NA HAJI NASSOR, PEMBA
MWANASHERIA wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya amana Zanzibar ofisi ya Pemba, Massoud Ali Massoud, amewataka wanawake, wanaonyimwa au kucheleweshewa mirathi, kuitumia Kamisheni hiyo, ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Alisema, wanawake wamekuwa ndio waathirika wakubwa, pale familia zinapochelewesha kurithi, ama wakati mwengine kutorithi kabisa, hivyo Kamisheni ni sehemu muhimu kwa waathirika kama hao.
Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika Samail Gombani Chake chake, na kuyashirikisha makundi ya wanawake na watu wenye ulemavu, alisema sio busara kwa wanawake kuendelea kukoseshwa haki zao.
Alieleza kuwa, ni wakati sasa kwa jamii za kiislamu kuitumia Kamisheni hiyo, kwa ajili ya kupata ushauri na mamna bora ya kufanya shughuli za mirathi.
‘’Sasa wananchi wanaotaka kufanya mirathi waje ofisini kwetu, maana hata lile tozo, limeshuka kutoka asilimia 5 kabla ya mwaka 2008 na sasa kufikia asilimia 0.25,’’alieleza.
Akatolea mfano kuwa, kwa sasa mirathi yenye thamani ya shilingi milioni 1, gharama inayopaswa kulipwa na wahusika ni shilingi 2500, badala ya shilingi 5,000 ya zamani.
‘’Kwa mujibu wa kanuni yetu, gharama nyingine ni ile ya usafiri kutoka ofisini kwetu, hadi eneo ilipomirathi husika, mabayo hii itamuwajibikia muhusika,’’alieleza.
Hata hivyo, amewakumbusha wanaume, kuacha tabia ya kukalia mirathi kwa muda mrefu, na badala yake watekeleze matakwa ya aya ya Qur-an, inayoharakisha jambo hilo.
Kwa upande wake Mratibu wa Kamisheni hiyo Pemba sheikh Ali Haji Ali, amesema ili ofisi hiyo ifanyekazi, hakunabudi kwa wananchi, kuitumia.
Alisema, serikali kwa maksudi imeshusha gharama ya tozo la urithishaji kutoka asilimia 5 ya mali inayotaka kurithiwa, hadi asilimia 0.25.
Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha urithi cha Kamisheni hiyo Ali Mbarouk Dadi, alisema kwenye mirathi, wanawake wanayohaki ya kupata mirathi kwa wakati.
‘’Wakati mwengine wapo baadhi ya wanaume, wanapoona warithi wenzake ni wanawake na tena ni wenye ulemavu, huona hawana haki, jambo ambalo sio sahihi,’’alieleza.
Wakichangia mada kwenye mkutano huo, baadhi ya washiriki akiwemo Raya Ali Hamad wa Wete, alisema bado elimu ya matumizi ya ofisi hiyo, iko chini.
Nae Riziki Hadid Rashid, alisitiza haja kwa ofisi hiyo, kufika vijijini na kutoa elimu zaidi kwa wanawake, juu ya haki na nguvu walizonazo kwenye urithi.
‘’Inawezekana wanawake tunaona suala la kupata mirathi yetu kwa wakati, ni kama zawadi kutoka kwenye familia, hivyo kama yatachelewa hatuoni kuwa ni haki kuhimiza,’’alieleza.
Kwa upande wake Raya Khamis Hamad na mwenzake Amina Omar Mohamed, waliipongeza Kamisheni ya Wakfu na Mali ya amana, kwa kufikiria kufanya mkutano huo.
Katika mkutano huo uliojumuisha washiriki 30, mada kadhaa zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wanawake katika mirathi na wanawake na mirathi.
Kamisheni hiyo ipo kwa mujibu wa sheria nambari 2 ya mwaka 2007, ambapo moja ya jukumu lake la msingi ni kuendesha mirathi kwa familia za kiislamu.
Mwisho
Comments
Post a Comment