimu kwani husaidia kupata taarifa za idadi ya watu,
katika mamlaka za Wilaya kwenye utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo
huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye mgawanyo wa
rasilimali.
MWISHO.
Comments
Post a Comment