NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘’NILIVUNJIKA
mkono, baada ya kuparamia nyumba kumkimbia muume mtarajiwa alipokuja kwetu, ili
tusionane,’’anasema Saada Khsmi Kombo (65) wa Micheweni.
Hadi leo mkoni wake mmoja wa kushoto, eneo vilipootea
vidole hapako sawa,baada ya ajali hiyo.
Kwa utamduni ulivyokuwa enza hizo, ilikuwa mwanaume hata
kwa ambae alishabisha hodi na kuweka nia ya kufunga ndoa, haikuwa rahisi,
kukutana na mtarajiwa wake.
Ndio maana Saada anasema, alilazimika kwenda mbio nyingi,
kwani hakuwa na hamu ya kukutana na mume wake mtarajiwa, hasa kutokana na
malezi yalivyokuwa.
KWANINI
ILIKUWA HAWAONANI?
Rehema Faki Sheha (60), baada ya muume kuweka nia na
posa kufuata, hapo mwanamke hukosa hamu hata ya kula, na hakukua na jambo la
ushawishi la kukutana nae.
Anasema huo ndio utamaduni wa Micheweni, na wao wakiurithi
tokea enzi na karne, ingawa hayo anasema ilitokana na mafundisho ya wazazi wao.
Walikuwa wakielezwa, kuwa mara baada ya mtoto wa kike
kufikia utuuzima (kuvunja ungo), na kama akikutana na mwanamme na kufanya nae
tendo la ndoa, atawapotezea heshima wazazi wake.
‘’Sio tu kwamba ilikuwa tunafunzwa madhara ya kupata
mimba, au kuondoa uke, kujishusha thamani, lakini ilikuwa tukielezwa kuwa ni
kuuvua nguo ukoo,’’anasema Saada Said Kombo (60).
Aisha Simba Mkasha (55) anasema, suala la kukutana na
mwanamme hata kwa mazungunzo, kwao ilikuwa ni marufuku, labda iwe eneo la
kutafuta elimu.
Haya anasema yalipelekea, kuanzia saa 12:00 jioni
ilikuwa ni marufuku kwa mtoto wa kike wa Micheweni, kutembea nyakati hizo bila
ya sababu za msingi.
‘’Mimi mara moja mama alinituma nyumba ya tatu,
kumpelekea mtoto dawa, basi nilipokutana na mjomba, alinichapa bakora tatu na
mama nae aligombwa na kuwekewa kikao,’’anasilimulia.
Anasema mjomba, yengewezekana kwenda katika eneo
jingine, je mama yake engejuaje, akimaanisha ililazimika kufuatanishwa na mtu
mwengine.
Hayo yote anasema, yalipelekea hata baada ya mwanamme
kuweka nia ya kufunga ndoa, isiwe rahisi mtoto wa kike kukutana nae kwa mazungumzo.
Mwanaimani Khamis Juma, (45) anasema hata kwa umri wake,
posa za Micheweni, anaziona zikoa tofauti na maeneo mengine, kaunzia siku ya
kwanza hadi ndoa.
KWA
UPANDE WA BWANA HARUSI MTARAJIWA
Faki Khamis Kai (59) anasema, hakuwa na uhuru wa
kukutana na mke wake mtarajiwa, na hasa baada ya kamati ya maamuzi ya wazazi,
kumkubali rasmi.
Muume mtarajiwa, baada ya kuchunguuzwa kwa mwezi mmoja
na jawabu kupatikana kuwa amekubaliwa, alikuwa akitoa huduma kama za chakula na
kitoweo.
‘’Lakini anaepeleka huduma hizo kwa mtarajiwa sio muume,
bali ni baba yake, kaka, shangazi au mtu mwengine kutoka kwenye familia yake,’’anasema.
Hii ilihofiwa, mtarajiwa kuhamia ndani ya nyumba ya mchumba
wake na kupelekea mdhara ya kuingiliana kimwili, kabla ndoa kufungwa.
Hamad Mbwana Shaame, (55) anasema, wakati mwengine
wazazi wa mtoto wa kike, wanaweza kumualika mkweo wao mtarajiwa, kwa mfano
kujumuika pamoja kwenye chakula.
‘’Usishangae wakati muume mtarajiwa anaalikwa, mke wake
mtarajiwa ameshamishiwa kutoka kwao, kwenda kwa ndugu na jamaa zake
wengine,’’anasema.
Hapa anamaanisha kuwa, suala la mke mtarajiwa na muume
mtarajiwa, kamwe hawaonani mpaka siku ya harusi.
‘’Mimi ndoa yangu ilifungwa miezi minne baada ya posa,
na muume ilikuwa tunakaa jirani, lakini nilimuona sura yake hasa, baada ya
sikua saba ndoa kufungwa,’’anasimulia Mtumwa Khatib Omar.
Chakushangaaza utamaduni wa Micheweni ikiwa, suala la
kuekesha mke, tokea akiwa na umri kati ya miaka saba hadi 10, na kuanza
harakari za kupelekea huduma, unakubalika.
‘’Kwetu jambo kama hili wala halisababisha mtoto wa kike
kukosa ufahamu wa masomo, wala kutembea tembea, maana ni urithi tokea wazazi
wetu,’’anasema Hidaya Kombo Kassim.
NDOA/HARUSI ZA MICHEWENI ZA ASILI
Mke mtarajiwa, kwa siku saba kabla ya siku ya harusi,
huhamishwa kutoka kwao kwenda kwa shangazi yake au mtu mwengine.
Akiwa huko hufunzwa namna ya kuishi maisha ya ndoa, ili
awe mvumilivu, mstahamilivu, mwenye Imani, kujenga mapenzi na wakwe zake.
Rehema Faki Sheha, anasema lengo ni kuhakikisha anakuwa
rafiki na mazingira yoyote atakayokutana nayo kwa muume wake, na hasa suala la
ugumu wa maisha.
‘’Mafunzo aliyokuwa akipewa mtoto wa kike hayahusiani na
uvulivu wa muume mwizi, mlevi, mpigaji bali hasa ni kupambana na maisha mapya
ya ndoa na kumbadilisha muume kitabia,’’anasema.
Halima Haji Hamad anasema mafunzo hayo, pia yalikuwa
yakiwasisitiza wanawake hao, namna ya kutimiza wajibu kwa muume, ikiwa ni
pamoja na kumuhimiza usafi.
Khamis Othman Kombo, anasema mafunzo yalikuwa yakisaidia
mno kuhakikisha ndao zinadumu, na kujiepusha na migogoro.
‘’Kwa mfano mke niliyenaye sasa huu ni miaka 46, lakini
tunapokosana kabla mimi sijajua, alikuwa ananiaga kwenda kwao, kumbe anakimbia
changamoto iliyojotokeza na akirudi maisha yanaanza upya,’’anasema.
Kuhusu sherehe ya ngoma, wanasema ilikuwa ni ngoma aina
ya msondo pekee, na kwa asilimia kubwa, ukiwahusisha wanawake na watoto.
Ngoma hii ilikuwa ikipigwa siku moja kabla ya harusi na
siku husika, na kutoka hapo siku ya tatu familia hujiandaa kumpelekea mtoto wao
vyombo.
‘’Tukifika kule, sisi hufua nguo za harusi na kumpikia
maana, siku ile huwa yule aliyempeleka ‘kungwi’ hutakiwa kupumzika, baada
kufanyakazi nyingine,’’anasema Mwajuma Hamad Khamis.
POSA
NA NDOA ZA LEO ZA MICHEWENI
Fatma Hamad Ali, anasema huo umeanza kupotea kwa kasi,
hasa baada ya uwepo wa utandawazi ulioambatana na demokrasia uhuru wa
kujieleza.
‘’Sasa kila mmoja awe mtoto wa kike au kiume anamtafuta
mtarajiwa wake na kumpeleka mbele ya wazazi, na shida zaidi kama
atakataliwa,’’anasema.
Alishashuhida ndoa tatu katika maisha yake, kuvunjika
siku moja kabla, baada ya wazazi kumpokea muume kinyume na matakwa ya mtoto wao.
Issa Juma Haroub (30) anasema, sasa watoto wa kike na
kiume wanakaa kwenye baraza na kupanga mipango ya harusi, aina ya nguo, vyombo
na hata mahari.
Zuwena Mkasha Khalfan (26), anaona kuna athari kubwa ya
kuacha utamaduni wa wazazi wa kumchagulia mke au muume mtoto wake.
‘’Wapo wanawake wenye umri kama wangu, wameshaolewa na
waume wanne, kwa kule kujichagulia wenyewe waume, na kisha wanayokumbana nayo
hawana pakwenda,’’anasema.
WAZEE
Hamada Shaame Khamis (73) kila muacha utamaduni anaweza
kuyumba katika moja ya maeneo, aidha kwenye malezi ya watoto, uchungaji wa
ndoa, heshima kwa majirani.
Sharifu Massoud Hamad (60) anasema, sasa ndoa kudumau
kwa miaka 30 hadi 45 ni jambo la maajabu, na anaona hazipo.
‘’Mimi nimedumu ndani ya ndoa kwa miaka 35, kabla muume
wangu kufariki, na ilikuwa kila mmoja anamvumilia mwenzake, kwani yeye kapewa
mimi na mimi nimepewa yeye na wazazi wetu,’’anasema.
Anasema sio rahisi kurudi tena kwa ile ya Micheweni asili,
ambayo watoto walikuwa wanatii kwa wazazi wao, jambo lililoongeza baraka na
mapenzi ndani ya familia.
WANAHARAKATI
WANASEMAJE?
Wanasema, haki ya muume kuchagua mke amtakae, ndio hasa
inayokuza maelewano, ushirikiano, uaminifu miongoni mwa wanandoa.
Tatu Abdalla Msellem, wa Chake chake anasema, kama
utamaduni haukwazi upande mmoja, unafaa kuendelezwa na kukuzwa, kwani msingi wa
maisha ni kuishi kwa amani.
Asha Khamis Juma wa Mkoani, anasema kila eneo huwa na
utamaduni wake, ingawa la kuzingatia ni kuhakikisha hakuna udhalililishaji na
ukatili.
‘’Kwa mfano ikiwa eneo la Micheweni walikuwa na posa hadi
ndoa zinazofuata utamaduni na ndoa zinadumu bila ya manung’uniko ni jambo
jema,’’anasema.
VIONGOZI
WA DINI YA KIISLAMU
Sheikh Said Ahmad, anasema dini ya kiislamu, inaridhia
mwanamke mtarajiwa kuonekana na mume mtarajiwa, uso na viganja chini ya familia
yake.
Kwa mfano muume mtarajiwa anataka kumuona mtu
aliyependekezewa na familia yake, iko ruhusa ya kumuona, ingawa wasio wao
wawili peke yao.
Sheikh Mohamed Issa Ali, anasema hata kama anataka kuona
nywele, ngozi, mguu, mkono anaweza kuwatuma dada zake au shangazi zake.
SERIKALI
KUU INASEMAJE?
Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar
Tabia Maulid Mwita, anasema moja ya jukumu la Idara ya Utamaduni na Sanaa, ni uhifadhi,
uendelezaji na ukuzaji wa shughuli za utamaduni kwa wananchi.
Aidha waziri huyo anasema, kazi jukumu jingine ni utoaji
wa elimu ya utunzaji wa utamaduni ambao unalenga kuendeleza jamii husika.
Mwisho
Comments
Post a Comment