NA AMRAT KOMBO, ZANZIBAR@@@
Binaadamu siku zote hutakiwa ajuwe alipo na wapi anataka
kwenda. Katika maisha hii huwa ni ndoto ambayo humpelekea mtu kupitia mengi,
baadhi yao yakiwa ni mtihani mmoja baada ya mwengine.
Jambo muhimu ni kutokata tamaa na kuendelea kupambana na
pale unapoteleza au kuanguka unapaswa kuinuka na kuendelea na safari huku ukiwa
na matumaini ya siku moja utafika huko unapokusudia kwenda.
Bi Huzaima Ali
Hamdani, miaka 51, ambae ni mjasiria mali wa uchoraji piko na biashara ya vyakula, ni mmoja wa wanawake
aliyekabiliana na mithani mingi katika safari yake ya uchoraji aliyoianza 1997.
Kila alipokutana na kikwazo hakukata tamaa, bali aliendelea
kupambanana na kuanza biashara nyengine,
ikiwemo ya kuuza urojo, maandazi na chapati, ili kuhakikisha anajipatia kipato
cha halali cha kujiendesha kimaisha.
"Kila siku asubuhi nauza urojo, mandazi chapati na
juisi na ikifika jioni nauza supu ya utumbo na chapati,"alisema.
Alipomsikia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akisema wachoraji watapewa mfuko wa
kuendeleza biashara zao hakusita kufuatilia kwa kwenda halimashauri kujaza fomu
ambayo imeshafikishwa benki na anayo matumaini
ya kupata mkopo utakaomsaidia kuimarisha biashara yake.
Wakati akiendesha biashara zake alikuwa ameshajiunga katika
Chama cha Democrasia na Maendeleo ( Chadema) akiwa mwanachama katika mwaka 1996
na baada ya muda alichaguliwa kuwa kiongozi katika tawi.
Wazazi wake walimuwekea pingamizi hapo awali, lakini hilo
halikumkatisha tamaa kwa vile alikuwa na ndoto ya kuwa kiongozi na alifarajika
alipoona mume wake hakuwa na pingamizi na akawa karibu naye.
Alipokuwa kiongozi katika tawi akawa bado hakuridhika na
nafasi hio na akaingia katika kinyang’anyiro cha kugombea ubunge katika mwaka
2020 na ingawa hakubahatika kuipata nafasi hio hakukata tamaa na kuamini ipo
siku ndoto yake itatimia.
"Nilifanikiwa
kuweka mikutano kutokana na biashara zangu,na nikafanya kampeni ya
kugombania ubunge katika mwaka 2020, nikabahatika kupata kura 400, japo
hazikutosheleza lakini sikuanguka sana na jambo ambalo linanifanya mwakani
nigombanie tena ." anasema
SABABU ZA KUINGIA KATIKA SIASA
"Hadi leo ukienda katika hosptali kitanda cha
wajawazito kimoja wanakaa watu watatu. Hili jambo linanikera na nimeamua nikiwa
kiongozi mwenye nafasi ya kusaidia kulitatua nitasimama kidete kuhakikisha
usumbufu huu unaondoka’’, alieleza.
Licha ya kutopata nafasi ya kuwa mbunge mwana mama huyu
anaendelea kuongoza wenzake kwa kutoa elimu kwa wanawake wenzake ya kujitambua
na kujuwa kwamba wanayo haki ya kuwa viongozi.
Pamoja na hayo anashirikiana na vijana na kuwasaidia
anapokuwa na uwezo. Mfano mmoja ni wa kuona vijana wanashiriki katika michezo
na aliwashaijisha vijana wa jimbo l la Welezo shehia ya Mchokichini, Tumbatu,
kwa kuwapelekea mipira na kuwafahamisha umuhimu wa kujihusisha na siasa kwa
vile ndio msingi wa maisha yao ya kila siku.
Miongoni mwa mafanikio ya harakati zake za kuongoza wenzake
Bi Huzaima ameweza kuwashawishi wanawake
10 kuingia katika uongozi.
"Nilipoenda Tumbatu waliniomba niwapatie ofsi na kwa
vile uwezo wangu bado ni mdogo, nilichanga na kuwapelekea shilingi 300,000
zilizosaidia matengenezo ya ofsi hiyo, ingawa mwisho wa siku hawakunishika
mkono katika safari yangu ya kutaka kusonga mbele kwenye uongozi. Hata hivyo
sijakata tamaa," aliongeza.
Alisema uzoefu alioupata ni unapofanya kazi kwa bidi
wanatokea wenzako wanaokuwa hawafurahii na hukuona kuwa ni mtu unayejiona
badala ya kuthamini kile unachokifanya.
Alieleze kusikitishwa kwake na kuona bado jamii inatawaliwa
na mifumo dume ambayo humtenga mwanamke na hata kumuona hana haki ya kuingia
kwenye safu ya uongozi na miongoni mwa wenye kufanya hivyo ni wanandoa.
"Lakini pia wapo wanawake ambao wamejijengea hofu ya
kuingia kwenye siasa kutokana na kuwa na uelewa mdogo na kuona siasa ni kwa
ajili ya wanaume pekee yao,’’alieleza.
MAFANIKIO
Miongoni mwa mafanaikio aliyoyapata ni kujifunza mengi
kupitia siasa na kuwa mtu anayejiamini na kuwa na ujasiri wa kuweza kuzungumza
pahala popote.
Neema Said Mwishehe ambae ni mjumbe wa Baraza kuu la Taifa kupitia Chadema alikuwa mjasiria mali
wa vyakula na kabla ya kuingia katika siasa alikuwa anauza urojo na wakati huo
aliwaona wanachama wa Chadema walivyokuwa wanawahamasisha watu. Hapo ndipo alipohamasika na kujikuta anaingia kwenye
siasa katika mwaka 2018 wakati akiwa kijana mbichi wa miaka 18.
Alipojiunga na chama hicho alianza kutumikia nafasi
mbalimbali, ikiwemo ya Mwenyekiti wa Shehia ya Kijitoupele na Mwenyekiti wa
jimbo kwa upande wa vijana na baaadaye Mwenyekiti wa Wilaya hadi kufikia mjumbe
wa Baraza Kuu la Taifa la chama hicho.
Akiwa katika nafasi hizo aliamua kuachana na biashara zake
kutokana na a majukumu kuongezeka huku akiwa na shauku ya kujiendeleza
kwenye elimu na siasa.
Alisema miongoni mwa
watu waliomshajihisha kuingia katika siasa ni Huzaima ambae alimuelewa
kuwa ni mwanamke mwanamke jasiri, anaejiamni na kuwajibika katika uongozi wake
na hali hio ilimpeleeka kumfanya mmoja
wa watu waliokuwa wanampa ushauri.
Hata hivyo, safari
yake ya uongozi haikuwa nyepesi kwani alikumbana na vikwazo ambavyo wanawake wengi hukutana navyo
katika siasa, hasa wale wenye umri mdogo na alipata shida kuwaongoza watu
waliomzidi umri.
Alisema miongoni mwa faida aliyoipata katika chama chake ni elimu ya kupiga vita vitendo
vya ukatili na udhalilishaji kwa wananchi na kumepelekea kuwa mstari wa mbele
katika mapambano ya kutokomeza vitendo hivyo.
Hivi sasa anajitayarisha kugombania uwakilishi katika jimbo
la Kijitoupele kupitia tiketi ya chama chake.
Asiata Said Abdallah ambae ni mueka hazina wa Kanda ya
Unguja katika CHADEMA alisema aligombea
nafasi mbalimbali baada ya kushawishiwa na Huzaima ambaye alimuona kuwa ni
mwanamke anayependelea maendeleo kwa wanawake wenzake.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Shukuru Malonda, alisema mwanamke ana nafasi ya uongozi katika kanisa
na kijamii na kutoa mfano wa viongozi wa kike, waliongoza na kuwasimamia watu
katika dini ya Kikirsto. Miongoni mwao ni Esta ambae alikuwa Malkia na Debora
alikuwa Nabii.
"Katika kanisa letu tumewachaguwa wanawake wawili na wanaume wanne ambao ni wachungaji na Wainjilist 12, wanawake watano na wanaume saba, ndio
wanaoongoza kanisa," alisema.
Mratibu wa kuinua
wanawake katika uongozi katika Chama Cha Wandishi wa Habari Wanawake
Tanzania (TAMWA Zanzibar), Maryam
Ame, alisema wanatoa elimu kwa
wanawake wanaotaka kuwa viongozi ili
wajitambua na kutatua changamoto za kiuongozi.
Alisema hadi wanawake 172 Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo ya uwongozi ambayo
yamewasaidia kutambua vikwazo wanavyoweza kukutana navyo na namna ya
kukabiliana navyo.
Aliwanasihi wanawake wanaotaka kuingia kwenye uongozi
kutokuwa na hofu kwani hio ni haki yao iliyoainishwa katika katiba na mikataba
mbali mbali ya kikanda na kimataifa ambayo nchi yetu imeiridhia na kuamua
kuitekeleza.
MWISHO
Comments
Post a Comment