NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MKAGUZI wa shehia ya Mlindo Wilaya ya Wete Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi amewataka wananchi wa shehia hiyo kuendelea kukiamini kilimo kwani ndio njia pekee itakayowasaidia kuwainua kiuchumi.
Akizungumza katika muendelezo wa ziara yake ya ushirikishwaji wa jamii katika dhana ya ulinzi shirikishi wakati akikagua shamba la Hassan Hamad Hassan na familia yake, aliwapongeza kwa kuamua kujiwekeza kwenye kilimo na ufungaji kwa ajili ya kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.
Alisema kuwa, kilimo ni uti wa mgongo wa maendeleo katika nchi, hivyo ni vyema wakakiamini na kuelekeza nguvu zao zaidi huko, ili kiwaletee manufaa katika familia zao na jamii kwa ujumla.
"Ninachowashauri tu msitumie jembe la mkono kwa sababu mnachoka sana kwani mnatumia nguvu nyingi, hivyo mulime kwa kutumia zana za kisasa, pia mjitahidi kuzingatia uhifadhi wa mazingira kwa kutumia mbolea rafiki ili kilimo chenu kiwe endelevu na kuzalisha mazao bora," alisema Inspekta huyo.
Aidha aliishauri familia hiyo kuwashajihisha wanajamii wenzao kujiunga kwenye vikindi vya ushirika ili kufaidi fursa zinazotolewa na Serikali, ikiwemo pembejeo na mikopo isiyo na riba ambayo itawawezesha kuepuka baadhi ya changamoto.
Vile vile alimshauri mkulima huyo atumie nafasi yake kuihamasisha jamii kutunza amani hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu 2025, kwani bila ya amani hakuna shughuli ya maendeleo inayoweza kufanyika, hivyo ni wajibu wa kila mzazi kuwakataza vijana wao ili wasijiingize na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake baba wa familia hiyo ambae pia ni kiongozi wa shamba hilo, Hassan Hamad Hassan alisema, jambo analolifanya Mkaguzi huyo kwa kupita mabondeni kusikiliza changamoto zao zinazowakabili ni jema, kwani wanaamini kwamba ni njia moja wapo ya kutafutiwa ufumbuzi.
Akitaja changamoto zinazowakabili katika kilimo chao kuwa ni uhaba wa pembejeo, ukosefu wa maji ya kumwagilia, ukosefu wa mtaji pamoja mazao yao kuharibiwa na wanyama.
Aidha mkulima huyo ameeleza, licha ya changamoto zote hizo ingawa kilimo cha mboga mboga kimekuwa mkombozi wa familia yake kwani ndicho anachokitegemea katika kuendesha maisha yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto, matibabu pamoja na kujenga nyumba yake ya kuishi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment