:
MHADHIR wa Chuo Kikuu Huria Tanzania ‘OUT’ tawi la Pemba, Sheikh Bakari Kombo Bakari, amesema waumini wa dini ya kiislamu, wanao wajibu wa kuendeleza mafunzo waliyoyapata katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kivitendo.
Amesema isitoshe kwa waislamu, kuona kwamba mwezi wa Ramadhani umemalizika na kuacha ibada mbali mbali walizokuwa wakizitekeleza kipindi hicho cha mfungo, kwani itakuwa ni sawa kama vile walijizuia kula na kunywa katika wakati huo.
Mhadhiri huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislamu waliohudhuria kwenye mahafali ya sikukuu ya Eid al-fitri, yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar na kufanyika msikiti wa Makonyo Wawi Chake Chake.
Alisema ni wajibu ya wazazi na walezi, kuwalea watoto wao katika maadili ya uisalamu, na kuwabidiisha kufanya ibada ikiwemo kuswali, kusoma Qur-an na kutoa sadaka kwani ndiyo mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W).
‘Vijana wetu wengi wameacha ibada na badala yake wamekuwa wakijishughulisha na mambo ya kipuuzi, kama vile mpira na kuacha kumcha Allah ‘SW’.
Muhadhiri huyo wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, aliwakumbusha waislamu juu ya kuwasaidia mayatima na maskini, ambao wapo kwa idadi kubwa katika maeneo mbali mbali, wakiwa wanadhalilika baada ya kukosa wasimamizi.
Aidha ametoa wito kwa waislamu, kufuatilia mienendo ya watoto wao katika kipindi hiki cha sherehe za Iddi, kwani wengi wao wamekuwa wakisheherekea kinyume na mafundisho ya uislamu.
‘’Watoto wetu wamekuwa wakitenda matendo maovu kama vile ulevi, kufanya zinaa na kwenda maeneo ambayo ni yenye vitendo vya kumuasi Allah kama kwenye kumbi za musiki,’’alitahadharisha.
Akisoma risala katika maghafali hayo, Naibu Katibu wa JUMAZA Zanzibar sheikh, Saleh Juma Kali, alisema mchango wa kila muislam, na kwa nafasi yake aliyonayo ni muhimu na inahitajika katika kupinga vitendo vyote viovu.
Alielezea UKUWEM na JUMAZA, ni taasisi ambazo zimesajiliwa rasmi na zimeanzishwa kwa lengo la kuwaendeleza waislam na kuwaleta pamoja, huku jumuiya hizo zikifanya kazi mbali mbali kama kuendeleza dawaa.
Kwa upande wake Naibu Amiri wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar ‘JUMAZA’ ustadh Seif Khamis Nasor, amewahimiza waislam kujitokeza katika maghafali kila yanapo fanyika, kwa lengo la kujipatia makatazo na amri za Muumba.
Mwisho.
Comments
Post a Comment