NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na
Msaada wa Kisheria ambae pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala Bora Zanzibar, Zaina
Daud Khalid, amesema anatamani kuona sera ya Msaada wa kisheria ijayo, inaweka mazingira
rafiki zaidi, kwa wasaidizi wa sheria katika shughuli zao za kila siku.
Alieleza kuwa, kwa vile bado wasadizi wa sheria, wanaendelea
kuwa nguzo tegemeo kwa jamii na hasa watu maskini, lazima sera yao, iwe madhubuti
na imara, kama ile iliyopo sasa ya mwaka 2017.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Idara ya Katiba na Msaada
wa Kisheria, aliyasema hayo Oktoba 26, 2023 ukumbi wa Chuo cha Samail Gombani
Chake chake, wakati akifungua mkutano wa kukusanya maoni, juu ya rasimu ya sera
ya Msaada wa Kisheria.
Alieleza kuwa, sera iliyopo sasa, ambayo inaendelea
kukusanyiwa maoni kwa ajili ya kuandikwa nyingine, imetekelezwa vyema na karibu
asilimua 90 ya shughuli zake, zilifikiwa kama ilivyotarajiwa.
Katika hatua nyingine, aliwataka washiriki hao,
kutoa maoni yao kwa uwazi na ukweli, ili kamati inayokusanya maoni hayo, wapate
kuyaingiza kwenye rasimu hiyo.
Akiwasilisha muhutasari wa rasimu ya sera hiyo, Afisa
sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Ali Haji Hassan, alisema
kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, kwanza kulifanywa utafiti, uliogundua uhitaji
wa kuwa na sera mpya.
Alieleza kuwa, sera hiyo ambayo kwa sasa inatimiza wastani wa miaka saba, matamko yake mengi yameshatekelezwa, na yaliobakia ni machache mno.
Wakitoa maoni yao kwenye mkutano huo, wadau hao
walipendekeza kuwa, elimu zaidi isisitizwe na iwe kipaumbele kwa jamii.
Mwalikishi wa taasisi za wasaidizi wa sheria
Zanzibar, Nassor Bilali Ali, alisema lazima sera itamke suala la kupatiwa
mazingira wezeshi kwa wasaidizi wa sheria.
Nae mjumbe kutoka Umoja wa watu wenye Ulemavu ‘UWZ’
Nassor Suleiman, alisema kama sera inakuja na mfuko kwa ajili ya wasaidizi wa
sheria, ienezwe kwenye maeneo kama bandarini na uwanja wa ndege, ili wageni na
wengine wachangie.
Kwa upande wake mwakilishi wa ofisi ya Mwanasheria
mkuu wa serikali Zanzibar Jecha Vuai Jecha, anasema ili tathimini ya kweli ya kuwa
mwaka 2026, wazanzibar 30, kila 100 wawe wameshapata elimu ya msaada wa
kisheria, mkazo uwekwe.
Mwisho
Comments
Post a Comment