Na Nafda Hindi, ZANZIBAR
Mkurugenzi wa chama cha Waandishi Wahabari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ Dkt Mzuri Issa amesema kujitoa na kufanya kazi kwa bidii ni nyenzo muhimu itakayosaidia kuendeleza na kuimarisha Taasisi kusonga mbele kimaendeleo.
Dkt Mzuri amesema hayo wakati akifungua mkutano wa kuwatambulisha wanachama wapya waliopitishwa kwenye mkutano Mkuu wa mwaka 2024 kwa lengo la kuongeza utetezi wa haki za wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari.
Amesema Taasisi ili iweze kusonga mbele kimaendeleo inahitaji mashirikiano ya pamoja na uwajibikaji jambo ambalo linaweza kuleta mustakbali mwema kwa Taasisi, mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“TAMWA ZNZ ilisimama kwa kujitoa sisi wanachama, tumeanzisha jengo letu jipya kwa kukatwa mishahara sisi wenyewe,” Dkt Mzuri Issa, Mkurugenzi TAMWA ZNZ.
Nae Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ Asha Abdi amewahimiza wanachama hao kulipa Ada ya Uanachama kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kusimamishwa uanachama wao.
“ Miongoni mwa changamoto ni pamoja na wanachama kutolipa ada kwa wakati na kutoshiriki kazi za kuisaidia Taasisi kwa njia ya kujitolea,” Asha Abdi, Mwenyekiti wa Bodi, TAMWA ZNZ.
Mapema Mjumbe wa Bodi ya TAMWA ZNZ Hawra Shamte amewakumbusha wanachama hao kutumia fursa zilizopo katika Taasisi hiyo kwa lengo la kukuza uwajibikaji na kuleta maendeleo nchini.
Nao wanachama hao wameahidi kufanya kazi kwa pamoja na TAMWA ZNZ kwa kusaidia kuendeleza harakati za kutetea haki za binadamu zikiwemo za wanawake na watoto kupitia vyombo vya habari.
TAMWA ZNZ ilisajiliwa rasmi mnamo mwaka 2006, kwa sheria ya Society Act No 6 (1995), ina wanachama zaidi ya tisini kutoka Unguja na Pemba ambao ni wanawake na ni wataalamu wa masuala ya habari.
MWISHO
Comments
Post a Comment