IMEANDIKWA NA KHAULAT SULEIMAN, SUZA
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imekabidhi ng’ombe 153 wa maziwa kwa wafugaji 153
kisiwani Pemba, ambao wameletwa kutoka Afrika Kusini.
Ng’ombe hao
wamekabidhiwa wafugaji wa vikundi mbali mbali vya Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa
lengo la kuwawezesha wafugaji hao kufuga kibiashara na kuwaleta tija.
Akikabidhi ng’ombe hao Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamata Shame Khamis aliishukuru benki hiyo kwa kushirikiana na mradi wa TI3P na Shirika la Heifer International Tanzania
kwa juhudi zao za kumkwamua mfugaji wa kawaida kiuchumi na kumuwezesha kukuwa kibiashara zaidi.
Alisema kuwa, anaamini kuwa kupitia mkopo huo ng’ombe
kwa wafugaji hao kutaweza kuwakwamua kiuchumi, kwani watazalisha maziwa mengi
na kuuza, jambo ambalo litawapatia fedha zitakazowakwamua na maisha duni.
"Wafugaji nendeni mkafuge kwa tija ili
kujiletea maendeleo wenyewe na Taifa kwa ujumla, kuweni mfano kwa wafugaji na wakulima wengine,’’ alieleza Waziri Shamata .
Aidha Waziri huyo aliwataka wafugaji hao kushirikiana kulinda mifugo yao, ili kuepuka kupata maradhi, kuharibiwa, wizi na kusema
kwamba ikitokea mtu yeyote akanajis mifugo hiyo atachukuliwa hatua za sheria.
"Andaeni utaratibu mzuri kwa mifugo yenu kwani mwezi wa Oktoba watajifungua, hivyo wanahitaji mazingira ambayo hayatawaletea madhara wao na hata watoto wao, vifaa vya
uzalishaji wa maziwa vitafuteni kwa wingi, ili tuweze kupata engezeko
kubwa la uzalishaji wa maziwa nchini,”
alieleza.
Nae Meneja wa Benki hiyo Dames Damian alieleza kuwa, kwa kushirikiana na Shirika la Heifer international Tanzania, Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na
Mifugo, pamoja na chama Kikuu cha Wafugaji wa Ng’ombe cha pemba (PDCU), TADB imetoa mikopo ya ng’ombe wa kisasa wa maziwa (mitamba) wenye mimba kati ya miez 3-6 kwa riba nafuu ya asilimia tisa (9%), ambapo mkopo huo umegharibu shilingi 877,608,000.
“TADB imetoa ruzuku ya asilimia 25 kwa wafugaji hao,
hivyo wananchi ondoeni hofu kuhusu mikopo juu ya
kuwawezesha kwani tayari benki yetu imeshatenga fedha za kuwawezesha miradi yenu, ili iweze kuleta tija kwenu na Serekali,” alieleza.
Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Mifugo Pemba, Asha Zahran Mohamed alieleza, mradi huo utaweza kuwakomboa wafugaji kwa uzalishaji mwingi wa
maziwa na kuachana na maziwa yenye kemikali.
"Wizara ipo tayar kutoa mashirikiano ya kutosha kwa kutoa elimu ya matibabu pamoja na kutoa mbegu za shindano bure kwa ajili ya upandishaji wa mbegu kwa ng’ombe hao, hivyo wawe
tayari kushirikiana na wizara yetu,” alieleza.
Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, aliwataka wafugaji hao na Wizara husika kushirikiana pamoja, ili lile lengo la Serekali liweze kufikiwa la uzalishaji wa maziwa mengi kisiwani Pemba.
"Hatua hii tunategemea italeta tija kwa wananchi na
Serekali, hivyo sasa ni jukumu lenu kuwajibika ipasavyo ili mradi huo uwe na ufanisi zaidi,” alifahamisha
Mkuu huyo.
Akiwasilisha risala fupi kwa niamba ya
vikundi vilivyokabidhiwa ng’ombe hao, Meneja wa Ushirika Subira Talib
Khamis alieleza kuwa, kwa
kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo, tayari wameshapata mafunzo ambayo yatawawezesha kufuga na kuzalisha maziwa na nyama katika hali ya usalama zaidi, hivyo Serekali watarajie ongezeko la lita asilimia 15 kwa siku .
Zaidi ya vikundi saba vimekabidhiwa ng’ombe hao,
miongoni mwa hivyo ni kikundi kutoka Kifundi Konde, Tundwa Piki, kikundi cha Mola
Kinyasini, Tumeridhika kutoka Finya, Tuko Imara Kiungoni, Kiuyu na Kinyasini Jiamishe.
MWISHO.
Comments
Post a Comment