Skip to main content

JAA LA KIBELE ZANZIBAR LILIVYOGEUKA KISIMA CHA AJIRA

 

IMEANDIKWA NA ALI SULEIMAN, PEMBA

KIJIJI cha Kibele kipo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Zanzibar.

Kwa mujibu sensa ya watu na makazi ya 2012, kijiji hiki kina watu wasiopungua 3,000.

Wengi wao wanajishughulisha na kilimo.

Hapa ndipo lilipo jaa kuu la Unguja, ambalo linatumika kukusanyia taka zinazozalishwa majumbani, masokoni, madukani, barabarani na kwenye hoteli za kitalii.

Jaa hili lipo umbali wa mita 300 kutoka barabara kuu iendayo Wilaya ya Kusini.

Wastani wa tani 190 za taka mchanganyiko kama za plastiki, tairi mbovu, televisheni na majokovu yasiyofaa kwa matumizi, zinatupwa katika jaa hili kila siku.

Aidha hili ndio eneo linalotumika kuharibu dawa au vyakula visivyofaa kwa matumizi ya binaadamu.

Vingi ya vifaa vya elektroniki ninavyoviona katika jaa hili ni vile vilivyoingizwa kutoka ng’ambo kama biashara chakavu.

Eneo hili lina ukubwa wa zaidi ya mita 1,000 sawa na viwanja 10 vya mpira. Ukifika hapa, unapokelewa rundo la taka zilizotawanyika huku harufu kali ya uvundo ikihanikiza eneo lote.

Kama ni mtu mwenye roho nyepesi,ni vigumu kuvumilia harufu mbaya inayotoka katika jaa hili.

Mamia kwa maelfu ya nzi wanazaliwa kila dakika katika jaa hili ambalo haliko mbali na makazi ya watu na wadudu wapenda uchafu kama mende wanaoneka kwa wingi.

Ndege aina ya Kunguru na yange yange, wanaruka kutoka eneo moja hadi jengine la jaa kutafuta chakula, kwao ni eneo lenye chakula cha kutosha.

Lakini licha ya kuwa ni eneo la kutupia taka, ni sehemu muhimu inayozalisha ajira za vijana, wakiwemo wanawake. Kila siku makumi ya vijana wa kike na kiume, wanasafiri kutoka mjini na vijiji jirani kuja kufanya kazi katika jaa hili.

Kazi wanayoifanya ni kukusanya chupa za plastiki na taka nyengine zenye ajisili ya chuma, shaba na bati.

Baada ya kukusanya taka hizi, wanarejesha tena mjini na kuziuza kama bidhaa chakavu kwa mafundi wa vibatari, majiko na kwenye maduka ya kununulia bidhaa chakavu ambayo yamejaa kila kona.

Katika muda wa siku tatu nilizokaa hapa nikifanya kazi ya kukusanya chupa,ilitosha kubaini ni sehemu linayotoa ajira karibu kwa vijana 50, wengi wao wakiwa wanaume.

Fatma Haji (35) mkazi wa Magomeni wilaya ya mjini Unguja ni mmoja ya wanawake niliokuta nae.

Kazi iliyompeleka katika jaa hili ni kukusanya chupa za plastiki na shaba.

Siku ya kwanza kutana nae, Fatma alikuwa amekusanya zaidi ya chupa 10,000 ambazo amezihifadhi ndani ya jaa hilo akisubiri gari ya kuzirejesha mjini.

Akiwa na polo lake mgongoni, anasema chupa na waya za shaba anazopata anaziuza kwa wanunuzi wa bidhaa chakavu.

Kilo moja ya shaba anauza shilingi 7,000 hadi 8,000 na mzigo wenye chupa 5,000 anauza kwa shilingi 80,000. Hiyo ndio kazi inayompatia kipato cha kuendesha familia yake ya watoto watatu.

“Kila siku nakuja hapa, nina watoto wanaonitegemea hivyo nisipokuja nitashindwa kuwahudumia,” anasema huku akipeleka chupa zake sehemu ya kukusanyia.

Lakini kupata chupa sio kazi rahisi kutokana na ushindani uliopo kutoka kwa vijana wengine.

Hivyo Fatma analazimika kuamka saa 11.00 alfajiri na kuwahi jaani mapema, vyenginevyo anakuta chupa zimeokotwa.

Anasema hajali harufu ya uvundo inayotoka katika jaa hili, muhimu kwake ni kupata chupa kabla ya kurudi nyumbani.

“Wakati mwengine wanunuzi wanatufanya huku, muhimu uwe umezikusanya,” anasema.

Ndani ya jaa kuna shehena za chupa zilizohifadhiwa ndani ya uzio uliotengenezwa kwa viroba (vipolo) na vyandarua vilivyochakaa.

Kazi nyengine inayofanyika ni ya vitu vyenye asili ya chuma na bati.

Kuna vijana wameweka mezani ya kupimia uzito na kisha kupakia garini na kurejesha mjini.

Ame Ali (27) mwenyeji wa Karakana Wilaya ya Mjini ni mmoja ya vijana wa kiume niliokutana nao.

Kazi yake ni kupima taka za chuma, shaba na bati na kupakia kwenye gari ndogo na kisha kuzisafirisha mjini.

Ali ananihadithia kwamba jaa hilo ni sehemu muhimu ya kujipatia riziki hasa kwa vijana.

Bila ya hofu, akiamini anazungumza na mtu mpya katika jaa hilo, ananisimulia jinsi kazi hiyo inavyoendesha maisha yake.

“Tunaokota vipande vya bati, shaba au chuma na kupima pale (ananionesha mezani ya saa inayoning’inia kwenye tawi la mti) halafu tunapakia garini na kurejesha mjini.

Kule tunauza kwenye maduka ya bidhaa chakavu,” anasema. “Hatupati pesa nyingi, lakini bora kufanya kazi hii kuliko kukaa vijiweni kuvuta bangi au kupora,” anasema.

Anasema anapata kati ya shilingi 30,000 hadi 40,000 kwa siku lakini siku kazi inapokuwa mbaya anapata shilingi 5,000 au 10,000.

“Kila mmoja anaweza kuja na kufanya kazi hii, hakuna anaekatazwa muhimu uweze kuvumilia harufu mbaya ya taka,” anasema.



Mara nashuhuhudia magaari mawili ya Baraza la Manispaa,yakileta taka kwenye jaa hili.

Mimi na wenzangu tunakimbilia sehemu ambayo taka mpya zinamiminwa.

Kwa tahadhari kubwa tunachekura na kutafuta vitu vinavyotufaa.

Mwangalizi wa jaa anatushauri kuchukua tahadhari kwani tunaweza kujichoma na vitu vyenye ncha kali.

“Angalieni msije mkajichoma,” anasema mwangalizi mmoja ambae hakutaja kijana lake litajwe.

Waangalizi wanaishi kando kidogo ya jaa lakini muda mwingi wanautumia wakiwa eneo la jaa kuongoza gari zinazoingia na kutoka.

Kwa Fatma, anasema chupa anazokusanya zinasafirishwa kwenye viwanda vya maji na vinywaji baridi Zanzibar na Tanzania Bara. “

Kuna watu wananua kwa wingi na kusafirisha Dar es Salaam na wengine wanauza hapa,” anasema.

Mmoja ya wanunuzi wa bidhaa chakavu, ambae aliejitambulisha kwa jina maarufu la Kachara, anasema biashara hiyo ameianza miaka mitatu sasa.

Kachara ambae ananunua bidhaa za chuma, shaba na bati kando ya barabara iendayo Mbuzini, ananunua bidhaa kutoka kwa watoto na watu wazima.

“Baada ya kununua nakusanya hapa, kama kuna bidhaa inayohitaji kuvunjwa, kuna kijana wangu ambae namlipa kwa ajili ya kazi hii,” anasema.

Kachara anasema bidhaa zake anapeleka kwenye viwanda vya chuma Dar es Salaam ambako huyeyushwa na kutengenezwa bidhaa mpya za chuma, bati au shaba.

Anasema kwa siku anatumia hadi shilingi 400,000 kuwalipa watu wanaopeleka bidhaa hizo.

“Nimeajiriwa na nalipwa kwa kazi hii. Kila baada ya wiki mbili naletewa fedha za kununulia na baadae wenyewe wanakuja kusafirisha,” anasema.



Hata hivyo, kitendo cha waangalizi wa jaa hili kuchoma taka hakiwafurahishi vijana hawa kwa sababu taka wanazozitegema zinayeyuka.

“Siku nyengine jaa linachomwa moto, kitendo hiki kinatuumiza kwa sababu bidhaa tunazozifuata zinayeyuka, lakini ndio utaratibu wao, hatuwezi kuwazuia,” anasema Ali.

Akizungumza kwenye mafunzo ya kuijengea uwezo kamati ya ajira wilaya ya Mjini na Magharibi Unguja katika ukumbi wa wagonjwa wa afya ya akili Kidongochekundu, Aprili 2016, Mkurugenzi Idara ya Ajira, Ameir Ali Ameir, alisema tatizo la ajira kwa vijana bado ni changamoto. Alisema vijana wengi kukosa sifa za kuajiriwa na baadhi kuchagua kazi.

Lakini taka zinaweza kuwa suluhisho la tatizo la ajira miezi michache ijayo na pengine idadi ya vijana wanaokimbilia Kibele, inaweza kupungua au kuongezeka lakini sasa watakuwa wakifanya kazi rasmi zenye maslahi zaidi.

Ni baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) na Kituo cha Sayansi na Mazingira cha New Delhi India, kusaini mkataba wa makubaliano na ushirikiano wa usimamizi wa taka. Mkataba huo ulisainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sayansi na Mazingira cha New Delhi, Chandra Bhushan na Mkurugenzi Mkuu wa ZEMA, Sheha Mjaja Juma.

Mradi huu kwa kuanzia utajikita katika sekta ya utalii ambako ndiko kunakozalishwa taka kwa wingi. Ingawa bado utekelezaji haujaanza rasmi, Majaja anaamini mradi huo utaisaidia Zanzibar kuwa na miongozo na mbinu bora za usimamizi wa mazingira pamoja na kufanya tafiti za kimazingira.

ILO
Tarehe 18 Juni, 1998 Shirika la Kazi Duniani (ILO) lilipitisha Azimio la juu ya Kanuni za Msingi na Haki Kazini na Ufuatiliaji wake huko Geneva, hivyo kutilia maanani changamoto zinazoletwa na kuingia kwa mfumo wa uchumi huria wa ulimwengu ambazo zimekuwa ndio mwelekeo wa majadiliano mengi katika ILO tangu 1994. 

Aambapo pomoja na mambo mengine, azimio hilo linatambua na kuthamini wanaojiajiri na hasa ikiwa ajira zao ni halali na zimekuwa na mchango wa kuinua pato la nchi husika.

Kumbe hapa azimio hilo, linawagusa hata waokota vyuma chakavu na hata vitu vya plastiki katika jaa la kibele kisiwani Unguja, maana wamekuwa wakichangia pato la taifa na upande mwengine kupunguza tatizo la ajira serikalini.



                                    mwisho

Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 mchan

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’’ali

…….SUZA WATOA USHAURI WA ADHABU YA KUNYONGWA

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ WANAFUNZI wanaosomea uwalimu Chuo cha taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ kampasi ya Benjamin Wiliam Mkapa Wete Pemba, wamependekeza adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa mtu atakaetiwa hatiani, kwa kosa la dawa za kulevya. Walisema, haiingii akili kuona, mahkama imeshamtia hatiani mtu kwa kukutwa na dawa za kulevya, ambazo huathiri nguvu kazi ya taifa na kisha, kupewa hukumu ya kifungo pekee. Wakizungumza leo Juni 26, 2024 kwenye kongamano la vyuo vikuu, juu ya masuala ya msaada wa kisheria, kuelekea wiki ya msaada wa kisheria Zanzibar, lililofanyika Chuoni hapo, walisema wakati umefika sasa kutolewa kwa hukumu hiyo. Walipendekeza kuwa, ni vyema kwa mtu anayetiwa hatiani asibakie chuo cha Mafunzo pekee kuitia tena hasara serikali kwa chakula na wakati mwingine matibabu, wakati tayari ameshasababisha madhara, kwa vijana. Mshiriki Juma Nafasi Juma, alifafanua kuwa kama mtu ameamua kuliumiza taifa kwa kuingiza, kusafirisha, kusambaaza dawa za kulevya, hivyo ni vy

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa ufafan