NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
AFISI ya
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar afisi ya Pemba, imewahakikishia wananchi wa
shehia ya Chonga wilaya ya Chake chake, kuwa kama wako tayari kushirikiana na
vyombo vya sheria, shehia yao itakuwa salama na vitendo vya kihalifu.
Hayo yameelezwa leo Septemba 6, 2024 na Mwendesha Mashtaka Dhamana wa mkoa wa kusini Pemba, kutoka afisi hiyo, Seif Mohamed Khamis, wakati akijibu hoja
za wananchi hao, waliooneshwa kushindwa na vitendo vya kihalifu vinavyofanywa
na watoto wao, kwenye mkutano wa kuwajengea uwezo wananchi hao.
Alisema,
kama kweli wananchi hao wameshakua tayari kuviondoa vitendo vya kihalifu kama
wizi, utumiaji wa dawa za kulevya, wajitayarishe kuona mabadiliko muda mfupi
ujao.
Alieleza kuwa,
atahakikisha ofisi yake, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kitengo cha
dawa za kulevya, wataunda timu ambayo wanawategemea wazazi na walezi, ili
kuiweka Kipapo salama.
Alisema, hata wao watafurahishwa mno, ikiwa wazazi sasa wako tayari,
kuhakikisha wanashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kwani uhalifu hauathiri
tu shehia hiyo pekee.
‘’Sisi baada
ya maelezo yenu, tumeona ipo haja ya kuhakikisha tunaunda timu kati yetu na Jeshi
la Polisi na kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, ili kuisafisha shehia ya Chonga na vitendo vya kihalifu,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Wakili huyo wa serikali, aliwakumbusha wananchi hao, kuhakikisha
wanawaibua wahalifu waliomo katika shehia yao, ili wakati ukifika wa operesheni
iwe rahisi kuwakamata.
Kwa upande
wake, Wakili wa serikali kutoka Afisi hiyo Zubeir Awam Zubeir, alisema hakuna
hatia yoyote mahakamani, pasi na wananchi kutoa ushahidi.
Akizungumzia
mkutano huo maalum, alisema lengo lake hasa ni kuwafuata wananchi walipo, ili
kusikiliza maoni yao, kama sehemu ya kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
‘’Tunapokuwa
afisini, huwa tunaona majalada tu ya watuhumiwa, lakini sasa tumeamua kufika
kwa wananchi wenyewe, ili watuhadithie na kutupa ushauri wa kuondoa matendo hayo,’’alieleza.
Hata hivyo
amewakumbusha wananchi hao, kutozifanyia sulhu kesi za udhalilishaji, na badala
yake zikitokezea tu, wananchi waziripoti katika vyombo vya sheria.
Mkuu wa dawati la jinsia la Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba Habiba Ali Said, alisema bado wapo wananchi wamekuwa wakizichelewesha kuziripoti kesi za udhalilishaji.
‘’Tumebaini,
baada ya mtoto kubakwa, mzazi anamtafuta aliyembaka mtoto wake, na baada ya
siku tatu hadi nne, ndio anaamua kufika Polisi kulalamika, kitendo cha
kuchelewa kwake, ameshapoteza asilimia kubwa ya ushahidi,’’alieleza.
Akijibu baadhi
ya maswali ya wananchi hao, alisema kama watashirikiana vilivyo na Jeshi la
Polisi, hasa katika eneo la ushahidi, vitendo vya kihalifiu vitamalizika katika
jamii.
Akifungua mkutano
huo, sheha wa Chonga Ali Juma Nte, alisema elimu hiyo kwa wananchi wake ni
muhimu, kwani shehia yao, imekuwa ikiongoza kwa uhalifu.
Baadhi ya
wananchi, walisema kasoro kubwa bado iko ndani ya Jeshi la Polisi, kwa
kutofuatilia vilivyo, baadhi ya kesi wanazoziripoti kituoni.
Abdalla Omar
Ali na mwenzake Said Omar Ali, walisema bado ndani ya Jeshi la Polisi, wapo baadhi
ya askari wanafanyakazi kinyume na kanuni zao, jambo linalowafanya kutokuwa na hamu
ya kushirikiana nao.
Kwa upande
wake, Salim Mbarouk Ali na Mohamed Shaib Kombo, walisema kwa sasa shehia yao, inatishia kwa kuwepo kwa matukio ya kihalifu, kama mauwaji na wizi.
‘’Kwa sasa haipiti
wiki moja, shehia ya Kipapo usisikie kuna mtu kauliwa, kupigwa, wizi wa kuku,
uvunjaji nyumba au watoto kudhalilishwa, hili sasa linatuchosha,’’walieleza.
Miongoni wa
majukumu makuu ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, ambayo imeanzishwa mwaka 2002,
kufuatia marekesbisho ya nane ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ni kuendesha
mashtaka, kusimamia vyombo vya dola ili kusiweko na matumizi makubwa ya nguvu.
Mwisho
Comments
Post a Comment