MGOMBEA Uwakilishi
Jimbo la Chambani wilaya ya Mkoani, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ‘CCM’
Bahati Khamis Kombo, amesema kama akipata tena ridhaa, kundi la wanawake wajane
na vijana, atawaimarishia miundombinu ya kujiwezesha kiuchumi.
Akizungumza na
waandishi wa habari, mara baada ya uzinduzi wa kampeni eneo la Dodo Pujini,
alisema kupitia Ilani ya CCM, mikakati yake, ni kuona na kundi hilo
analiwezesha.
Alisema, ndani
ya jimbo hilo, anajua kuwa wapo vijana wasiokuwa na ajira na wale wajane
walionyimwa haki zao kwa njia moja ama nyingine, hivyo nia yake ni kuwawezesha.
Alieleza kuwa
moja ya mbinu atakazotumia ni kuwapa taaluma ya ujasiriamali na kuwatafutia mikopo,
ambayo itakuwa chachu ya kuendesha maisha yao.
Alisema njia
nyingine ni kuwawezesha kwa kazi za mikono, kama kufuma na kushona, ili iwe
njia sahihi ya kufikia ndoto zao.
‘’Hapa ninacho
hitaji kutoka kwa wananchi wa jimbo hili, kwanza waweke kando tofauti za vyama,
wanipe kura ili niendeleze mbinu za kuling’arisha jimbo letu,’’alifafanua.
Aidha mgombea
huyo, aliwataka wanachama wa vyama vingine, kuendelea kubakia na vyama vyao,
hadi miaka 100 ijayo, ingawa anachotaka ni kura za za ndio.
‘’Suala la
vyama kwa kila mmoja na chake hakuna shida, maana ndio demokrasia, lakini
ninachoomba waniazime kura, niwalipe maendeleo,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, mgombea huyo uwakilishi, alisema ahadi nyingine kwa wananchi wa jimbo
hilo, ni kuimarisha huduma za kijamii, ikiwemo maji safi na salama kwa vijiji
vyenye changamoto.
‘’Inawezekana
bado kuna vijiji kutokana na chakavu wa miundombinu huduma ya maji ni
changamoto, nipeni tena ridhaa kumaliza tatizo hilo,’’alifafanua.
Hata hivyo, alisema
kama akipata ridhaa, ataendelea na utamaduni wake wa kusaidia kambi za wanafunzi
wanaojiandaa na mitihani ya taifa, ikiwa ni njia moja wapo ya kuimarisha elimu.
‘’Pamoja na
sekta ya elimu, nitaangalia kwa vile vijiji ambavyo hata barabara ya kifusi ni
changamoto, ingawa naelewa kasi ya Dk. Mwinyi, haijakiacha hata kijiji kimoja,’’alifafanua.
Nae Mgombea Ubunge
wa Jimbo hilo Mohamed Abra-haman Mwinyi, alisema wakati umefika kwa wapiga kura
kuwaamini, ili kuliimarisha jimbo hilo.
Alieleza
kuwa, wananchi wa Chambani kwa kila mwenye macho kamili, atakubali kuwa sasa
jimbo hilo, limepiga hatua ikiwemo huduma za afya, elimu, barabara, huduma ya maji
safi na salama.
‘’Mimi
niwasihi wananchi wa Jimbo la Chambani wakichague Chama cha Mapinduzi na
wagombea wake wote, ili kuliendeleza jimbo hili, vyenginevyo watakuja juta,’’alisema.
Mapema Mwenyekiti
wa CCM wilaya ya Mkoani Ali Juma Nassor, alisema CCM imefikiwa vyema ndani ya
wilaya ya Mkoani, kwa kuwepo miundombinu kamili ya huduma za kijamii.
Kuhusu
uimarisha na matawi ya chama, alisema kwa sasa yaliomo jimbo la Chambani ni ya
kisasa na watendaji wanafanyakazi, kwenye mazingira bora.
Baadhi ya wananchi
wa Chambani, waliwataka wagombea hao kutokuwa na hofu ya kura zao, kwani
wanayakumbuka mazuri waliowatendea miaka mitano, iliyopita.
Hassan Juma
Mohamed, alisema zipo alama zilioachwa na Mwakilishi wao, ikiwemo ujenzi wa
skuli za maandalizi, ukarabati wa vyumba vya madarasa.
Nae Hussan
Haji Kombo, alisema katika eneo la shehia ya Ukutini, hadi leo wanaendelea
kutumia huduma ya maji safi na salama, baada ya kuchimbiwa kisima cha kisasa.
Kwa upande
wake Subira Mohamed Makame, alisema skuli ya maandalizi iliyopo Chumbageni,
wanaendelea kujivunia ikiwa ni ahadi, iliyotekelezwa na Mwakilishi wao.
Mwisho
Comments
Post a Comment