IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA.
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ‘ZSSF’ kisiwani Pemba, umekabidhi sadaka ya fedha taslim, kwa watoto yatima 60 kisiwani humo, kama sehemu ya maandalizi ya kusherehekea sikukuu, baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Akikabidhi sadaka hiyo kwa nyakati tofauti, Meneja wa ZSSF kisiwani humo, Rashid Mohamed Abdalla, alisema ZSSF inapaswa kuihudumia jamii, wakiwemo watoto waliokosa wazazi wao.
Alisema, ZSSF imeguswa mno na kundi la watoto hao, na dio maana imeamua kwa mara hii, kuacha kufutarisha makundi mengine na kuwapatia sadaka watoto hao.
Akiungumza katika ofisi za wilaya za Micheweni, Wete, Mkoani na ofisini kwao Chake chake, alisema ijapokuwa, sadaka hiyo ni ndogo, lakini itasaidia katika maandalizi ya sikukuu.
Alieleza kuwa, watoto hao ambao wamepoteza mmoja kati ya wazazi wao, au wote wawili, nao wanahitajia kupata furaha na chukula kizuri hasa kipindi cha sikukuu.
‘’Kwa msimu huu ZSSF makao makuu, imeamua kuacha kuyaita makundi mengine kwa ajili ya futari, na imeona bora kukutana na mayatima japo kidogo kila wilaya, ili kupata sadaka,’’alieleza,
Katika hatua nyingine Meneja huyo, amewaomba watu na mashirika mengine yenye uwezo, kuliangalia kwa karibu kundi hilo, ili kulisaidia kwa njia moja ama nyingine.
Hata hivyo aliwakumbusha waajiri kuendelea kufikisha michango ya wafanyakazi wao ZSSF, ambayo wakati mwengine, ndio hiyo inarudi kwa jamii
‘’ZSSF pamoja na wajibu wake wa kutoa mafao mbali mbali kwa wanachama, wake lakini pia imekuwa ikiihudumia jamii katika sekta mbali mbali, ikiwemo elimu na afya,’’alisisitiza.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Micheweni Saleh Mohamed Saleh, alisema sadaka hiyo sio ndogo, na itawasaidia kwa kiaisi kikubwa watoto hao na walezi wao.
Nae Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Chake chake Rashid Said Nassor, alisema watoto yatima wilayani mwake ni wengi, lakini hao waliokabidhiwa sadaka itawasaidia.
‘’Idara ya ustawi wa Jamii wilaya ya Chake chake inaupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF, kwa hatua ya kuwaona watoto, kwa matayarisho ya sikukuu,’’alieleza.
Nae Afisa Usajili wa ZSSF Msabaha Massod alisema, ZSSF itaendelea kuwa karibu na jamii kila siku, ili kuona wanaondokana na changamaoto kadhaa, iwe kwenye sekta ya elimu au afya.
Baadhi ya watoto hao, walisema hatua hiyo imewasaidia mno katika matayarisho ya sikukuu, na kuwaomba wengine, wenye uwezo kuwasaidia wenzao.
‘’Sisi watoto yatima kwa Pemba tupo wengi mno, sasa kama ZSSF imekusanya 60, na wengine wawasaidie kundi jengine, ili kila mmoja aishi kwa furaha,’’alisema Fatma Mohamed.
Hata hivyo watoto hao yatima, wameuomba Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF, kuendelea na utaratibu kila hali ya fedha itakaporuhusu.
Mwisho
Comments
Post a Comment