NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
Viongozi wa kamati ya dini
mbali mbali kisiwani Pemba (Pemba Interfaith Committee), wameipongeza jamii
ya wazanzibari kwa kuendelea kuishi kwa
umoja na mshikamano, jambo lililoifanya Zanzibar kua mfano bora wa ustaarabu na
utulivu.
Tamko hilo lilitolewa
na Mwenyekiti wa kamati hiyo kwa upande
wa wanawake Amina Salim Ahmed katika
ukumbi wa mikutano wa Samail uliopo Gombani Chake chake Pemba,
katika kikao cha tathmini ya juhudi
zilizofanywa na kamati katika kushajihisha amani kabla, wakati na baadhi ya uchaguzi mkuu
uliofanyika Oktaba 29 mwaka huu.
Alieleza tamko hili ni
mwendelezo wa wito wa kila mara unaosisitiza kwamba amani tulionayo ni tunu na
kila mmoja anapaswa kuithamini na kuilinda kwa matendo ya kheri na kauli zenye
hekima.
Alisema kuimarika kwa
amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi kulitokana na juhudi kubwa zinazofanywa na
viongozi wa dini, Serikali, na wananchi katika kudumisha misingi ya maelewano
ambayo imeijenga Zanzibar.
Alifahamisha kua dini
zote zinahimiza upendo, ustahamilivu na kuheshimu utu wa kila mwanadamu, hivyo
ni vyema kila mmoja kuendeleza kuyaishi mafunzo haya katika maisha ya kila
siku.
"Dini zote
zinafundisha upendo, ustahamilivu na kuheshimu utu wa kila mmoja, hivyo ni
vizuri muendelee kuyaishi mafunzo haya katika maisha ya kila siku"
alieleza.
Aidha aliendelea
kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia marifa, busara na subira katika
kushughulikia mambo mbali mbali ya kijamii na kifamilia ili kudumisha amani
iliopo katika visiwa vya Zanzibar.
Hata hivyo alihamasisha matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kuelimishana na
kuhamasishana mambo yenye faida kwa jamii
pamoja na kuepuka taarifa zisizo za msingi au kauli zinazoweza kupunguza
heshima baina ya watu.
‘’Tunasisitiza matumizi
mazuri ya mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuelimishana na kuhasishana
yale yote yenye faida kwa jamii, pamoja na
kuepuka taarifa zisizo za msingi au kauli zinazoweza kupunguza heshima
baina ya watu’’,alisisitiza.
Aidha kamati
ilitoa pongezi kwa taasisi zote
zinazounga mkono juhudi za kukuza amani, kujenga uwezo wa vijana na kuimarisha
huduma za kijamii.
Awali akizungumza katika mkutano huo Mratibu Ofisi
ya Mufti Pemba Said Ahmad Mohamed aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuendelea
kuhubiri amani katika maeneo yao, pamoja na kutoa taarifa za viashiria vya
uvunjifu wa amani katika vyombo vya sheria.
"Endeleeni
kuhubiri amani katika maeneo yenu kwa kutumia njia mbali mbali ili kuhakikisha
amani iliopo inadumu, pia toeni taarifa ya viashiria vya kuvunjwa kwake katika
vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa", alieleza.
Akizungumza kwa niaba
ya wajumbe wa kamati hiyo Fadhil Juma Mohamed ambae pia Naibu katibu wa Jumuiya ya waalimu wa Madrasa
Pemba alisema, wamekua wakifanya juhudi za kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda amani kwa kuwafikia
watu wa makundi mbali mbali wakiwemo vijana na wanawake katika kipindi chote
cha uchaguzi mpaka kumalizika kwake.
Aidha waliahidi
kuendelea kutoa elimu hiyo kwa kila kundi lililopo katika jamii zao, kwa lengo
la kuhakikisha Zanzibar inaendelea kudumumu katika amani kwa maslahi ya nchi na
wananchi wake.
Kwa upande wake Afisa Mradi wa Swahili Coast unaosimamia kamati hiyo Khelef Nassor Rashid alisema, kamati hiyo inayojumuisha viongozi wa dini, Vijana na wanawake inafanya kazi ya kuhubiri amani pamoja na kushajihisha maadili, ambayo yatawafanya vijana kuishi katika ustaarabu wa jamii zao.
Kamati ya dini mbali mbali imekua ikifanya kazi ya kutoa elimu ya utunzaji wa amani kwa kushirikiana na shirika la Norway Church Aid (NCA) kupitia mradi wake wa Swahili Coast kwa mashirikiano ya ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
MWISHO
Comments
Post a Comment