Na Nusra Shaaban, ZANZIBAR
Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) imefanya mkutano na taasisi za serikali, asasi za kiraia,viongozi wa kidini pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, kujadili changamoto za kisheria na kijamii ambazo zinakwamisha ushiriki wa wanawake kwenye masualaya uongozi na demokrasia.
Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Dkt Shein ZURA,Maisara Mjini Zanzibar, umewapa fursa viongozi mbalimbali kushiriki kujadili changamoto wanazopitia wanawake katika kugombania nyadhifa za uongozi, changamoto hizo ni pamoja na vile fikrapotofu,rushwa,ujuzi mdogo wa stadi za uongozi,elimu ndogo,majukumu mengi ya nyumbani,kipato duni na nyenginezo.
Akizungumza na washiriki katika mkutano huo, Mratibu wa mradi wa kuwaimarisha wanawake na uongozi kutoka ZAFELA Khamis Ali Rashid amesema mkutano huo una lengo la kujadili kwa pamoja changamoto hizo pamoja na kuandaa mpango wa utatuzi wa changamoto hizo kwa kila mmoja ulingana na nafasi yake aliyonayo katika utumishi wa umma.
Viongozi kutoka taasisi mbalimbali walioshiriki katika mkutano huo waliwasilisha maoni yao katika kuondosha changamoto hizo, wengi wao wakihimiza suala la uwajibikaji kazini na kutoa mrejesho wa ila hatua inayochukuliwa.
“Mbali na hayo ili aendelee kupatikana mwanamke imara anaejiamini na anaeweza kujenga uthubutu wa kugombania nafasi za uongozi basi lazima hatua hiyo iandaliwe tangu mwanamke yupo mdogo.”Suhaila Abdullah Afisa Vijana kutoka wizara ya habari idara ya maendeleo ya vijana alieleza.
Hemed Saleh Ali, Kadhi wa wilaya kituo cha Mwanakwerekwe Zanzibar anasema “Uislamu haujamkataza mwanamke kuwa kiongozi,inawezekana kuna ufahamu mdogo katika jamii kuhusu suala la uongozi katika uislamu ndio maana hali hiyo inawarudisha nyuma wanawake na uongozi.
“Ni lazima kuwe na mkakati kwa wanawake kupendana wao wenyewe kwa wenyewe ili hata sisi wanaume tunapokuja kuweka uadui wetu basi tushindwe kutokana na nguvu ya umoja wao". Alisisitiza Said Suleiman Ali mjumbe kutoka KOK Founadation.
Naibu Mkurugenzi kutoka ADC Mtumwa Faiz Sadik amesema “ili kupiga hatua wanawake na maendeleo ya uongozi ukiachilia mbali changamoto wanazopitia lazima kuwepo na utekelezaji wa mipango na maazimio ya vikao mbalilimbali vinavyoandaliwa kuhusu wanawake na uongozi”
Kadhalika kwa mujibu wa Bi Halima Ibrahim Mohd kutoka Chama cha ACT,anasema wanawake hivi sasa wamejitahidi kuchukua jitihada kubwa ya kushikana mikono, hatutaki kusikia kama wanawake hatupendani, kwa kuthibitisha hilo uchaguzi ujao tunakampeni ya kumnyanyua mwanamke, awemo katika ngazi za maamuzi,kamati kuu na halmashauri juu.
Aidha,hayo yanajiri ikiwa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar ZAFELA kwa kushirikiana na TAMWA –Zanzibar na PEGAO kwa upande wa Pemba inaendelea kutekeleza mradi wa Wanawake na
Uongozi unaofahamaika kwa jina la “STRENTHEN WOMEN IN LEADERSHIP”(SWIL),unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
Mwisho.
Comments
Post a Comment