IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
MSAIDIZI
wa Sheria Jimbo la Wete Pemba Khamis Faki Simai amesema, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzubar zimekuwa zikichukua
juhudi mbali mbali katika kuhakikisha vitendo vya ukatili na udhalilishaji
vinaondoka nchini, ingawa jamii bado haijawa tayari.
Alisema kuwa, jamii inapaswa
kuthamini juhudi za Serikali hizo katika kupambana na janga la udhalilishaji,
kwani wanaoumia ni watoto ambao ndio legemeo lao la baadae na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa
vijana yaliyofanyika katika Ukumbi wa skuli ya Chasasa Wete, Msaidizi huyo wa
Sheria alisema kuwa, watu wamekosa hofu ya Mungu na ndio maana hata hawajali
kwamba kufanya udhalilishaji ni kosa.
‘’Watu wamekosa imani na ndio maana
haya matendo hayamalizi licha ya kupigwa vita na Serikali pamoja na wadau
wengine, hivyo tuendelee kupambana ipo siku wanajamii wataelewa kuwa hili ni
jambo baya,’’ alisema mkufunzi huyo.
‘’Ni muhimu sana kijana kupata
taarifa sahihi kuhusu mwili wake, mambo yanayoweza kuathiri haiba yake na afya
yake, kuepukana na mambo maovu yakiwemo uzinzi, wizi na madawa ya kulevya,’’
alifahamisha muwasilishaji huyo.
Aidha alisema kuwa, wanatakiwa
kujifahamu, kujitathmini na kujiamini, wafanye maamuzi sahihi, kujiwekea
malengo, kuhimili mihemko, misongo ya mawazo, shinikizo na mawasiliano.
‘’Mutumie muda wenu kufanya vitu
vitakavyowapatia faida kwenu na mufuatilie habari mbali mbali zitakazowasaidia
kujifunza na kuwa na upeo mkubwa wa kufikiri,’’ alieleza.
Mapema akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi
wa Jumuiya ya Wasaidizi ya Sheria Wilaya ya Wete (WEPO) Hemed Ali Hemed
alisema, anaamini kwamba mafunzo hayo yatawasaidia vijana kujipambanua na
kuungana pamoja katika mapambano dhidi ya udhalilishaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa WEPO
Khalfan Amour Juma aliwataka vijana wafuate maadili ya dini yao ili waepukane
na vitendo viovu ambavyo vinaweza kuwasababishia matatizo.
Nae Msaidizi wa Sheria Rashid Hassan
Mshamata alieleza kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha vitendo vya
udhalilishaji vinaondoka katika jamii, hivyo waungane pamoja kudhibiti.
Akitoa shukurani kwa niaba ya
washiriki wenzake Saumu Abdi Ali alisema wamejifunza vitu vingi ambavyo
vitawasaidia katika maisha yao na kuahidi kutoa elimu hiyo kwa wanajamii, ili
kufikia lengo la mapambano dhidi ya udhalilishaji.
MWISHO.
Comments
Post a Comment