NAIBU Katibu Mkuu wa Utumishi na
Utawala bora Zanzibar Omar Haji Gora, amesema kupandishwa kwa mshahara kwa
watumishi wa Umma katika serikali
ya awamu ya nane ni miongoni mwa juhudi za serikali za kuwaandalia mustakbali
mzuri wa maisha watumishi baada ya kustaafu.
Alisema hayo katika ufunguzi wa
mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa wastaafu watarajiwa watakaolipwa mafao yao ya kustaafu kazi na mfuko wa
hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF, yaliofanyika katika ukumbi wa Kiwanja cha
kufurahishia watoto Tibirinzi Chake chake Pemba.
Alisema katika kuhakikisha watumishi wa umma wanakua na mustakbali nzuri wa maisha yao baada ya kustaafu serikali imechukua juhudi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara kwa wafanyakazi wa serikali, kupandisha pensheni, pamoja na kutoa mafunzo ya maandalizi kwa wastaafu ili kuweza kupata uelewa wa namna bora ya kujiandalia mazingira ya kuyakabili maisha baada ya kustaafu.
"Ili kuhakikisha mstaafu
anauwezo wa kuyakabili maisha baada ya kustaafu mwaka 2022 serikali iliongeza
kiwango cha mishahara kwa watumishi ambapo kwasasa kima cha chini cha mshahara
ni shillingi laki tatu, kuongeza pensheni kwa wastaafu kutoka elfu 90 hadi laki
1na 80, pamoja na kuandaa mafunzo ya watumishi ya kujiandaa na kustaafu",
alieleza.
Aidha aliwataka wastaafu hao
watarajiwa kuwatumia maafisa utumishi waliomo katika taasisi zao katika
kuhakiki taarifa zao kabla ya muda husika wa kustaafu ili kuepukana na
changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza, ikiwemo kuchelewa upatikanaji wa
mafao yao.
Hata hivyo aliwashauri washiriki wa
mafunzo hayo kuishi katika uhalisia wa
maisha yao, pamoja na kujiandaa kiakili,Kimwili na kijamii katika kukabiliana
na changamoto za maisha ya kila siku hususan baada ya kustaafu.
Alieleza kuwa wastaafu wanamchango
mkubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla, ndio maana serikali ikaweka mfuko wa
hifadhi ya jamii na kanuni ya utumishi
wa umma inayosisitiza kuagwa kwa wastaafu pamoja na kupewa zawadi, ili kuonesha
mchango na thamani zao katika maendeleo ya nchi.
Aidha alisisitiza viongozi wa taasisi
kuzitekeleza kanuni hizo kwa vitendo, ili kuenzi na kuthamini michango ya
wastaafu katika kipindi chote cha
utendaji wao wa kazi.
"Wastaafu wanamchango mkubwa kwa
jamii na taifa kwa ujumla, ndio maana serikali ya awamu ya nane ikaweka mfuko
wa hifadhi ya jamii pamoja na kuweka
kanuni ya utumishi wa umma
inayosisitiza kuagwa kwa wastaafu pamoja na kupewa zawadi, ili kuonesha mchango
na thamani zao katika maendeleo ya nchi, nasisitiza viongozi wa taasisi
kuzitekeleza kanuni hizo kwa vitendo",alifafanua.
Mapema akizungumza katika mafunzo
hayo Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF Nassor Shaaban
Ameir aliwahakikishia wastaafu watarajiwa
kua, mfuko wa ZSSF uko imara na unafanya kazi kwa mujibu wa Sheria na
kanuni ili kuhakikisha wanachama wananufaika ipasavyo na mfuko huo.
Alieleza utaratibu wa kuwepo kwa
mfuko wa hifadhi ya jamii ni utaratibu wa nchi nyingi ulimwenguni, uliokuja
kusaidia upatikanaji wa haki za msingi za watumishi baada ya kulitumikia taifa.
Aliongeza kua kwa mujibu wa tathmini
iliofanywa na mfuko huo mwaka 2024/2025 inaonesha kua mfuko huo uko imara kwa
muda wa miaka 50 ijayo, hivyo aliwataka wanachama wa mfuko huo kuendelea
kuwekeza katika ili kujihakikishia maendeleo Zaid.
Akiwasilisha mada kuhusu matayarisho ya kustaafu Mkufunzi msaidizi wa
mafunzo hayo Devid Kitomary aliwataka
wastaafu kua na mpangilio mzuri wa
matumizi ya fedha ili kuweza kuyakabili maisha baada ya kustaafu.
Aidha aliwataka washiriki wa mafunzo kuekeza katika maeneo tofauti ikiwemo
biashara, ufugaji, maeneo ya kilimo sehemu nyengine zenye tija pamoja na
kufuata ushauri wa kitaalamu katika
uwekezaji wao.
Nao washiriki wa mafunzo hayo
waliupongeza mfuko wa ZSSF kwa kuandaa mafunzo hayo yaliowasaidia kujifunza
kuhusu matayarisho ya kustaafu, na jinsi ya kukabiliana na maisha baada ya
kustaafu, ambayo yanaweza kuwasaidia katika kukabiliana na maisha baada ya
kustaafu.
Mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar
(ZSSF) ulianzishwa chini ya sheria ya
mfuko wa Usalama wa Zanzibar Na 2 ya 1998, ikiwa miongoni mwa kazi zake ni kuhifadhi michango ya wanachama
na kutoa mafao kwa wanachama wake, huku fao lake kuu likiwa ni fao la ustaafu na inafanya kazi katika visiwa vya Unguja na Pemba.
MWISHO
Comments
Post a Comment