IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
VIJANA
wa kijiji cha Bwagamoyo shehia ya Piki Wilaya ya Wete Pemba wametakiwa
kujiepusha na changamoto ya udhalilishaji pamoja na makundi hatarishi, ili
waishi kwa amani katika jamii.
Akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji hicho,
Msaidizi wa Sheria Wilaya ya Wete (WEPO) Hamad Omar Ali alisema vijana
wanapaswa kujielewa na kujiepusha na mambo ambayo yataweza kuwapeleka sehemu
mbaya.
Alisema kuwa, ni vyema vitendo vya
udhalilishaji, wizi na madawa ya kulevya vinaweza kuwasababishia wasiishi kwa
amani katika maisha yao, kwani watakapokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria,
hivyo wajiepushe ili waishi kwa amani na familia zao.
‘’Vijana ni taifa la leo, hivyo
mnatakiwa kufanya mambo ambayo mtaisaidia jamii yenu kupata maendeleo na sio
kujiingiza katika mambo yasiyofaa, kwani mtajisababishia matatizo,’’ alisema.
Alieleza kuwa, wamekuwa wakichukua
juhudi mbali mbali za kuwaisaidia wanajamii kuwapa elimu ya kujua haki zao na
kujiepusha na changamoto, ili wafikie sehemu nzuri.
Aidha aliwataka wazazi na walezi
kuwahimiza watoto wao kwenda skuli na madrasa, jambo ambalo litawasaidia
kushughulikia masomo yao muda wote na kuepuka makundi maovu.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi kutoka
WEPO Hamad Mjaka Bakar alisema kuwa, wamekuwa wakienda vijijini kutoa elimu na
kushauriana katika kupambana na janga la udhalilishaji, kuwasaidia kupata haki
zao, kutoa changamoto zao na kutafuta njia mbadala ya kuwasaidia.
‘’Katika jamii kuna changamoto nyingi
na baadhi ya wanajamii hawajui namna ya kufanya ili waweze kuzitatua, hivyo
usaidizi huu wa kisheria utawaidia sana na kuweza kutatua shida zao,’’ alisema.
Mapema Mkurugezi wa WEPO Hemed Ali
Hemed alisema kuwa, kuwa janga la udhalilishaji linaendelea siku hadi siku,
hivyo wanaamini kwamba njia wanayoitumia ya kupita kwenye jamii kutoa elimu
itasaidia sana kupambana na vitendo hivyo.
‘’Tunazungumza na makundi mbali mbali
ikiwemo ya wazee, vijana, wanawake na watoto na kuwapa nasaha ili tuweze
kuibadilisha jamii wafuate maadili bora yatakayowasaidia katika malezi,’’
alieleza.
Nae msaidizi wa sheria Khamis Shamis Hassan alisema, lengo la mikutano hiyo ni kuhakikisha jamii inaelewa dhana nzima ya udhalilishaji na kutafuta njia ya kuweweza kudhibiti ili watoto wabaki salama.
Sheha wa shehia hiyo Asha Khamis
Nassor alieleza kuwa, kutokana na ushirikiano alionao kwa wananchi wake, kwa
sasa matendo mengi ya uhalifu yameondoka jambo ambalo anajivunia sana.
‘’Wanajamii ukiwaonea aibu basi
hufanyi lolote, kwa hivyo nimefanikiwa kuondosha magenge ya wizi na madawa ya
kulevya, vijana wanaosuka na kukata mikato isiyoeleweka, pia tumedhibiti
udhalilishaji kwa kiasi kikubwa,’’ alisema.
Sheha huyo aliwataka wanajamii
kuendelea kushirikiana na kutoa taarifa sehemu husika pale ambapo kutatokea
changamoto ili ziweze kutatuliwa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment