NA HAJI
NASSOR, PEMBA@@@@
MASHEHA
wa shehia za Wawi na Wesha wilaya ya Chake chake Pemba, wameahidi kuwa watakula
sahani moja kisheria, na mtu yeyote atakaekamatwa akihujumu nguzo zenye majina
ya mitaa katika shehia hizo.
Walisema,
baadhi ya wananchi wamekuwa wakijaribu kuzing’oa nguzo hizo kwa maksudi, na
kuwataka waache mara moja tabia hiyo, kwani atakaekamatwa, sheria itachukua
mkondo wake.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, kufuatia katika baadhi ya
vijiji kung’olewa nguzo hizo, walisema yeyote hatovumiliwa.
Sheha wa
shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, alisema tayari katika moja ya vijiji vyake
nguzo iliyokuwa na jina la kijiji imeshang’olewa na kuwataka wananchi, wairejeshwe
mara moja.
Alieleza
kuwa, kwa vile serikali imetumia gharama kubwa kutengeneza nguzo hizo kwa ajili
ya kurahisisha shughuli mbali mbali, hatokaa kimnya hadi itakaporejeshwa.
‘’Niwaombe kama
kuna mwananchi anajua taarifa za kuibiwa kwa nguzo hizo, aje anipe kwa kina,
kwani jambo hilo halitokuwa dogo kama haijarejeshwa,’’alisema.
Katika hatua
nyingine, sheha huyo wa shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, alielezea
kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya wananchi kuzitikisa tikisa nguzo hizo.
Sheha wa
shehia ya Wawi Sharifa Waziri Abdalla, alisema wapo wananchi wamekuwa
wakizitumia nguzo hizo hata kufungia wanyama wao, jambo ambalo sio sahihi.
Alisema,
anazo taarifa kuwa zipo baadhi ya nguzo huangushwa kwa makusdi, na nyingine
kuchukuliwa, ambapo mwananchi huyo atakayebainika atafikishwa Polisi kujibu.
‘’Ukiharibu
nguzo yenye jina la mtaa, ama ukiiba itakuwa umeiba mali ya serikali, hivyo
lazima kwa kuhujumu huko mali hizo, ufikishwe mbele ya vyombo vya sheria,’’alifafanua.
Aidha sheha
huyo aliwataka wananchi kila mmoja, kuwa mlinzi wa mwenzake, kwani nguzo hizo
zenye majina ya mitaa ni kwa manufaa ya watu wote wakiwemo wageni.
‘’Tuelewe
kuwa, majina haya ya mitaa yapo kwenye mtandao wa serikali na faida yake kubwa
ni kuwarahisishia wageni kwa kufuata nguzo za mitaa hadi anakokwenda,’’alifafanua.
Baadhi ya
wananchi wa shehia hizo, walielezea kusikitishwa kwao, na baadhi ya wananchi
wenzao, kuihujumu miundo mbinu ya mitaa na vijiji.
Khadija Issa
Msellem wa Wesha, alisema hakuna haja kwa wananchi wenzao, kuzing’oa nguzo hizo,
kwani moja ya faida kubwa ni mitaa kuwa na majina ya kudumu.
Amina Omar
Mzale wa shehia ya Wesha, alisema ni vyema atakaebainika kuihujumu miundombinu
hayo, kuchukuliwa sheria kali, ili iwe funzo kwa wengine.
Askari
shehia ya Wawi Issa Ahmad, alisema kimsingi nguzo ni mali ya wananchi,
wanayohaki ya kuzilinda na kuhakikisha hakuna anaeziharibu, kwani athari yake
ni kubwa.
Nassor
Khamis Mohamed, alisema wakati umefika sasa wa wananchi kuelimishwa juu ya
umuhimu wa nguzo hizo, kwani wengi wanafikiria ni kama urembo.
Akizundua
zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, aliwataka
wananchi kujali gharama iliyotumika katika kutengeneza nguzo hizo.
Mwisho
Comments
Post a Comment