NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
KAMISHNA wa Tume ya Haki za Binadamu Zanzibar Khatib Mwinchande amesema, maafisa wa utekelezaji wa Sheria kwa nyakati zote wanapaswa kutimiza wajibu walioekewa kisheria kwa kuhudumia jamii na kulinda watu wote dhidi ya vitendo vinavyoenda kinyume na Sheria, kwa kuzingatia kiwango cha juu cha uwajibikaji kinachohitajika na taaluma yao.
Akizungumza na maafisa wa Jeshi la Polisi Pemba katika mafunzo ya uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya Utawala Bora katika mchakato wa uchaguzi mkuu 2025 yaliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, kamishna huyo alisema, katika kipindi cha uchaguzi Jeshi la Polisi lina wajibu wa kujiepusha na migogoro isiyo ya lazima na badala yake wahakikishe usalama wa watu na mali zao katika kipindi chote cha uchaguzi.
Alisema kuwa, ni wajibu wa Jeshi la Polisi kusimamia uhuru, haki na amani ili wananchi waweze kutimiza haki yao ya kikatiba katika kuchagua viongozi wao, huku wanapotekeleza majukumu yao wazingatie maadili ya kazi, kuzingatia haki za binadamu na utawala Bora.
"Mafunzo hata yatawasaidia maafisa wa Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao na kuhakikisha haki za binadamu na misingi ya utawala uora inazingatiwa wakati wote wa mchakato wa uchaguzi," alisema Kamishna huyo.
Alieleza kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa wa maafisa wa Jeshi la Polisi kama maafisa wa utekelezaji wa Sheria kuhusu umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala uora katika uchaguzi mkuu 2025," alieleza.
Kamishna huyo alisema, Tume kwa kuzingatia Sheria ina jukumu la kuhamasisha hifadhi ya Haki za binadamu na wajibu kwa jamii pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora.
Alisema kuwa, ili uchaguzi uwe huru na wa haki kabla, wakati na baada, haki za binadamu zinapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutekeleza kwani uchaguzi ni mchakato muhimu katika nchi inaozingatia misingi ya demokrasia, uhuru, haki na amani, hivyo wananchi hutumia haki yao kushirikia katika shughuli za utawala wa umma moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliowachagua.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba SSP Kilogi Warioba aliwataka maafisa hao kuyatumia vyema mafunzo hayo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zao za kila siku, ili wawe ni wenye kufuata misingi ya Sheria.
"Tujue wajibu wetu ni nini, pia tunaelewa changamoto za utendaji wetu wa kazi nini, tujiepushe kuwa ni sehemu ya uvunjifu wa haki za binadamu, hii itatusaidia sana katika utekelezaji wa majukumu yetu," alisema Kaimu huyo.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Afisa Sheria kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Pemba, Mohamed Massoud Said alisema, askari Polisi ni wadau muhimu katika ulinzi wa haki za binadamu kwenye jamii, hivyo ni vyema kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu yao unazingatia Sheria, kanunue na muongozo, ili kuepuka uvunjifu wa haki za binadamu.
"Askari Polisi wakati wa chuchaguzi wana wajibu wa kulinda haki za binadamu, wanapaswa kutekeleza majukumu yao bila ya upendeleo wa mtu, kikundi au chama fulani cha siasa na wanapaswa kutoa ulinzi kwa raia wenye sifa za kushiriki katika uchaguzi bila ubaguzi, unyanyasaji wa kimwili, maneno au vitisho," alifafanua.
Akizungumzia manufaa ya Polisi kuheshimu haki za binadamu alisema ni kuboresha ufanisi wa Polisi na ni wajibu kisheria na kimaadili, Tanzania kuheshimiwa kimataifa, kujenga na kuimarisha mfumo wa utekelezaji wa Sheria uliojikita kwenye heshima, taaluma na uhalali, huimarisha ufanisi wa kazi zao pamoja na imani ya umma kuongezeka kwao.
Akitaja madhara na athari za ukiukwaji wa haki za binadamu unaweza kufanya utekelezaji wa Sheria kuwa ngumu, kuunda vizuizi vinavyokwamisha maendeleo ya utekelezaji wa Sheria kwa ufanisi, hudhoofisha heshima na uaminifu wa Serikali kimataifa, huiweka Serikali kwenye shinikizo la kimataifa kujibu mifumo ya ufuatiliaji wa haki za binadamu, kusababisha machafuko ya kiraia pamoja na kuwalazimisha Polisi kuchukua hatua za kukabiliana na matukio badala ya kuzuia.
Nao washiriki wa mafunzo hayo waliiomba Tume kutoa mafunzo hayo pia kwa vikosi vyengine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi, ili kila mmoja aelewe na kulinda haki za binadamu.
MWISHO
Comments
Post a Comment