HABIBA
ZARALI, PEMBA@@@@
KATIBA
ya Zanzibar ya 1984 kifungu 11 (1) imeeleza kuwa binadamu wote ni huru, na wote
ni sawa na kila mtu anastahiki heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Ikafafanuliwa tena kifungu cha 12 (1) kuwa watu
wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo
haki bila ya ubaguzi wowote , kulindwa na kupata haki sawa mbele
ya sheria.
Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ibara ya 12 (1)
nayo imeelezea kuwa binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa, na kila mtu
anastahiki heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Tena kwenye Ibara ya 13 (4) ikaweka marufuku kwa
mtu yoyote kutobaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake
chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji
wa kazi au shughuli yoyote ya nchi.
Kimataifa upo Mkataba wa haki za watu wenye
ulemavu katika ibara ya 5, imeeleza
kutokuwepo ubaguzi, na kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria.
Mkataba
huo pia unapinga aina zote za ubaguzi zilizojengeka katika misingi ya ulemavu, ambapo
katika masuala yanayohusu watoto wenye ulemavu maslahi yao yatazingatiwa na
yatapewa kipaumbele.
Wakati huohuo, kwenye sheria ya watu wenye ulemavu ya Zanzibar nambari 8
ya mwaka 2022, kifungu cha 30 kinasisitiza wajibu wa kila mtu kulinda, kutetea
haki za watu wenye ulemavu, ikiwemo pale wanapovunjiwa haki zao za msingi.
Nacho kifungu
cha 31 kikaelezea zaidi huku kikifafanua kuwa, watu wenye ulemavu
hawatobaguliwa au kudhalilishwa kwa namna yote kwa sababu tu ya ulemavu wao.
KASORO ZA SHERIA
Kifungu cha
151 (1) cha sheria nambari 7 ya mwaka 2018 Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai Zanzibar, imeweka wazi makosa yasio na dhamana.
Kati ya
hayo limo kosa la ubakaji, kuingilia kinyume na maumbile, kuingilia maharimu,
kubakwa kwa kundi, kunajisi mtoto wa kiume, ingawa kasoro ipo kwenye kifungu
cha 116.
Uzuri wa Kifungu
hicho namba 116 ni kuwa, kimekataa dhamana kwa kosa la kunajisi mtu
mwenye ulemavu wa akili, hata kama mtuhumiwa huyo alikuwa anajua kuwa
aliyemnajisi ana ulemavu huo.
Je! Sheria
hizi, Katiba na mikataba ya kimataifa inazingatiwa kwa vitendo au hali
ikojo! hapa kisiwani kwetu Pemba?.
KESI ZA WATU WENYE ULEMAVU ZILIZOFUTWA
Mahakama ya
Mkoa Chake Chake, Juni 21, mwaka 2022 iliifuta kesi ya Abdalla Khatib,
aliyedaiwa kumbaka mtu mwenye ulemavu wa akili, baada ya kutofautiana ushahidi
wake alioutoa mlemavu huo wa akili.
‘’Ilinibidi
kuondoa kesi maana, muathirika (mwenye
ulamevu wa akili), ametofautiana na mashahidi wa upande wa mashataka, juu eneo
alilobakwa,’’alisema Hakimu Muumini.
Mama mwenye mtoto wake
alobakwa, mwanzoni mwa mwaka 2018, kesi hiyo ilichukua muda hadi mwaka 2020
kufutwa kwake sababu ikiwa ni mkanganyiko wa maneno.
“Nenda rudi kuanzia
kituo cha Polisi hadi mahakamani huku kukiwa na ushirikiano mdogo na kukosekana
kwa mkalimani ilibidi mwanangu akose haki yake hata kama kabakwa.” anasema.
“Kwa vile mtoto wangu
ana tabia ya kupoteza kumbukumbu siku
aliyotoa ushahidi wake, alisema alifanyiwa tendo hilo ndani ya nyumba, ingawa
Polisi alitaja kwenye kichaka na kuachiwa huru mtuhumiwa kwa sababu ya mkanyiko
wa maneno,’’anasimulia mama huyo.
Lakini hata dada wa
mtoto wa miaka 16 mwenye ulemavu wa matamshi, wa Wawi Chake chake, anasema
baada ya mdogo wake kutoa taarifa za kubakwa na kijana Shaaban Mohamed Issa
miaka 35, mtuhumiwa hakukamatwa na baada ya wiki tatu alikuwa anatembea mitaani.
WADAU WA KUPINGA UDHALILISHAJI
Ofisa
ustawi Wilaya ya Mkoani Aisha Abdi, anasema changamoto kubwa kwa wenye ulemavu
mbalimbali baada ya kudhalilishwa, ni kukosa taaluma ya kuyaripoti matendo
hayo.
Anasema
wakati mwengine huwa hawawezi kukumbuka walilosema mara ya kwanza ambapo napo
ni sababu ya kukosa haki zao.
Hakimu wa
mahakama maalum ya kupambana na udhalilishaji mkoa wa kaskazini Pemba, Muumini Ali Juma, anasema changamoto inayojitokeza hadi
kesi za watoto wenye ulemavu, kutofikia pazuri ni changamoto ya ushahidi.
“Wanapohojiwa
kituo cha Polisi huwa na ndugu ama jamaa zao huwasaidia kukamilisha maelezo ya
mwanzo, lakini kisheria hawaruhusiwi kufika tena mahakamani,’’anafafanua.
Anabainisha,
kuwa sheria haimtambui mkalimani wa awali aliyesaidia kutoa maelezo kituo cha
Polisi, na kisha kufika mahakamani, ikihofiwa kuegemea upande mmoja.
Haji Shoka
Khamis mwana mtandao wa kupinga udhalilishaji wilaya ya Mkoani anasema,
miongoni mwa sababu ya watu waliobakwa
kutovifikia vyombo vya sheria, ni kuwepo kwa rushwa kwa baadhi ya vyombo vya sheria.
Anasema
katika kuzifikia suluhu kesi za udhalilishaji hasa za watu wenye ulemavu ni
lazima kuwe na utayari kwa jamii na wazazi wenyewe.
Mwanaharakati
wa msaada wa kisheria na haki za binadamu Siti Habib anasema wanatowa elimu kwa
jamii pamoja na kupitia vifungu vya sheria ambavyo havijazingatia usawa wa haki
za watu wenye ulemavu.
Mohamed Ali
Abdalla afisa mtakwimu Wilaya ya Mkoani anasema,dana dana ya kwenda na kurudi ya kila siku kwenye
vyombo husika ikiwemo polisi ni kikwazo kinachoviza kesi za udhalilishaji.
Mratibu wa
Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) ofisi ya
Pemba Fat-hya Mussa Said, anasema ndio maana TAMWA Zanzibar inaendelea kuziibua
kasoro za sheria hizo, ili ziangaliwe upya.
‘’Sisi baada
ya kugunduwa kasoro ya sheria basi hushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo waandishi
wa habari ikiwemo kuwapa mafunzo mbalimbali ili waweze kuzitangaza na kushajihisha kufanyiwa marekebisho ”anasema.
Tatu Abdalla Msellem kutoka jumuiya ya Tumaini jipya Pemba, anasema
watoto wengi wanaofanyiwa udhalilishaji wakiwemo wenye ulemavu ni wale ambao wazazi wao tayari
wameshatengana.
Anasema watoto wenye ulemavu wanahitaji malezi madhubuti ya kuhakikisha
wanalindwa ingawa kwa wazazi waliotengana
ni vigumu kufanikiwa.
“Wako baadhi ya wanaume wanapoona mwanamke kazaa mtoto mwenye ulemavu
basi humwacha ama kumtelekeza hilo hukosesha
mtoto haki yake ikiwemo ya elimu,ambayo humsaidia anapofikwa na changamoto za
udhalilishaji.
VIONGOZI WA WATU WENYE
ULEMAVU
Afisa wa watu wenye ulemavu Wilaya ya Chake Chake
chake Mwadini Juma Ali anasema mtu mwenye ulemavu wa akili ama wasioona apewe nafasi maalum.
Anasema sheria inaeleza kuwa watu wote ni sawa
ingawa inawapa ugumu maradufu watu wenye ulemavu, na kuhimiza watu kutowa
ushahidi kwani wasipofanya hivyo hupelekea kesi kufutwa na kuwakoseshwa haki
zao.
“Kuna kesi nyingi hufutwa kutokana na watu wenye
ulemavu kutokana na mkanganyiko wa ushahidi kwani wengine hukosa kumbukumbu na
kupelekea maelezo kutofautiana hivyo ni vyema jamii kutowa ushahidi wa kesi
hizo ,”anasema.
Akitoa mfano wa kesi ambazo ilikuwa na tatizo la
ushahidi ni ile ya Mtuhaliwa, dereva wa daladala Wesha ambayo baba mzazi alikataa kutowa ushahidi
anasema ingawa zipo nyingi kama hizo.
Mratibu Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu
Pemba Mashavu Juma Mabruk anasema kinachorejesha nyuma ni rushwa muhali na rushwa
fedha.
“Mara nyingi wanaochangia kuharibu ushahidi ni
wahanga au familia zao ambao hupewa mbinu za kuharibu ushahidi na watuhumiwa wa
kesi hizo na kupelekea kufutwa kwa kesi”, anasema.
Naibu katibu wa jumuiya ya watu wenye Ualbino Pemba
Mudathir Sharif Khamis anasema elimu ni kitu pekee kitakachowawezesha watu
wenye ulemavu.
Anasema kama watu wenye ulemavu watasomeshwa wataweza
kukabiliana na changamoto kadhaa zinazowakabili katika maisha yao ikiwemo
kujuwa kueleza kwa kusoma na kuandika wanapofikwa na vitendo vya udhalilishaji.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wasioona Zanzibar 'ZANAB' wilaya
ya Mkoani Ali Hemed Khalifa aliitaka jamii kuwasimamia watu wenye ulemavu
badala ya kuwakandamiza kwani nao wana haki sawa kama wengine.
Anasema hata vyombo vya sheria navyo vitende haki na viangalie watu wenye ulemavu kwa jinsi ya
hali zao na kwasaidia kupata haki zao kwa mujibu wa sheria pale wanapodhalilishwa.
WAZAZI WA
WATOTO WENYE ULEMAVU
Mzazi Asha Ahmed wa Mtambile anasema serikali iwawekee
adhabu kali wanaowadhalilisha watu wenye ulemavu kwani wanapoachiwa ndio huzidi
kufanya matendo hayo.
“Bado sheria inawapa nafasi ya kujipenyeza penyeza
wanaowadhalilisha watu wenye ulemavu lakini ni wakati sasa wa kufanyiwa
marekebisho sehemu hizo”,anasema.
Kassim Ali wa Mkoani wanasema hawezi kuwa sawa mtu mwenye
ulemavu wa akili ama wasiosema na mtu asiye na ulemavu hasa katika kutowa
ushahidi.
“Asiye na ulemavu hata aitwe mara kumi atatowa ushahidi
lakini mwenye ulemavu kama wa akili ni ngumu hivyo achukuliwe pale aliposema awali”,anasema.
ATHARI YAKE
Mzazi wa mtoto mwenye
ulemavu anasema ni vyema sheria ingewatazama watu wenye ulemavu ili wakaweza
kuchukuliwa ushahidi wa awali kwani wengine hawana kumbukumbu za muda mrefu na
hatimae hukosa haki zao.
Hakimu wa
mahakama maalum ya kupambana na udhalilishaji
wilaya ya Wete Muumini Ali Juma
anasema wanafanya hatuwa mbalimbali ikiwemo kupeleka mapendekezo kwa uongozi
husika ya kuhakikisha yanafanyika mabadiliko
ya sheria na kuweka mazingira rafiki ili watu wenye ulemavu hasa wa akili
waweze kupata haki sawa pale wanapofanyiwa dhalilishaji.
NINI KIFANYIKE
Wazazi na walezi wasiwe rahisi kuharibu kesi za watoto
wenye ulemavu na badala yake wasimamie hadi kupata haki zao.
Sheria iruhusu na
kuwekwe wakalimani wa kutosha ambao watasimamia kesi za watu wenye ulemavu
sambamba na kuwepo sheria ambayo itakuwa
na usawa kwa watu wote.
Ingetungwa
sheria moja tu ambayo itajumuisha makosa yote ya udhalilishaji, badala ya sasa
kuwepo kwenye sheria mbali mbali.
Polisi na Mahakama zisimamie kesi bila kujali huyu ni
nani kuanzia uendeshaji mrefu wa kesi, ukusanyaji na uchunguzi.
Kila kesi iamuliwe na mazingira husika iangalie kufanyika
kwa kosa na kuachana na tofauti zinazojitokeza kwenye ushahidi.
Huwenda watunga sheria hawakuwaki kufikiria katika
utelekezaji wa majukumu yao itakuja
kutokea kukutana na kesi ngumu za
udhalilishaji ambazo hufanyiwa watu wenye ulemavu.
Hata hivyo kwa dunia ya sasa ambayo inachangamoto ya
mmongonyoko wa maadili kila jambo baya ambalo huwezi hata kulifikiria basi
hutokea.
Kinachohitajika ni kwenda na wakati kulingana na uhitaji
kwa sasa suala la kubadilisha sheria ili kupambana na majanga ya
udhalilishaji na changamoto nyenginezo
linapaswa kuzingatiwa kwa umakini na kimkakati mahususi.
mwisho
Comments
Post a Comment