Na Nafda Hindi, Zanzibar @@@@
Chama cha waandishi wahabari wanawake Tanzania TAMWA ZNZ,
wamekutana katika mkutano wao wa kila mwaka kutathmini utekelezaji wa shughuli
zake kwa mwaka unaokwisha 2023, kujadili
maendeleo, changamoto pamoja na kupanga mikakati imara ya utekelezaji wa mwaka
ujao 2024.
Mkutano huo wa siku mbili uliofanyika katika ukumbi wa TAMWA
uliowashirikisha wafanyakazi wa TAMWA ZNZ akiwemo Mwenyekiti, Wajumbe na wadau
kutoka Asasi mbali mbali za kiraia.
Mapema akifunguwa mkutano huo Mkurugenzi wa Chama cha waandishi
wahabari wanawake TAMWA ZNZ Dk Mzuri Issa amesema udhalilishaji ni janga katika
jamii hivyo wanaharakati wa kupinga vitendo hivyo wasichoke na waendelee
kujitoa kwa lengo la kuwalinda watoto.
“Udhalilishaji bado upo unaendelea hivyo wanaharakati
wasichoke kupambana ili kuwasaidia watoto na wanawake kuhakikisha wanaondokana
na vitendo hivyo,” Dk Mzuri Issa.
Nae Afisa mradi wa
kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji kutoka TAMWA Zaina Salum amesema
wanakumbana na changamoto kadhaa katika kupiga vita vitendo hivyo ikiwemo
uwajibikaji kwa watendaji wanaosimamia vitendo hivyo hasa katika eneo la utoaji
wa hukumu Mahakamani.
“Mahakama bado hawajawa na mfumo bora wa kutoa hukumu katika
kesi za udhalilishaji kwa mfano utasikia mashahidi hawakufika mahakamani au
mtuhumiwa katoroka ni vitu ambavyo kwa kweli vinarudisha nyuma wanaharakati na
jamii kwa ujumla,” Zaina Salum.
Mkufunzi kutoka Idara ya Mawasiliano na Mafunzo ya Habari Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Imane Duwe amesema vyombo vya habari vitimize wajibu wake kwa kuripoti kwa kutowajibika kwa vyombo vya sheria kuhusiana na vitendo vya udhalilishaji ili wajirekebishe na kufanya ipasavyo.
“ Vyombo vya habari vinajitahidi kuripoti vitendo hivyo
lakini bado vitendo vinaendelea hivyo wachukuwe jukumu la kuwakumbusha wajibu
wa watendaji kutoka vyombo vya sheria,” Imane Duwe.
Wadau kutoka Asasi za Kiraia wakitoa mchango wao
wameipongeza TAMWA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuisadia jamii kupambana na
vitendo vya udhalilishaji na kuziomba Taasisi nyengine kuiga mfano huo kwa
lengo la kuisaidia jamii.
“TAMWA ina inafanya vizuri katika kazi zake za kuisaidia
jamii na kuonesha njia juu ya mambo mbali mbali ikiwemo vitendo vya ukatili kwa
wanawake na watoto,” Wadau.
Aidha Afisa Mradi wa kuwawezesha wanawake kugombea nafasi za
Uongozi (SWIL) Maryam Ame Chuom amesema wanatoa mafunzo mbali mbali ya
kuwajengea uwezo wanawake kushiriki katika nafasi za maamuzi na tayari wanawake
mia moja sabiini, ikiwa Unguja ni mia moja na sabiini kwa Pemba na wameahidi
wanawake kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Tumetowa mafunzo kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ni
wanawake 45 kwa Unguja na 35 kwa Pemba na awamu ya pili ni wanawake 55 kwa
Unguja na 35 Pemba,” Maryam Ame.
Kwa upande wa Mradi wa haki ya Afya ya uzazi kwa wanawake na
wasichana Afisa Mradi huo Zaina Mzee amesema wametowa mafunzo kwa waandishi
wahabari hamsini na nane kwa Unguja na Pemba, wanawake ni arubaini na sita na
wanaume ni kumi na mbili.
“Mafanikio tumeyapata
kwa waandishi kuibuwa changamoto mbali mbali zinazoikumba sekta ya Afya na
wanawake pamoja na wasichana na baadhi yao zimepatiwa ufumbuzi kama kituo cha
Afya Wesha Pemba kupatiwa huduma ya maji ambapo awali haikuwepo kabla ya ziara
ya waandishi.” Zaina Mzee.
Kwa upande wa Mradi wa KIJALUBA ISAVE, Nayrat Abdula ambae
ni Afisa Uwezeshaji wanawake Kiuchumi wakishirikiana na Shirikisho la Jumuiya
ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJIWAZA) Amesema mradi huo umekuja kuwasaidia
wanawake wenye ulemavu ambao wameonekana kutengwa kwa muda mrefu
Aidha Sabrina Mwinjuma Meneger mradi wa VIUNGO amesema
wamesaidia wanawake wapatao …kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri kupitia mradi
huo kuondokana na utegemezi hasa kwa vijana na wanawke kwa Unguja na Pemba.
Katika mradi wa VIUNGO umewafikia wanawake elfu tatu mia
tisa na tisini na nne kwa Unguja na
Pemba elfu sita mia moja na nane.
Tatu Mtumwa ambae ni Afisa mradi wa kuwajengea uwezo
waandishi vijana kuripoti na kuandika habari za wanawake kugombea nafasi za
Uongozi amesema wametoa mafunzo kwa waandishi wahabari wapatao ishirini na nne,
wanawake ni kumi na tisa na wanaume ni sita, Unguja ni kumi na nane na Pemba
sita.
Hata hivyo kitengo cha Habari na Mawasiliano kutoka TAMWA
wamesema wamejipanga vyema katika mwaka ujao kuhakikisha wanaitumia fursa ya
mitandao ya kijamii ipasavyo kwa lengo la kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo na
jamii kupata ujumbe wa haraka kwa kile wanachokifanya.
Kwa mujibu wa Mkuu wa
Utawala na Fedha Mohammed Khalid amesema TAMWA imeteleza miradi tisa kwa mwaka
2023 ikiwemo Mradi wa Kuwajengea Uwezo wanawake kugombea nafasi za Uongozi,
VIUNGO, Haki ya Afya ya Uzazi kwa wasichana na wanawake,Mradi wa kuwawezesha
wanawake wenye ulemavu (ISAVE KIJALUBA), Tumia jukwaa la habari kumaliza
Udhalilishaji, Uhuru wa habari, Shajihisha hatua za kitaifa kumaliza
Udhalilishaji, Mafunzo kwa waandishi wahabari kumaliza Udhalilishaji na Mafunzo
kwa waandishi wahabari vijana juu ya kuandika habari za wanawake na Uongozi.
TAMWA ni Jumuiya isiyo ya Serikali ilioanzishwa
mwaka 1987, yenye lengo la kujenga Tanzania yenye Amani inayoheshimu haki za
kibinadamu inayofanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na TAMWA ZNZ ilianza rasmi
2004 hapa Zanzibar kufanya kazi zake za kuisaidia jamii.
Comments
Post a Comment