NA ZUHURA JUMA,PEMBA
KILA ifikapo Mei 3 ya kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari.
Siku hiyo waandishi hupata nafasi ya kujadili mazuri na mabaya wanayokumbana nayo katika kitumiza kazi ya kikatiba ya kuwapa habari wananchi.
Zipo tasisi kabla ya kufikia kilele hicho, huwa na shughuli mbali mbali kama vite matembezi katika maeneo wanayochukua habari au mikutano ya pamoja.
Kwa upande wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba , PPC wao walikuwa na shughuli ya kongamano la siku moja lililofanyika Gombani Chake chake kisiwani humo.
Kongamano hilo lililowashirikisha waandishi wa habari, wahariri na wadau mbali mbali, kwa lengo la kuhakikisha kwamba kuna uhuru wa vyombo vya habari.
Ilitajwa kuwa, vyombo vya habari ni daraja muhumu katika jamii, ambalo husaidia kupata habari na taarifa mbali mbali, kutoka kwa watawala na jamii wenyewe.
Mabadiliko hayo huletwa kwa njia mbali mbali kama vile kuelimisha, kushajihisha, kuelekeza na kujenga ushawishi wa mambo ambayo yanapotekelezwa jamii hurekebishika.
Ali Mbarouk Omar ambae ni Katibu Mkuu PPC wakati akiwasilisha mada ya uhuru wa kujieleza na maadili ya waandishi wa habari, anasema siku zote habari zinajenga ujasiri.
Kama wananchi wakipatiwa habari sahihi na zenye ukweli ndani yake, itakuwa ni daraja la kufanya uamuzi sahihi kwa maslahi ya tifa lao.
‘’Wananchi walio wengine hukumbwa na wagoa wa kupaza sauti zao, ijapokuwa wanaishi kwenye dimbwi la shida na dhiki, lakini mtu muhimu ni mwandishi wa habari,’’anasema.
Anabainisha kuwa, licha ya majukumu yao ya kupasha habari, kuelimisha na kuburudisha, lakini wanazidi kuchukua nafasi muhimu katika jamii kama wakala wa mabadiliko.
Uwakala huu kwa wanahabari, anasema unaweza kuwa rahisi ikiwa wamendaa vipindi au uandishi wa Makala baada ya wao kufanya utafiti.
‘’Hapa niwakumbushe waandishi wa habari, lazima tuwe na utamaduni wa kufanya utafiti utakaoambatana na matumizi sahihi ya takwimu, ili tunapoisaidia jamii, tuwe na uhakika’’,anafafanua.
Anasema, mwandishi huyatumia mazingira tofauti katika kukamilisha kazi za kihabari ikiwa ni pamoja na ofisini, kwenye mikutano kisiasa na kijamii, vijijini, viwanja vya michezo na wakati wa uchaguzi.
Kwenye kongamano hilo, alikuwepo pia Makamu Mwenyekiti wa PPC, Khadija Kombo Khamis ambaye nasema, ushirikiano unahitajika kati ya wadau na waandishi wa habari.
Khadija anaona katika kuhakikisha wanasaidia upatikanaji wa taarifa ambazo zitasaidia katika maslahi ya taifa, suala la waandishi kupewa ushirikiano ni ngao muhimu.
"Pasi na kuwa na vyombo vya habari nchini, hakuna chochote kinachoweza kuendelea, hata maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana, hivyo ni muhimu kwa wadau kutoa taarifa na sio kuficha", anaeleza.
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KWA MWANDISHI WA HABARI
Maadili ya uandishi wa habari, ndio nguzo zinazoshikilia uandishi salama, na wenye manufaa kwa jamii husika.
“Pia utashi wa akili wa kutambua kuwa, kuna habari nyingine, inaonekana nzito au kubwa, lakini ikiwa inahatarisha usalama wa nchi, kuchochea migogoro au haina faida kwa mwandishi unaiweka kando, itasaidia kukuweka katika mazingira salama wakati wote”, anasema Makamu Mwenyekiti huyo.
Anafafanua, ipo haja kwa waandishi kufahamu viashiria vya mazingira ya hatarishi kwa lengo la kujinusuru na madhara yanayoweza kuwapata, wakiwa kazini au mahala popote.
Kongamano hilo lilifunguwa na Mrajisi wa Asasi zisizo za serikali NGO's Pemba, Ashrak Hamad Ali, akwaeleza waandishi hao kujikita katika kuwaelimisha wannachi, juu ya maendeleo yaliofikiwa.
Akawaeleza waandishi hao kuwa, wanazo nguvu kubwa na ikiwa watazitumiza kwa uweledi na hasa kuziekeleza vijijini, wanaweza kuwa daraja tegemo kwa wananchi.
Anasema, kuna mambo mbali ambayo yatasaidia kuwepo maendeleo katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuelimusha jamii juu ya umuhimu wa kutumia rasilimali za bahari, kutangaza utamaduni na utalii.
“Katika nchi yetu kuna uhuru wa vyombo vya habari, hivyo uhuru huu utusaidie kuchapuza maendeleo na sio kuleta mfarakano, kwa sababu nguvu yenu mukiitumia vizuri tutavuna mazuri na mkiitumia vibaya mtasababisha migogoro”, anaeleza Mratibu huyo.
Alitumia kongamano hilo, kuwashauri watoa habari, kukaza buti na kuwa ushirikiano mpana waandishi wa habari, ili kuwapa taarifa pale wanapohitaji.
“Kufuata maadili ni muhimu katika kazi yenu ya habari, kwani kinyume chake mnaweza kuchafua amani iliyopo na kusababisha vurugu na mwisho wake nchi kukosa maendeleo”, alisema.
UMUHIMU WA SAUTI (HABARI) KATIKA JAMII
Ni vyema kwa waaandishi sauti zao zikawa ni zenye uwezo wa kubadilisha sera, misimamo, tabia, mitazamo mibaya ya watu, pamoja na kuwa na sauti zinazojenga maridhiano na usawa.
Kuwe na sauti inayoweza kubadilisha maamuzi mabaya yanayoumiza jamii ya watu wengi na kuwafanya watu wachukue maamuzi yanayofaa.
“Wasio na sauti wanahitaji vyombo vya habari viwasemee, kwani wao hawana fursa za kusema na hawawezi kusema wenyewe, hivyo vyombo hivi vinawajengea ujasiri wa kusema”, anafafanua Mrajisi huyo.
WANAHABARI NA WADAU WA HABARI
Ali Massoud Kombo ambae ni Mkurugenzi wa Jamii tv online, anasema pamoja na kujitahidi kuibua matatizo kwenye jamii, lakini bado wanakabiliwa na tatizo la baadhi ya viongozi kuwaingilia kwenye mamlaka yao, jambo ambalo sio sahihi.
"Baadhi ya viongozi wanatumia mamlaka yao vibaya kwa kutuwekea mipaka na kutupangia habari za kuzitoa wanazozitaka wao, hivyo tunasema wasituingilie", anakemea.
Mdau wa habari Dkt. Amour Rashid, yeye kubwa anawashauri, waandishi wa habari kuwa wabunifu na kuepuka kukariri habari hizo.
Akaenda mbali zaidi na kuwataka waandishi hao, kujiendeleza katika misingi ya lugha, kusoma sheria na Katiba ya nchi.
Said Mohamed Ali ambae ni mwanachama wa PPC, anawataka waandishi wa habari, kujiamini katika kazi zao, sambamba na kuzingatia maadili ya kazi yao.
“Wanahabari sasa ni wakati wa kuutumia uhuru wa habari uliopo, ipasavyo kwa kuibua changamoto zinazowakabili wananchi, lakini tusikae kimya wananchi wanaumia”, anasema.
Anasema kuwa, wananchi waliopo vijijini wamekuwa na ukosefu wa taarifa nyingi na kukosa baadhi ya huduma, ipo haja kwa waandishi kuwasaidia.
Msaidizi Katibu Mufti Zanzibar anayefanyia kazi zake, Pemba Sheikh Said Ahmad Mohamed, anasema katika kufanikisha hayo, waandishi waendelee kujikita zaidi vijijini, kwa kuibua changamoto zinazowakabili wananchi.
NINI KIFANYIKE
Vyombo vya habari vinaweza kuwa nyenzo muhimu ya kusaidia jamii, kinachohitajika, katika kufikia azma hiyo ni kuwa na vyombo vya habari, waandishi wa habari na wadau wanaotambua umuhimu wa habari.
Vyombo vya habari vizingatie maadili pamoja na kuwa na jamii inayopenda haki.
Kongamano hilo la kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari liliandaliwa na PPC kwa kushirikiana na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
MWISHO.
Comments
Post a Comment