NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MGOMBEA Uwakilishi wa Jimbo la Chambani kwa tiketi ya CCM Bahati
Khamis Kombo, amesema kama akipewa tena ridhaa ya kushika nafasi hiyo,
atahakikisha anaendeleza alipoishia kwa miaka mitano iliyopita.
Mgombea huyo uwakilishi aliyasema hayo leo Septemba 29,
mwaka huu uwanja wa mpira wa Dodo Pujini jimboni, kwenye uzinduzi wa kampeni
kwa jimbo hilo, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa Ilani ya CCM.
Alisema aliamua kuomba tena nafasi hiyo, baada ya kuona bado anadeni
la maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Chambani, katika huduma mbali mbali za kijamii.
Alisema, CCM kila baada ya miaka mitano, imekuwa
ikiwaletea Ilani, ambayo ndio mpango kazi mkuu wa utendaji wa kazi, na inatoa
dira ya miradi kadhaa inayokusudiwa kutekelezwa.
‘’Hivi sasa CCM, imeshaleta tena Ilani kwa ajili ya uchaguzi
wa mwaka 2025/2030 na ndani yake yamo miradi ya maendeleo, na ndio maana, naomba
tena ridhaa kuyaendeleza hayo,’’alifafanua.
Nae Mbunge mteule nafasi za wanawake mkoa wa kusini Pemba
Maryam Azam Mwinyi, amesema wagombea wote walioteuliwa na CCM, wanatosha kuwaletea
heshima ya maendeleo wananchi.
‘’Kwa hakika, wagombea kuanzia wale wa wadi, majimbo na ngazi
ya urais, wanayoheshima na uhakika wa kuwaletea maendeleo wananchi bila ya
ubaguzi,’’alifafanua.
Mapema Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mkoani Ali Juma Nassor,
alisema chama kimerudi tena kwa wananchi, kuwaomba ridhaa, ili kuendeleza
maendeleo.
Alieleza, CCM imewaletea madiwani, wawakilishi, wabunge na ngazi
ya urais, ili kuendelea kuzitatua changamoto za wananchi katika sekta mbali mbali.
Nae mjumbe wa Baraza kuu la UWT taifa Leila Mohamed Mussa,
amesema ndani ya CCM vitendo vinatosha na sio porojo, kama vilivyo baadhi ya
vyama.
Aidha alisema vipo vyama vimekuwa na maneno mazuri ambayo,
hayana msingi wala dira, na kuwaomba wananchi kuwapigia kura wagombea wote wa
CCM.
Akizungumzia Mgombea uwakilishi wa Jimbo la Chambani Bahati Khamis
Kombo, alisema amekuwa mweledi wa kudai haki za wananchi, bila ya ubaguzi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa UWT taifa Zainab Khamis Shomari, aliwashauri wananchi wa jimbo hilo, kuwachagua viongozi wote CCM, ili
kuendelea kulibadili jimbo la Chambani kimaendeleo.
‘’Leo tukilizungumzia Jimbo la Chambani, lenyewe linabadiliko,
maana viongozi wanaoliongoza wanakubalika kwani wanafanyakazi kwa nia thabiti,’’alifafanua.
Akiwanadi wagombea ubunge, uwakilishi na madiwani wa Jimbo la
Chambani Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa, Massoud Ali Mohamed, amesema
kura sio anasa bali ni kazi.
‘’Kama ni kazi, basi wanaoiweza ni wagombea wa Jimbo la Chambani
pekee, na hivyo kura zenu msizitupe kwa kuwapa wagombea, ambao kisha wanayahama
majimbo yao,’’alisema.
Hata hivyo, aliwashauri wagombea wa vyama vyingine, kushindana
kwa sera, na sio matusi wala kashfa, kwani watanzania hawahitaji malumbano.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Chambani Mohamed Abrhaman Mwinyi, amesema
anahitaji ushrikiano wa dhati kutoka kwa wananchi, ili kufanikisha ndoto za
wananchi.
mwisho
Comments
Post a Comment