NA HAJI NASSSOR, PEMBA@@@@
SHERIA ya watu wenye Ulemavu Zanzibar
nambari 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 28 (e) kimeweka wazi, haki ya watu wenye
ulemavu, kujumuishwa kwenye harakati za uchumi.
Ikaelezwa kuwa, mtu mwenye ulemavu ana haki ya kujitegemea na kujumuishwa
katika shughuli za kijamii, kiuchumi na siasa.
Kifungu chingine ni kile cha 30, kinachotoa wajibu wa kila mmoja, kulinda
na kutetea haki za watu wenye ulemavu, zikiwemo cha kiuchumi.
Hata kifungu cha 31, kimepiga marufuku, mtu yeyote kumbagua mtu mwenye
ulemavu, kwa namna yoyote ile, tena kwa sababu ya ulemavu wake.
Kwenye kifungu cha 42 cha sheria hiyo, kimekataa kumficha mtu mwenye
ulemavu, kwa lengo la kumzuia asishiriki katika moja ya haki zake, zikiwemo za
kiuchumi.
Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, Ibara ya 27, ikasisitiza
nchi zilizoridhia mkataba huo, lazima ziweke mazingira sawa na wasiokuwa na
ulemavu, katika ajira na kujiajiri.
Haya yalikuja kulindwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kuanzia kifungu
cha 12 (2), kikisisitiza hakutakuwa na sheria itakayokuwa na kifungu,
kinachoonesha ubaguzi.
Tena hata kifungu cha 22 (1) (a) kimeainisha kuwa, ni wajibu wa kila
mmoja, kujituma katika kazi za halali na zile za uzalishaji mali, ambapo hapa
watu wenye ulemavu wakiwemo.
Na ndio maana, Jumuia ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania
TAMWA-Zanzibar, kwa kuyaona hayo, ikaja na mradi jumuisha wa kijaluba iSAVE ZANZIBAR.
NINI KIJALUBA iSAVE ZAZNIBAR?
Ni mradi jumuishi, unaolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi na
kijiamini.
Kupitia
mradi huu, watu hao wenye ulemavu kwa sasa wameshajengewa uwezo, kuhusu maisha
yao wenyewe, na jamii zao.
Maana, lengo
kuu hasa la mradi huu wa Kijaluba iSAVE Zanzibar, unaangazia zaidi, kukuza
uwezo wa watu hao, kwa kujenga mitazamo chanya, juu ya ushiriki wao, na
kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato.
Mratibu wa
mradi huo kutoka TAMWA -Zanzibar ofisi ya Pemba, Mohamed Salim Khamis, anasema
kipato hicho, hasa kwa aina ya maradi huo ulivyo, ni kupitia katika vikundi vyao
vya kuweka na kukopa ‘saccos’.
Mbiznu za
utekelezaji wa mradi huo, anasema moja wapo ni kuwawezesha watu hao, kupata
kipato, jambo ambalo tayari kwa sasa limeshafanyika.
‘’Jingine ni
kuwezeshwa, ili wawe na ushiriki kamili, katika miradi na maendeleo ya jamii,
kutokana na mazingira yao,’’anasema.
Mbinu
nyingine aliyoitaja, ni kuangalia vikwazo vinavyowakatisha tamaa watu hao hasa
katika jamii zao.
‘’Kwa mfano,
kama jamii wanamitazamo kuwa, watu wenye ulemavu hawawezi, tutoa elimu, au kama
tutagundua wanatengwa, tutaelezea haki zao kwa jamii,’’ anaeleza.
Kwa sasa
tayari watu hao wenye ulemavu kupitia mradi huo, wameshaanzishiwa vikundi vya
kuweka na kukopa (iSAVE groups).
Baada ya kupewa
mbinu za kisasa kwenye vikundi vyao vya kuweka na kukopa, kisha wataunganishwa
na tasisi za kifedha kama benki, ili waweza kuomba mikopo.
Walishasema
wahenga kuwa, mgagaa na upwa.. wala hali ugali mkavu, hapa msemo huu utasadifu,
kwa kundi la watu wenye ulemavu, maana wanagaa gaa kwenye ufukwe wa Kijaluba.
Na hili linaingia
akilia, maana walengwa wakuu wa mradi huu, ni watu wenye ulemavu wakiwemo
watoto, wanawake, wanaume, kwamba kila 60 kwenye 100 wahusika watakuwa wao.
Akimaanisha
kuwa, kwa mfano kila watu 10 wataokanufaika na mradi, basi sita wawe watu wenye
ulemavu na wanne wale wasiokuwa na ulemavu.
‘’Kwa hiyo,
wanajamii wa wilaya ya Chake chake kwa Pemba na wilaya ya Kusini kwa Unguja,
ndio ambao watafikiwa na mradi huu, kwa njia ya majaribio,’’anafafanua.
WATEKELEZAJI MRADI
Mratibu wa
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba,
Fat-hya Mussa Said, anasema, mradi unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya
shirikisho la Jumuiya za watu wenye ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’ pamoja na
TAMWA-Zanzibar.
TAMWA kazi
yao kubwa, ni kuhakikisha kila kitakachofanywa ndani ya mradi, jamii inapata
taarifa kwa, kuwatumia waandishi wa habari.
‘’TAMWA
tunaguswa na haki za watu wenye ulemavu, na ndio maana tukawa washirika wa
utekelezaji wa mradi huu, ambao unafadhiliwa na Chama cha watu wenye ulemavu
cha Norway ‘NAD’, anafafanua.
Anaona kama
jamii ya wilaya ya Chake chake itajali kwa kiasi kikubwa haki za watu wenye ulemavu,
mradi huo utatekelezwa kwa mafanikio.
USHIRIKA ‘MWANZO
MGUMU’
Ushirika huu
wa ‘Mwanzo mgumu’ wenye wanachama 30 jumuishi ambao umaenzishwa Mei 28, mwaka
huu lengo likiwa lilelile la kuwakomboa watu wenye ulemavu.
Hapa Mwenyekiti
wa ushirika huo, wa kuweka na kukopa, Mayasa Hamad Salim, anasema ushirika huo
pamoja na uchanga wake, umeshapiga hatua.
‘’Kwa sasa,
pamoja na kuwa kuanza kutoa mikopo kati ya shilingi 100,000 hadi shilingi 400,000
kwa wanachama jumuishi, lakini tayari biashara zimeanza kufanyika,’’anasema.
Anafafanua
kuwa, watu wenye ulemavu hawakufikiria kuwa kupitia ushirika wao huo, wengeweza
kuwa na uhakika wa kipato, kupitia njia ya kukopeshana.
Katibu wa ushirika
wa mwanzao mgumu Khamis Said Massoud, anasema sasa wameanza kukopeshana bidhaa
ya sabuni na wameshafanya hivyo mara tano mfululizo.
‘’Unajua kabla
ya kujiunga na mpango huu, unaosimamiwa na mradi wa kijaluba, ilikuwa hata sabuni
ya kufulia kwa sisi watu wenye ulemavu, haikuwa ya uhakika, lakini sasa ni
kawaida mno,’’anaeleza.
Anasema hata
wameshatoa mikopo mitatu, yenye thamani ya shilingi 650,000, maana mwanachama mmoja
amekopa shilingi 400,000, mwengine shilingi 200,000 na mmoja shilingi 50,000.
Mwanachama
wa ushirika huo Fatma Najim Omara, anasema tayari ameshakopa shilingi 200,000
na kununua bidhaa za njugu nyasa, kwa ajili ya kuendelezea biashara yake.
‘’Naamini, kama
sio kuwepo wa ushirika huu, leo hii ningehitaji kiasi hicho cha fedha, ningemaliza
kijiji chote bila ya kufanikiwa,’’anaeleza.
Malengo yake
ya baadae, kwanza ni kukuza biashara yake ya genge yenye viungo vya mchuzi, ili
kuhakikisha kuwa na duka kubwa la chakula.
Sahera Mbarouk
Suleiman, anasema uwepo wa ushirika huo jumuishi wa kuweka na kukopa, sasa maisha
yake ana hakika wa kipato.
Kwa sasa nna
hisa 70, zenye thamani ya shilingi 35,000 fedha hizo sio kidogo, maana zinaniwezesha
kukopa hadi shilingi 400,000.
‘’Mimi naona
mradi wa Kijaluba iSAVE, umechelewa kunifikia, laiti wengekuwepo tokea zamani, ningeshakuwa
na uwezo wa kuajiri wengine,’’anaeleza.
Anasema wanaosema
watu wenye ulemavu hawawezi kufikia ndoto zao, huyo anaota ndoto za mchana, na
akitaka ushahidi wa hilo, wanamkaribisha kijiji cha Furaha Mbuyuni shehia ya
Mvumoni.
Kwake biashara
yake ya kuuza nguzo za mtumba, anaiona kuelekea kupata mafanikio, kwani licha ya
muda mfupi tokea kujiunga na ushirika huo, sasa ameanza kunawirika.
‘’Kwa sasa
hata muume wangu akiondoka miezi miwili hadi minne, sina wasiwasi wa huduma za
lazima, maana najua kwanza wapi nikakope,’’anaeleza.
Kabla ya
kuingia kwenye ushirika huo, anasema hakuwa na uhakika hata wa shilingi 100 kwa
siku kuipata, ingawa kwa sasa anaishi kwa amani.
‘’Mimi ni
mgonjwa wa sukari na presha, sasa wakati mwengine nilikuwa nahitaji walau shilingi
50,000 kwa ajili ya safari, na kwa wakati huo haikuwa rahisi kupata,’’anaeleza.
Anakumbuka vyema
kuwa, hata fedha za michango, ada ya masomo kwa wakati huo, kwake ilikuwa ni
mzito kuipata kwa uhakika, licha ya kuwa anae msaidizi katika hilo.
‘’Hata
michango kama ya harusi, matibabu, ufiwa, nguo za sikukuu kwa ajili ya watoto,
ilikuwa kazi kubwa, ikilinganishwa na sasa,’’anaeleza.
Mshika fedha
wa ushirikia huo Amina Said Ali, anasema wanachama hao 30, kwa sasa
wamekubaliana kuanzisha biashara ya sabuni.
‘’Kwa hatua
za awali, tulijikopa shilingi 34,000 na kununua sabuni paketi 30 na kila mmoja
alinunua na kijiingizia faida wastani wa shilingi 13,000, lakini mara ya pili,
ya tatu na ya nne faida ilingezeka shilingi 100, ingawa kwa msimu wa tano tumepasta
shilingi 15,000,’’anaeleza.
Anasema pamoja
na uwepo wa mradhi huo wenye sura ya biashara, ushirika pia umeanzisha kilimo
cha mboga za mriba, bamia, bilingani ili kuongeza pato.
‘’Kwa hakika
ujio wa mradi huu, sisi watu wenye ulemavu na wengine, tunaowawakilisha watoto
wenye ulemavu, tunaona TAMWA na wafadhili wao, hawakukosea,’’anaeleza.
Mzazi Juma
Maasoud Said anaemwakilisha mtoto wake mwenye ulemavu, anasema sasa watu wa
kundi hilo, wamekuja kukombolewa kwa vitendo.
‘’Nilikuwa
nishamkatia tamaa mtoto wangu wenye ulemavu mchanganyiko, juu ya hatma ya Maisha
yake, lakini leo sasa nna hakika kupitia mpango huu, maisha yake yameanza kuimarika,’’anasema.
Kwa sasa ana
hakika ya kupata sabuni na huduma nyingine kama mboga mboga, wakati wote,
kufuatia mpango ulioandaliwa ndani ya ushirika wao.
Kupitia ushirika
huo anasema sasa ameshajua njia za kujikwamua na umaskini wa kipato, ikiwemo
kufuga, kupanda mboga kwa ajili ya biashara na Kuanzisha biashara ndogo ndogo.
‘’Unajua
elimu waliotupa wenzetu TAMWA, kupitia mradi huu wa iSAVE Zanzibar sasa,
haikuniongoza kwenye ushirika pekee, lakini hata, nikiwa peke yangu sasa
najiamini,’’anaeleza.
HATUA ILIYOFIKIWA
Tayari
waalimu wasimamizi wa vikundi vya kuweka na kukopa wameshapewa mbinu za kwenda
kuihamasisha jamii, na hasa kundi la watu wenye ulemavu, kuanzisha vikundi vya
kuweka na kukopa.
Mwalimu wa
mafunzo hayo Bakar Haji Bakar kutoka TAMWA-Pemba, aliwaeleza wasimamizi hao
ngazi ya shehia, wahakikishe, hata kwenye uongozi wa vikundi kipaumbele ni watu
wenye ulemavu, jambo ambalo kwa sasa lipo.
‘’Kwa mfano
wale viongozi sita wa mwanzo, katika kila kikundi, watu wanne, wawe ni watu wenye
ulemavu, maana pia mradl huu unalenga kutoa fursa za uongozi kwao,’’anasema.
Kumbe mradi
huu utakapotia nanga Disemba 2024, kutoka pale ulipoanza Novemba 2022, watu
wenye ulemavu kwa wilaya ya Chake chake, wewe wameshaiva kiuongozi.
Kupitia
mradi huu wa majaribio, utaona kuna wananchi 1876, wakiwemo wanawake 1,122 na
wanaume 750, kutoka wilaya za Chake chake Pemba na Kuisni Unguja, ndio
wanaonufaika.
Chakuzingatia
tu ni kuwa, kila watu 60, kati ya 100, watakuwa ni wenye ulemavu mchanganyiko,
tena waliomo kwenye shehia za wilaya ya Chake chake kwa Pemba na au wilaya ya Kusini
Unguja.
Watu hao,
watawezeshwa kupitia vikundi maalum vitakavyoanzishwa katika kila shehia ya
wilayani humo, ambapo kila kikundi, kitakuwa na wastani wa wanachama kati ya 25
na wasiozidi 30.
Afisa Utawala
kutoka Shirikisho la jumuiya za watu wenye ulemavu Zanzibar ‘SHIJUWAZA’ kisiwani Pemba Aisha
Abdalla Juma, yeye amefurahishwa, na ujio wa mradi huo.
Upande
mwengine Mwezeshaji wa vikundi vya watu wenye ulemavu ‘CRP’ Fatma Abrahman Ali wa
shehia ya Ole wilaya ya Chake chake, anaesimamia vikundi tisa, vyenye wanachama
wastani wa 25 hadi 30 kwa kila kimoja.
Aidha mradi
huo ulioanza mwaka 2022, ukitarajiwa kumalizika mwaka 2024, utakwenda kushughulikia
vikwazo vinavyowarudisha nyuma, watu wenye ulemavu.
Kwa sasa
mradi huu, anatekeleza wilaya ya Kusini Unguja na Chake chake kwa Pemba, kama
eneo la majaribio, ambapo walengwa wakuu ni watu wenye ulemavu wakiwemo vijana,
watoto kwa asilimia 60 na 40 na watu wengine.
Mwisho
Comments
Post a Comment