NA ZUHURA JUMA, PEMBA:
………..KUNI ya akiba daima huicheka inayoteketea jikoni……bila ya kujua kuwa ikimaliza nayo itafuata…………..
Kauli hii ya wazee wa zamani, ndio inayotoa tawira kwa viongozi wa leo ambao huwacheka wanawake na watoto jinsi wanavyokumbwa na changamoto kwenye maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi.
Kumbe wanasahau kwamba, watoto ni kuni zilizojikoni na zinateketea na zikimalizika sasa ni zamu ya waliowakuwa wakichekelea na kuwaona watoto na wanawake hawahusiki kupewa taaluma ya ukimwi.
Mimi naamini watoto wa Tanzania, kama walivyo watoto wengine ulimwenguni kote, nao wana haki ya kuzaliwa wakiwa huru bila ya kuwa na VVUna ukimwi.
Watoto hao ambao hutajwa kuwa ndio taifa jipya na viongozi wetu wa kesho, wanaopaswa kulindwa ili kuhakikisha hawaambukizwi na VVU, ambapo matokeo yake hukubwa na magonjwa mengine.
Kwa Tanzania bado suala la elimu ya Ukimwi limekuwa likiguswa kijumla jumla ambapo makundi hatarishi kama ya watoto, wanawake na makundi mengine hayazingatiwi.
Hatari za watoto na wanawake kukumba na VVU na Ukimwi zipo nyingi ikiwa ni pamoja na ile ya kibaologia (kimaumbile) hadi kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Sababu hizo na nyengine huwafanya watoto na wanawake kukosa fursa sawa na kuwa na fursa finyu ya kupata taarifa sahihi za maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi.
Sababu hii hulifanya kundi hilo, kuwa rahisi kutekwa kimawazo, kiuchumi, kiakili na kusababisha kujiingiiza kwenye vishawishi vya kukumbwana VVU na kisha Ukimwi.
Na ndio maana kwa mujibu wa jarida la wekeza kwa watoto lineleza kuwa, asilimia 50 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 20 hadi 49 wameshafanya ngono kwa mara ya kwanza kabla ya kufikia umri wa miaka 18 na asilimia 10 kabla ya kufikia umri wa miaka 15.
Takwimu za sasa zinaonyesha kwamba asilimia ya wanawake wenye kiwango cha ufahamu wa kuhusu VVU na Ukiwmi ni 40 wakati kwa wanaume ni asilimia 47.
Hapa ndipo tunapoona kwamba kundi la wanawake na watoto bado halijaangaliwa ipasavyo juu ya elimu juu ya VVU na Ukimwi nchini Tanzania.
Tunapogusa elimu ya ukimwi kwa watoto wa kike na wanawake pia tunagusa suala la elimu ya kondomu ambayo hutajwa kwamba inaweza kuzuia kwa kiwango fulani maambukizi ya VVU na Ukimwi.
Takwimu zinaonyesha kwamba watoto wa Tanzania ambao hawajaolewa matumizi ya mipira hiyo iko kwa asilimia 55 ingawa changamoto kubwa ni matumizi sahihi na endelevu ya kondomu.
Ali Mbarouk Omar yeye ni Mratibu wa Tume ya Ukimwi Zanzibar ofisi ya Pemba, alisema bado elimu inahitajika zaidi kwa makundi hayo.
“Matumizi ya kondomu kwa anaeamini kwamba yanamzuia na maambukizi ya VVU na Ukimwi, yanahitaji elimu ya kina na hasa juu ya matumizi na uendelevu wake’’,alisema.
Nusu ya maambukizi ya ukimwi ulimwenguni yanawahusu watoto wa kike na hasa kuanzia miaka 20 hadi 24, na ingawa maambukizi zaidi miongoni mwa wanawake ni wale wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49, lilieleza jarida hilo.
Kwa vile kundi la wanawake na watoto limekuwa halijawekea mkazo wa kutosha juu ya elimu ya VVU na Ukimwi hata akina mama wenye ujauzito wako hatarini kujifungua watoto waliopata maambukizi.
Na ndio maana kila mwaka wajawazito wenye Ukimwi wapatao 119,000 wanahofiwa kuwa na uwezekano kujifungua watoto wenye UVV moja ya sababu ni kukosa elimu sahihi.
Jarida hilo limetamka kwamba, asilimia 96 ya vituo vya nchi nzima Tanzania, vinavyotoa huduma ya mama na mtoto, vinatoa elimu ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT).
Pamoja na hilo, bado kuna mapengo makubwa, maana hadi kufikia mwaka 2011 ni asilimia 64 ya akinamama wajawazito wenye maambukizi ya VVU na asilimia 56 ya watoto wachanga waliokuwa kwenye mazingira ya kuambukizwa Ukimwi walipata huduma ya kurefusha maisha ‘ART’.
Hao walifanikiwa kuzuiwa maambukizi hayo kutoka kwa mama kwenda kwa watoto, ambapo bado elimu ya kina kwa wanawake wasiopata kuolewa na vijana inahitajika.
Asha Mohamed Hassan (40) wa Chakec Chake Pemba ambae anaishi na Virusi vya Ukimwi kwa mwaka sita sasa, ambae alipata mtoto bila ya kuwa na maambukizi, alisema hilo linawezekana kwa asilimi 100.
“Kasoro iliopo hadi kufikia watoto wanazaliwa wakiwa na maambukizi mapya na kudhoofisha kufikia maziro matatu ni ufinyu wa elimu kwa vijana na wanawake’’,alisema.
Afisa elimu na uhamasishaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar ZAC, Sihaba Saadat, alisema kwamba vijana wa kike na wa kiume pamoja na mama wajawazito wakipatiwa elimu endelevu hakutarajiwi kuzaliwwa watoto wenye maambukizi mapya.
“Hatua kama tume ya ukiwmi ya kutoa elimu kwa wanawake, vijana wa kike na kiume tumepiga, maana sasa Zanzibar wapo wanojifungua wakiwa na maambukizi na watoto wao wakiwa huru’’,alisema.
Asha Said Humud wa Wete ambae anaishi na VVU na akiwa mjamzito alisema pamoja na elimu aliokwisha pewa, hana hakika kwamba atapata mtoto alie salama na VVU.
“Unajua hofu yangu ni ya kibinaadamu tu, lakini yupo mwenzangu ambae hajaamua kujitangaaza ingawa alishapewa elimu lakini mtoto wake pia ana VVU’’,alifafanua.
Mwanafunzi wa skuli yasekondari ya Shamiani Khadija Omar Haji alisema hajawahi kupata taalumu ya VVU na Ukimwi, jambo ambalo linampa wasiwasi juu ya maisha yake ya baadae.
Ingawa takriban skuli kadhaa zinavilabu vyanavyozungumzia kuhusu UVV na Ukimwi, lakini mwanafunzi Hamad Mohamed wa skuli ya Kojani, alisema yeye alishapa taaluma ya VVU na Ukimwi ingawa ni kwa muda mfupi.
Hadi mwaka 2014, kisiwa cha Pemba kilikuwa na wanachama watoto 60 wanaoishi na VVU ambapo idadi hiyo ni wale tu ambao kwa njia moja ama neyngine wamesajiliwa kupitia jumuia ya watu wanaoishi na VVU Pemba, ZAPHA+.
Kwa mujibu wa jarida la ‘kwanini kuwekeza kwa watoto?’ linalozungumzia ajenda za watoto, la mwaka 2013, limetamka bayana kwamba, watoto walioko skuli hushindwa kupata elimu sahihi ya VVU na Ukimwi. |
Kwa mujibu wa tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania, kwenye utafiti wake uliofanya wa kiashirio cha VVUna Ukimwi, Tanzania mwaka 2011/2012 umejumuisha kwa kupima wanawake na wanaume wafikao 20,811.
Kwa mujibu wa utafiti huo asilimia 5.1 ya watanzania wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wanamaambukizi ya VVU na Ukimwi, ambapo ambukizi hayo ni ya kiwango cha juu miongoni mwa wanawake, kuliko wanaume katika maeneo ya mijini na vijijini.
Maambukizi hayo nchini Tanzania yamepungua katika miaka ya hivi karibuni, ambapo kiwango cha hivi karibuni cha VVUna Ukimwi ni asilimia 5.1 ambapo asilimia 6.2 ni wanawake na asilimia 3.8 ni wanaume.
Kwa kulinganisha na
utafiti wa kiashirio cha VVU na Ukimwi cha 2007/2008 umebaini maambukizo ya
jumla kuwa ni asilimia 5.7 ambapo kwa Mkoa wa Njombe yalionekana kuwa juu na
kufikia asilimia 14.8 ambapo kwa wakati huo kiwango cha maambukizo ni cha
chini zaidi Pemba ambayo ni chini ya asilimia 1. Klabu ya waandishi wa habari za Ukimwi Tanzania ‘AJAAT’ imekuwa ikiweka mkazo kwa kuwapa elimu wa kina waandishi wa habari ili kuandika habari za mkundi maalumu.
Mkufunzi kwenye mafunzo yaliofanyika hivi karibuni mjini Zanzibar, Chalrse Kayoka, alibainisha kuwa kundi la watoto na wanawake bado halijandikiwa ipasavyo juu ya changamoto wanazokumbana nazo katika kujinga na VVU na Ukimwi.
Lakini sera taifa ya kudhibiti Ukimwi Tanzania ya mwaka 2001, ilieleza kuwa, elimu kuhusu hatari ya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto itatolewa kwa wanawake wote wenye umri wa kuzaa.
Sera hiyo ilieleza kuwa, pia kuwapa elimu wanawake ya uwezo wa kiuchumi ili kuwawezesha kuwapatia watoto wao vyakula vyenye virutubisho, sasa hapo ndipo unapogundua kwamba bado kundi la wanawake halijapewa kipaumbele.
Mwisho
|
Comments
Post a Comment