Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma
amelitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kuharakisha masuala ya upelelezi kwa kesi za
vitendo vya ukatili na udhalilishaji ili kuona zinamaliza ndani ya muda mfupi.
Kauli hiyo aliitoa jana katika kilele cha maadhimisho ya kufunga siku 16 za
harakati za kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto
yaliyofanyika katika kijiji cha Muyuni Wilaya ya Kusini Unguja.
Mhe. Riziki alisema taarifa za Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
zinaonesha hali inatisha kwani katika kipindi cha mwezi Januari hadi Octoba 2023
jumla ya matukio 1,620 yameripotiwa ambapo matukio 1,360 yanahusu watoto,
194 wanawake na wanaume 77.
Alisema pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi lakini bado
ucheleweshwaji wa upelelezi wa matukio hayo umekuwa mkubwa hali ambayo
inapelekea kesi nyingi kukaa muda mrefu katika vituo vya Polisi Zanzibar.
Alisema kuendelea kwa hali hiyo itaweza kuathiri malengo ya Serikali katika
mapambano ya kuondoa vitendo hivyo pamoja na kuwatia hatiani watu
wanaothibitika kutenda vitendo vya ukatili na kudhalilisha ndani ya nchi.
Aidha alisema ipo haja ya kutambua na kuweka kampeni maalum za kuyakabili
matendo ya udhalilishaji wa Kijinsia kwa kuweka nguvu kazi na kampeni isemayo
“Wekeza katika Kuzuwia Ukatili Dhidi ya Watu Wenye Ulemavu” na “Nijuze
Nijilinde Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia”.
Alieleza kwamba kundi hilo la watu wenye ulemavu limekuwa na changamoto
kadhaa ambazo zimekuwa zikiwakabili na hivyo haja ya tafakuri ya kina
inahitajika katika kumkomboa mtu mwenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili
wa Kijinsia.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdalla, alisema bado
matukio ya udhalilishaji yanaongezeka ikiwemo matukio ya kubaka, kunajisi
ambapo Wilaya ya Mjini na Magharibi ‘A’ na ‘B’ zinaongoza kwa kesi hizo
nyingi.
Alieleza kwamba wakiwa wanahitimisha kilele cha siku 16 lakini bado
mapambano yanaendelea hivyo ni lazima jamii kwa pamoja wanaumme na
wanawake wote wanalazimika kupambana na matendo hayo kwani bado kuna kazi
kubwa ya kufanya ili kuhakikisha matendo hayo yanaondoka nchini.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kusini Unguja, bi Radhia Rashid Haroub,
aliipongeza Wizara hiyo kwa kuadhimisha siku 16 za kupinga vitendo vya Ukatili
na Udhalilishaji katika mkoa huyo. Alisema bado nguvu za mapambano
zinahitajika kwani Mkoa wa Kusini matukio hayo yameongezeka mwaka jana
2022 kulikua na jumla ya matukio 1,320 ambapo kwa mwaka huu yamefikia
matukio 1,620 sawa na ongezeko la asilimia 16.
Kwa upande wa wanaharakati wa kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji
akizungumza kwa niaba bi Amina Yussuf Ramadhani alisema jamii wameshapat
uwelewa wa kuripoti matokeo hayo lakini bado tatizo la muhali linaendelea
kujitokeza na kusababisha baadhi ya kesi kusuluhishwa katika ngazi ya familia.
Comments
Post a Comment