WANAHARAKATI
wa haki za watu wenye ulemvu wakili kisiwani Pemba, wamesema wakati umefika
kufanyiwa marekebisho sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai nambari 7 ya mwaka
2018, ili kuongeza kifungu kitakachowanyima dhamana, watuhumiwa watakaowadhalilisha
watu wenye ulemavu wa akili.
Walisema, sheria hiyo kwenye kifungu chake cha 151, kimeanisha
makosa yasiyo na dhamana ikiwa ni pamoja na kuua kwa makusdi, uhaini, kubaka,
kusafirisha kiwango kikubwa cha dawa za kulevya, kuingilia kinyume na maumbile.
Makosa mengine yalioanishwa kwenye kifungu hicho, ambayo hayana
dhamana ni kumnajisi mtoto wa kiume, kubaka kwa kundi, kuingilia maharimu
pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema katika kifungu
hicho, haikuanishwa iwapo mtu atambaka, kumnajisi, kumuingilia kinyume na
maumbile mtu, mtoto, mwanamke au mwanammke mwenye ulemavu wa akili.
Walisema, kasoro hiyo inaweza kutoa mwanywa kwa wadhalilisha,
kuendelea kuliathiri kundi la watu wenye ulemavu wa akili, wakijua wanapata
dhamana mahakamani.
Mmoja kati ya wanaharakati hao kutoka Jumuiya kwa ajili ya watu
wenye ulemavu wa akili Zanzibar ‘ZAPDD’, kisiwani Pemba, Khalfan Amour Mohamed,
alisema lazima kuwepo kifungu mahasusi.
Alieleza kuwa, kifungu hicho kiongeze kosa jingine la ubakaji,
ulawiti na unajisi kwa mtu wa umri wowote, mwenye ulemavu wa akili, iwe ni kosa
lisilokuwa na dhamana, kama yalivyo mengine.
‘’Kubaka, kulawiti na kuingilia kinyume na maumbile hata kama
aliyedhalilishwa yuko sawa kwenye afya ya akili, akifika mahakamani mtuhumiwa hana
dhamana, lakini iweje kwa makosa hayo akitendewa mwenye ulemavu wa akili, kuna
dhamana,’’alihoji.
Kwa upande wake Mratibu wa TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya
Mussa Said, alisema kasoro hiyo isiporekebishwa, kundi la watu wenye ulemavu wa
akili, litaendelea kukosa haki zao.
‘’Kama sheria ni msumeno, na Zanzibar inaendelea kuzilinda haki
za watu wenye ulemavu wa akili, lazima na hili lifanyiwe marekebisho, ili
atakayemdhalilisha mtu wa kundi hilo, anyimwe dhamana,’’alishauri.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati tendaji wa Jumuiya ya wanawake
wenye ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’ Hidaya Mjaka Ali, aleleza kuwa, ili kulilinda
kundi hilo, lazima sheria ziwatambuwe.
Mama mzazi wa mtoto mwenye ulemavu wa akili kutoka shehia ya Pujini,
ambae mtoto wake alidhalilishwa na mtuhumiwa Abdalla Khatib Abdalla, alisema
ipo haja ya sheria kurekebishwa.
‘’Hata mimi nilishangaa kuwa, nasikia makosa haya hayana
dhamana, lakini ukimdhalilisha mtu mwenye ulemavu wa akili, kumbe dhamana
ipo,’’alihoji mzazi huyo.
Mzazi mwengine wa shehia
ya Kengeja wilaya ya Mkoani, ambae kijana wake mwenye ulemavu wa akili alibakwa
na askari wa chuo cha Mafunzo Suleyom Idd Saleh, alishangaa baada ya kumuona, alipata
dhamana.
Wakati akiwasilisha mapungufu ya sheria mbali mbali kwenye
mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na TAMWA, Mwanasheria wa serikali, Ali
Amour Makame alisema, suala la marekebisho ya sheria ni jambo jema.
‘’Ni kweli kifungu cha 151 (1) cha sheria nambari 7 ya mwaka
2018 ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Zanzibar, imeanisha wazi makosa yasio na
dhamana, ingawa la kudhalilishwa mtu mwenye wa akili, halimo.
Nae mwananchi Khadija Issa Mzale wa Chake chake, anashauri kuwa
ingetungwa sheria moja tu ambayo itajumuisha makosa yote ya udhalilishaji,
badala ya sasa kuwepo kwenye sheria tofauti kama vile ile ya kuwalinda wari na
mtoto wa mazazi mmoja nambari 4 ya mwaka 2005.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saadi Khamis,
alisema changamoto kubwa kwa wenye ulemavu baada ya kudhalilishawa, ni kukosa
taaluma ya kuyaripoti matendo hayo.
Aliyekuwa hakimu wa mahakama ya watoto Pemba, Luciano Makoye
Nyengo, alisema changamoto inayojitokeza hadi kesi za watoto wenye ulemavu wa
akili, kutofikia pazuri ni changamoto ya ushahidi.
Kijana Asha Said Omar mwenye ulemavu wa viungo wa Michakaini
Chake chake, alisema ni vyema kuharakishwa kwa marekebisho hayo, ili watu wenye
ulemavu walindiwe haki zao.
Kifungu cha 30 cha sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar nambari
8 ya mwaka 2022, kinasisitiza wajibu wa kila mtu kulinda, kutetea haki za watu
wenye ulemavu, ikiwemo pale wanapovunjiwa haki zao za msingi, ikiwemo
kudhalilishwa.
Na kifungu cha 31 kikafafanua kuwa, watu wenye ulemavu
hawatobaguliwa au kudhalilishwa, kwa namna yoyote, kwa sababu ya ulemavu wake.
Lakini hata mkataba wa kimataifa wa haki za watu weye ulemavu,
Ibara ya 5 imeweka usawa na kutobaguliwa mbele ya sheria, kwamba watu wote wako
sawa.
Hayo yakijiri, hata Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kuanzia
kifungu cha 11 hadi 25A kinasisitiza usawa mbele ya sheria na kwamba mtu
hatodhulumiwa haki zake.
Mwisho
Comments
Post a Comment