NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
WAANDISHI wa habari wameshauriwa
kujifunza lugha za alama ili kuhakikisha uwepo wa uandishi
jumuishi katika kazi zao.
Wito huo umetolewa na Mratibu Baraza
la Taifa la Watu wenyeulemavu Pemba Mashavu Juma Mabrouk wakati akizungumza na
mwandishi wa habari hizi ofisini Chake
chake Pemba.
Alisema ili kuhakikisha watu wenyeulemavu wa uziwi
wanapata nafasi ya kutoa taarifa kuhusu
mafanikio na changamoto mbali mbali walizonazo ni muhimu kujifunza lugha ya
alama ili kurahisisha mawasiliano baina yao.
Alieleza kua, suala la kutoa na
kupata taarifa ni haki ya kila mmoja katika jamii, lakini bado inaonekana ni
changamoto hususani kwa watu wenye ulemavu wa uziwi, kutokana na kukosa fursa
hiyo, kutokana na baadhi ya waandishi kutokujua namna bora ya kufanya nao mawasiliano.
" Kwavile kutoa na kupokea
taarifa ni haki ya msingi ya kila mtu, ni vyema waandishi wa habari kujifunza
na kuijua lugha ya alama, ili kurahisisha upatikanaji wa haki hiyo kwa watu
wenyeulemavu wa uziwi", alisema.
Alisema kua, watu wenye ulemavu wa
uziwi ni sehemu ya jamii, ambapo wanakua na changamoto na masuala yao mbali
mbali wanayotamani yasikike katika vyombo vya habari kwa lengo la kuataka
ufafanuzi, au msaada lakini changamoto
zinabaki katika njia za mawasiliano, hivyo uelewa wa lugha ya alama kwa
waandishi wa habari itasaidia katika ujumuishi wao.
Alisisitiza kua, lengo la uandishi habari jumuishi
halitafikiwa iwapo hakutokua na miundombinu rafiki ya kuwawezesha watu wenye
ulemavu kuwasiliana vizuri na waandishi wa habari.
Aliongeza kua, ipo haja kwa waandishi kujifunza lugha hiyo
ili kuungamkono sera, sheria, katiba na mikataba mbali mbali ya haki za watu
wenye ulemavu ya kuhakikisha wanajumuishwa katika sekta zote nchini.
Aidha alitoa wito kwa watu wa karibu
wa watu wenye ulemavu wa uziwi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waandishi wa habari pale inapohitajika,
kwa kuwakalimania ili kuhakikisha saiuti
za watu hao zinasikika na kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake Naibu
Katibu Mkuu Jumuiya ya Viziwi Zanzibar (JUVIZA) Yahya Hamed Seif alisema, kutokujua lugha ya
alama kwa baadhi ya waandishi wa habari ni changamoto inayokwamisha ujumuishi
wao.
Alieleza kua, hali hii inawakosesha
ushiriki wa moja kwa moja katika kuwasilisha maoni yao katika vyombo mbali
mbali vya habari, na kupelekea kutopaza sauti zao ipasavyo.
" Wapo waandishi wanaozungumza
na sisi kupitia ujumbe mfupi wa maandishi au kukalimaniwa na watu wetu wa
karibu, hiii inatunyima ushiriki wa moja kwa moja katika mijadala au mazungumzo
ya kuwasilisha maoni yetu, hasa ukizingatia wao ni sauti ya wasio na
sauti", alieleza Yahya.
Aidha alitoa wito kwa waandishi na
taasisi nyengine zinazosimamia haki za watu wenyeulemavu kujifunza lugha ya
alama ili kujiongezea maarifa na kuhakikisha ujumuishi wa mazungumzo yao ya
kila siku.
Kwa mujibu wa kifungu cha 28(1) (d)
cha sheria cha Sheria ya watu wenyeulemavu ya Zanzibar ya mwaka 2022 kinaeleza
kua watu wenyeulemavu wanahaki ya kupata habari na mawasiliano kwa kuzingatia
aina ya ulemavu.
MWISHO
Comments
Post a Comment