NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WADAU wa haki za binaadamu kisiwani
Pemba, wamegundua kuwa Zanzibar inazosheria, kanuni na sera nzuri kwa ajili ya
watu wa wenye ulemavu, ingawa changamoto kubwa ni utekelezaji wake kwa vitendo.
Walisema, kwa mfano ipo sheria na sera, inayotaka kila jengo
la umma, liwe ni njia maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ingawa changamoto
ni kutotekelezwa na mamlaka wakati wa ujenzi.
Wakizungumza kwenye kikao kazi, kilichoandaliwa na
Mwemvuli wa asasi za kiraia Pemba ‘PACSO’ chenye lengo la kupitisha changamoto
za kisheria kwa wanawake, watu wenye ulemavu na vijana, kilichofanyika leo Disemba 16, 2023 skuli ya
maandalizi Madungu Chake chake.
Walisema, hata suala la ajira kwa kundi hilo, limewekwa
katika sheria kama ilivyo suala la haki nyingine za kibinaadamu, ingawa shida
ni utekelezaji wake.
Mmoja kati ya wadau hao, Khalfan Amour Mohamed kutoka
Jumuiya kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa akili ‘ZAPDD’ Pemba, alisema inashangaaza
kuona majengo ya umma, hayana njia za kutembea kwa watu wenye ulemavu.
‘’Hii bado ni changamoto, utakuta jengo la ghorofa la
serikali, chini imewekwa njia maaluma ‘rams’ kwa ajili ya watu wenye ulemavu,
lakini haikuzingatia ofisi zilizoko juu,’’alisema.
Nae Salim Abdalla Salim, alisema kwa mfano waliandikia
barua kadhaa wakati wa ujenzi wa soko jipya la Machomane Chake chake, ingawa
hakuna lililozingatiwa.
‘’Leo soko la Machomane limemalizika, kakini bado kwa mtu
mwenye ulemavu hasa wa viungo, hawezi kuyatembelea maduka yote yliomo humo, hii
sio sababu ya sheria, ni utekelezaji tu,’’alisema.
Kwa upande wake Mwache Juma Abdalla, alisema kama sheria zitatekelezwa kama zilivyo, kundi la watu wenye ulemavu wataneemeka na haki zao.
‘’Sheria zipo nzuri, ikiwemo kuwekwa kwa alama za
barabarani, adhabu kwa atakaemuigiza au kumkebehi mtu mwenye ulemavu na hata
masuala ya ajira, ingawa shida ni kwenye utekelezaji,’’alieleza.
Nae mshiriki Khadija Sultan, alieleza kuwa, wakati
umefika sasa kwa wadau wa haki za watu wenye ulemavu, kuungana pamoja, ili
kuhakikisha, vifungu vya sheria vilivyopitishwa vinatekelezwa.
Akifungua kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa ‘PACSO’
Nassor Suleiman, alisema wamekuwa wakizichambua changamoto za kisheria na
kisera, zinazowakwaza watu wenye ulemavu, vijana na wanawake.
‘’Lengo ni kuona makundi hayo ambayo ni sehemu ya jamii,
wanafaidi haki na fursa zao, kama ilivyo kwa makundi mbali mbali, yaliopo
katika jamii husika,’’alifafanua.
Mratibu wa miradi kutoka ‘PACSO’ Mohamed Najim Omar,
alisema katika kikao cha kwanza, makundi ya wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu, waliibua changamoto za kisheria, ambazo kupitia kikao kitaangaliwa kwa
kina.
‘’Kikao cha leo ‘jana’ kitachambua na kuona kwa kina,
ikiwa yale yliyoibuliwa hapo awali, ni kweli ni changamoto za kisheria, kisera ama
kikanuni,’’alifafanua.
Akielezea yaliojiri yatokanyo na kikao cha kwanza,
Mratibu huyo alisema ni pamoja na kifungu cha 116 cha Sheria ya Adhabu nambari
6 ya mwaka 2018, juu ya kupewa dhamana aliyemlawiti mtu mwenye ulemavu wa akili.
Jingine alisema ni kutotekelezwa kwa uwekwaji wa miundombinu
rafiki kwenye majengo ya umma, kwa ajili ya watu wenye ulemavu na hasa wa
viungo.
Aidha lieleza kuwa, kwa upande wa wanawake ni kutokuwepo
kwa sheria maalum, inayozungumzia masuala mbali mbali ya wanawake, ikiwemo
suala la uongozi katika taasisi.
‘’Lakini hata kundi la vijana, walitaka kanuni ya kuwa na
uzoefu, kama sharti la kuajiriwa hasa kwenye sekta za umma, liondolewe ili kuwe
haki, wanaotoka vyuoni moja kwa moja waajirike,’’alieleza.
Mwanasheria Ali Hamad, alisema, hakuna kifungu
kinachooelezea uzoefu kama sharti la kupata ajira, ama kukosa ajira na hasa
katika sekta za umma.
Aidha alifafanua, hakuna mgongano wa hukumu unaotolewa
tofauti ikiwa mtu atapatikana na hatia ya kumdhalilisha mtu mwenye ulemavu,
kwani makosa kadhaa ya jinai yanafasiriwa kwenye sheri ya Adhabu.
Akifunga kikao
hicho, Mwenyekiti wa PACSO Mohamed Ali Khamis, alisema kuwa, maoni ambayo
yatapatikana katika kikao hicho, watayaandika vyema na kuyasilisha kwa Jumuiya
ya wanawake wanawake wenye ulemavu Zanzibar, ambao nao watakeleza mradi kama
huo, ngazi ya kitaifa.
‘’Kwenye mradi huu PASCO, inatekeleza ngazi ya kanda (zone), ingawa wenzetu wa ‘JUWAUZA’ wanatekeleza ngazi ya kitaifa na kisha maoni hayo, watayafikisha kwa viongozi wa kitaifa,’’alieleza.
Mwisho
Comments
Post a Comment