NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
Zanzibar Riziki Pembe Juma, amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa uwanja
wa mpira wa miguu uliopo Kangani wilaya ya Mkoani Pemba.
Alisema, sababu ambazo zilizotolewa za kuzorotesha ujenzi
wa uwanja huo, hazijamridhisha na kuwataka wajenzi wa uwanja huo, kuzidisha
kasi ya ujenzi.
Waziri Pembe, aliyasema hayo jana uwanjani hapo, kwenye
ziara ya siku tatu, aliyoambatana na Katibu Mkuu wake, Mattar Zahor Massoud, ya
kuvitembelea viwanja kadhaa kisiwani humo.
Alieleza kuwa, sababu ya uhaba wa tendaji, kuadimika kwa
saruji na kuchelewa kuvipokea baadhi ya vifaa vya ujenzi huo, wala sio sababu za
msingi.
Alieleza kuwa, viwanja hivyo vinasubiri kwa hamu na
wananchi na wanamichezo ili wavitumie, hivyo lazima kampuni ya Reform Sports kutoka
Uturuki, inayojenga viwanja hvyo kuzidisha kasi.
Alieleza kuwa, serikali imeamua kutoa fedha nyingi kwa
ajili ya ujenzi wa miundombinu ya viwanja hivyo, ni lazima waliokubali kuchukua
kazi hiyo, waiharakishe.
‘’Baada ya maelezo yenu, kwa hakika sababu za uhaba wa
watendaji, mara saruji kuadimika, mara mvua ilinyesha jana na jioni au
kuchelewa kupokea vifaa ni sababu nyepesi,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo Zanzibar Riziki Pembe Juma, alisema Dk. Mwinyi ameamuwa
kujenga viwanja hivyo ikiwa ni hatua ya kuibua vipaji.
Alieleza kuwa, vipaji hivyo kisha vinaweza kuzaa ajira,
kwani, kwa sasa michezo ni sehemu ya maendeleo kwa vijana mbali mbali.
‘’Dk. Mwinyi amekuwa akihakikisha anaweka miundombinu ya
viwanja hivi, tena vya kisasa, lengo ni kuibua vipaji, na kisha kiviendeleza
ili vijana hao waweze kupata ajira kupitia sekta hiyo,’’alifafanua.
Akiwa katika ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Ukutini,
Waziri huyo aliitaka kampuni inayojenga uwanja huo, kuzidisha kasi kwa haraka.
Mapema Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mattar Zahor Massoud,
alisema michezo ni eneo moja wapo, linalokusanya idadi ya watu wingi, tena kwa
wakati mmoja.
Alifafanua serikali ya awamu ya nane, kwa kujali umuhimu
huo, ndio maana imekuwa ikitumia fedha nyingi kuhakikisha inajenga viwanja
mjini na vijijini.
Alieleza kuwa, kilichobakia kwa wananchi na hasa vijana
kuvitumia viwanja hivyo, kwa mambo kadhaa ikiwemo kujega afya, umoja na kuwa
sehemu ya ajira.
‘’Niwaombe sana wananchi, viwanja hivyo tuvienzi na
kuvitunza maana ni sehemu ya kujenga umoja na kubwa zaidi ni kuona vijana
wanafika mbali kimichezo,’’alifafanua.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Pemba
Mfamau Lali Mfamau, alisema ujenzi wa viwanja hivyo ni sehemu ya mpango mkuu wa
wizara.
Kwa upande wake Mshauri Elekezi Fesal Soud, alisema
ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu Kangani, kwa sasa umeshafikia asilimia 92,
na wakati wowote utakamilika.
Alieleza kuwa, ujenzi wake ulianza mwanzoni mwa mwezi
huu, ingawa kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na hali ya
hewa, umechelewesha.
Wakati huo huo, wananchi wa Ukutini pamoja na sheha wao
Ali Hussein, waliipongeza wizara hiyo, kwa hatua ya kupata ajira za muda.
Katika ziara hiyo, Waziri huyo na ujumbe wake,
ulivitembelea viwanja wa mpira wa miguu Kangani, Ukutini, viwanja vya mchezo wa
kikapu Tenis Chake chake na Kangani, pamoja na wakala wa uchapaji.
Mwisho
Comments
Post a Comment