IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WADAU wa kupambana na masuala ya udhalilishaji Pemba wametakiwa kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanafanikiwa kuondosha vitendo hivyo katika jamii.
Akizungumza katika mafunzo ya kupambana na udhalilishaji, Mratibu wa mradi wa Uwezeshaji wa Kisheria na Upatikanaji wa Haki (LEAP II) kutoka Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wete, Rashid Hassan Mshamata amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anasaidia mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Alisema kuwa, wamebaini kwamba kuna kesi nyingi hufutwa kutokana na kukosa ushahidi, hivyo kupitia mafunzo hayo yatasaidia makundi ya jamii waliyoyaanzisha, kuiwezesha jamii kujua umuhimu wa kutoa ushahidi kwa ajili ya kupatikana kwa hatia ya kesi hizo.
"Hili sio suala la mtu mmoja bali ni la kila mtu kwa upande wake ahakikishe anapambana na vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto, tushirikiane kuihamasisha jamii kutoa ushahidi ili kesi zipate hatia," alieleza.
Alifahamisha kuwa, makundi hayo ya jamii (CWGS) yatasaidia kuibuka kesi za udhalilishaji na kiziripoti, pamoja na kutoa elimu kwa jamii ili ipate uelewa juu ya masuala hayo.
Kwa upande wake Mjumbe kutoka Jumuiya ya WEPO Said Rashid Hassan alisema, ili kuweza kulimaliza janga la udhalilishaji hawanabudi kushirikiana, kwani kesi nyingi zinafutwa kwa kukosekana ushahidi.
"Kwenye haya makundi yetu kuna wadau mbali mbali wa kupambana na udhalilishaji, hivyo tunatarajia mabadiliko makubwa, tunaamini kwamba jamii itaelewa kasoro ambazo ni kikwazo na nini kifanyike, ili kesi zipate hatia," alifahamisha Mjumbe huyo.
Akiwasilisha mada ya haki za binadamu Hakimu wa Mahkama ya Wilaya Wete Maulid Hamad Ali alisema, watu wote ni sawa mbele ya Sheria, hivyo sio vyema mtu kuvunja haki ya mwenzake kwa namna yeyote ile.
"Kila mmoja anatakiwa ajitahidi kulinda haki za binadamu kwa sababu binadamu wote wamezaliwa wakiwa sawa, hivyo hawapaswi kunyanyaswa wala kubaguliwa," alisema Hakimu huyo.
Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Ali Hamad Mbarouk alieleza kuwa, ni haki ya kila mtu kulindwa, kwani anaponyanyaswa na kudhalilishwa ni kosa kisheria na anapaswa kuadhibiwa.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wakiwasilisha ripoti ya kesi hizo, walisema matukio bado ni mengi na wanajamii wanaendelea kuyaficha, hali ambayo inawapa nguvu wadhalilishaji kuendelea kuwakatili watoto.
Walisema kuwa, kupitia mradi huo, watahakikisha wanajamii wanapata uelewa zaidi juu ya masuala ya udhalilishaji na kuwa mstari wa mbele katika kutoa ushahidi ili kesi zipate hukumu.
Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Jumuiya ya WEPO wakishirikiana na UNDP chini ya ufadhili wa Irish Embassy ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa skuli ya Chasasa Wete.
MWISHO
Comments
Post a Comment