HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
ZAKIA Rashid Baraka (36) wa Chanjamjawiri
wilaya ya Chake chake, anaetgemewa na watoto sita, sasa amejengewa makaazi ya
kudumu na aliyekuwa muume wake, baada ya kunufaika na ushauri wa kisheria, aliyopewa
na wasaidizi wa sheri wilaya ya Chake chake.
Mjane huyo, alisema baada ya kuachika na aliyekuwa
muume wake na kisha kumtaka ahame ndani ya nyumba waliokuwa wamejenga pamoja kijiji
cha Tundaua shehia ya Kilindi wilayani humo, alimua kufuatilia haki yake kwa
wasaidizi wa sheria.
Alisema, kisha mwanamme huyo alikutanishwa
nae, na kutakiwa kunijenga chumba kimoja, kwa vile alishakataa kumpa chumba
kimoja katika nyumba walipokuwa pamoja kindoa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, nyumbani
kwake Chanjamjawiri, alisema katika ujenzi wa nyumba hiyo anayoishi muume wake
kwa sasa alitumia nguvu kazi na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 1.
Alisema kuwa, alitegemea sana baada ya
kuchwa aidha engerejeshewa fedha ama kupewa haki yake ya chumba kimoja,
ingawa yote hayo hayakufanyika.
‘’Baada ya kufuatilia haki zangu kuanzia
kwa sheha na ofisi ya Mufti Mkuu Pemba, mote nilikwama, lakini nilipopewa ushauri
wa kisheria, nilifanikiwa na sasa naishi ndani ya chumba kimoja,’’alieleza.
Zakia alifafanua kuwa, kwa vile mama yake
mazazi alishapiga fondesheni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya familia, ilikuwa
rahisi kusimamisha matofali na kuezeka chumba chake kimoja, alichokubaliana na
aliyekuwa muume wake.
‘’Ijapokuwa nilizaa nae mtoto mmoja, kati
ya sita nilionao, lakini nilihitaji nipate haki yangu, na kwa sasa ameshanikabidhi
chumba kimoja kikiwa kimeezekwa,’’alifafanua.
Hata hivyo amewashukuru wasaidizi hao wa
sheria, kwa umakini wao wa kufuatilia lalamikoa lake, hadi kulipatia ufumbuzi,
ambao ulishindikana katika taasisi nyingine.
Wakati huo huo Zakia, amewataka wanawake
wenzake, wasikubali kuchangia wa nyumba au kununua kitu cha thamani pasi na
kuandikiana na waume zao.
Sheha wa shehia ya Kilindi Nassor Mohamed
Khamis, alisema anaifahamu vyema kesi ya mjane, ambayo anasema hata kamati ya
shehia, ilishindwa kumnasihi na kukubaliana na ushauri wa aliyekuwa muume wake.
‘’Baada ya kumuona Mohamed Mohamed (muume),
ni mzito wa kutuelewa, nilimataka Zakia (mjane), awasiliane na ofisi ya Mufti
Mkuu, ingawa alirudi tena, kwamba hajafanikiwa na kumuelekeza kwa wasaidizi wa
sheria,’’alieleza.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa
sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ ambae ndie aliyempa msaada wa
kisheria mjane huyo, Nassor Bilali Ali, alisema awali, muume huyo alitaka kuwa
mzito wa kufahamu, ingawa baadae alikiri na alihadi kumjengea.
‘’Huu unaweza ukawa mfano wa kwanza na mkubwa
ndani ya wilaya ya Chake chake, lakini walionufaika na msaada wa kisheria
katika maeneo mingine, wapo zaidi ya watu 7,000 kwa mwaka 2023,’’alifafanua.
Hata hivyo, alisema CHAPO inaendelea
kumuangalia mjane huyo kwa karibu, na inatarajia kumsaidia zaidi, kumuwekea
saruji chini na kumsaidia fikra ya kujenga banda ya vyumba viwili, kando ya
chumba hicho, ili kutanua makaazi yake.
Mratibu wa LSF zoni ya Pemba, Hamisa Bakar alisema,
LFS ikishirikiana na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, imekuwa
ikiwawezesha kimafunzo na mbinu, wasaidizi wa sheria, ili kukabiliana na
changamoto kama hizo.
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa
Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, alisisitiza kuwa kusema kuwa, ni vyema
wasaidizi wa sheria, wanapoibua changamoto, kuzifuatilia hadi upatikane ufumbuzi.
Sheria ya Msaada wa Kisheria Zanzibar nambari 13 ya mwaka 2018, ambayo imekuja kuanzisha Idara ya Katiba na Msaada wa
Kisheria, moja ya majukumu yake, ni kumtaka mtoa msaada wa kisheria, kutoa huduma ya msaada wa
kisheria, kwa mtu asiyekuwa na uwezo.
Mwisho
Comments
Post a Comment