IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WANAKIKUNDI
cha kuhifadhi mazingira cha ‘Nyange Cooperative’ waliopo shehia ya Mjiniole wilaya
ya Chake Chake wameiomba Serikali kuviunga mkono vikundi vyote
vinavyojishughulisha na uhifadhi wa mazingira kwa kuwachukulia hatua za kisheria
wananchi wanaokata miti ambayo hupandwa na vikundi hivyo kwa lengo la kuzuia
maji ya bahari yasipande juu kwenye mashamba yao.
Walisema kuwa, wamekuwa wakipoteza
nguvu nyingi kupanda miti ya mikoko kwa ajili ya kurudisha uoto asili na kuzuia
mabadiliko ya tabianchi, ingawa wamekuwa wakirudi nyuma kutokana na wananchi
kuikata huku wakiendelea kuachwa bila ya kuchukuliwa hatua.
Wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi wanakikundi hao walieleza kuwa, hakuna siku hata moja waliyoona watu
wanaokata miti hiyo wakichukuliwa hatua za kisheria licha ya kuzifikisha kesi
hizo sehemu husika.
‘’Kilichotushanga ni kwamba, siku
moja tulikata miti kidogo ili tupate pesa angalau ya kununulia vifaa
tunavyotumia lakini wananchi walikwenda kutushtaki na tulichukuliwa, sasa kwa
nini tunapopeleka kesi za wizi tunapuuzwa?, kwa kweli inauma,’’ walisema.
Mmoja wa wanakindi hicho Hamad Khatib
Hamad alisema, wao ndio waliopanda miti hiyo ingawa walipoikata walichukuliwa
kwenda kujielezea lakini hawakupatikana na hatia, hivyo waliiomba mamlaka
husika wanapowafikishia kesi wasipuuze.
Alieleza kuwa, itafika mahala na wao
watachoka kupanda miti, hali ambayo itasababisha maji ya bahari kupanda juu na
kuingia kwenye mashamba ya wananchi na kuharibu vipando vyao.
Mwanakikundi Hadia Ali Hamad alieleza
kuwa, ili waendelee kuotesha miti hiyo ipo haja kwa Serikali kuwawekea udhibiti
ili miti isikatwe kwa sababu wanapoteza nguvu nyingi kupanda bila mafanikio
yeyote.
‘’Hatujawahi kunufaika na miti hiyo
kwa kujipatia kipato, bali tumeona kwamba manufaa makubwa ni kuhifadhi
mazingira yetu, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo tunaomba
tuungwe mkono,’’ alifahamisha.
Nae mwanakikundi Khadija Henock
Maziku alieleza kuwa, zaidi ya miti ya mikoko 5000 imeibiwa katika shamba hilo
tangu walipoanza kupanda, jambo ambalo linawafanya wakose nguvu ya upandaji.
‘’Wanajamii na wakulima wa tungule
nao wanatuharibia sana, hivyo elimu itolewe kwa vijana juu ya umuhimu wa
kuhifadhi mazingira, ili tudhibiti hali hii, kinyume chake, maji yatapanda juu
tu kwenye makaazi ya watu,’’ alifafanua.
Alieleza kuwa, anaweza kuwakuta wizi
ingawa hawezi kuwakamata kwani wanakuwa na silaha, hivyo huwaacha tu licha ya
kuwa anaumia moyoni.
Aliishauri Serikali kuwaelimisha
wananchi juu ya kuhifadhi mazingira na kuwatoza faini kwa wale wanakamatwa kwa
wizi wa miti hiyo, ili eneo libaki katika hali salama.
Kwa upande wake sheha wa shehia hiyo
Hamad Said Mgau alisema kuwa, wanajitahidi kuwaelimisha wanajamii juu ya suala
ya uhifadhi wa mazingira ingawa binadamu hawezekani.
‘’Kila siku tunawakataza na
tunawaeleza na athari zake lakini bado wanaendelea kuikata miti na hawa
wanaopanda wanasema wamechoka kushtaki, kwa hiyo wanawaacha tu, jambo ambalo ni
hatari kwetu,’’ alieleza.
Afisa Mkuu Idara ya Misitu Pemba Samira
Makame Juma aliwataka wanakikundi hao kushirikiana pamoja katika ulinzi na
kutoa taarifa Idara ya Misitu ili watendaji wao wafike kuangalia athari iliyotokea
na kuchukua hatua ya kuwaita walioharibu au wa pande zote mbili kusikiliza
malalamiko yao kwa ajili ya hatua stahiki.
‘’Tushirikiane, wanakikundi wajiwekee taratibu
na wajulikane na uongozi wa shehia, wajue wanafanya nini, wakifanya hivyo
wanaweza kuungana na sheha pamoja na Idara ya misitu kuhakikisha eneo hilo
linahifadhiwa kwa taratibu maalumu,’’ alifafanua.
Mkuu huyo aliwataka wananchi
kuhifadhi misitu ya juu na ya baharini (mikoko) na kutumia sheria pale ambapo
patatokea athari ya uharibifu, ambapo wanatakiwa kujua kuwa miti hiyo sio mali ya
mtu mmoja bali ni ya wote kwani yanayawanufaisha wote katika kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi.
Shehia hiyo ina wananchi 2,800 ambapo
wanajishughulisha na kilimo cha mazao mbali mbali, uvuvi pamoja na uhifadhi wa
mazingira.
MWISHO.
Comments
Post a Comment