NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WADAU wa haki jinai kisiwani Pemba,
wamesema wakati umefika sasa, kuwepo kwa kifungu maalum cha sheria, kinachotaja
kiwango mahasusi cha fidia, kwa mtu aliyedhalilishwa.
Walisema, kifungu hicho
cha sheria, pamoja na kutaja kiwango, kiweke ulazima wa kulipwa kwa muhanga
huyo, na hasa pia kuilazimisha Mahakama, kuzingatia maumivu ya muathirika huyo.
Wakizungumza na mwandishi
wa habari hizi, walisema kwa sasa hakuna kifungu cha sheria, kinachoonesha
kiwango maalum, hasa kulingana na maumivu aliyoyapata aliyedhalilishwa, hali
inayopelekea kupata athari mara mbili.
Walisema, kwa sasa
Mahakama hufanya makisio ya kutamka kiwango cha fidia, ingawa imekuwa vigumu
kutaja kiwango kwa upana wa maumvivu.
Mratibu wa Chama cha
Waandishi wa Habari Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-Hya Mussa Said,
alisema wapo watoto hudhalilishwa na wengine kupoteza utu wao na wengine kupata
ulemavu, ingawa fidia inayotajwa huwa ni ndogo.
Alieleza kuwa, haiwezekani
mtoto aliydhalilishwa na kisha kutakiwa alipewa shilingi 100,000 au shilingi
milion1, kama fidia, jambo ambalo linamzidishia maumivu.
‘’Lazima sasa kuwepo kwa
sheria maalum, au kuwepo kwa kifungu ndani ya sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka
2018, ikitaja kwa upana, fidia kwa wahanga wa udhalilishaji.
Nae mwanaharakati
Mwanakhamis Issa Ali wa Chake chake, alisema thamni ya mtu, ni kutokuchezewa
sehemu yake, hivyo kama atatokea mwengine kumvunjia haki yake, kusiwe na adhabu
ndogo.
‘’Kwa mfano mtoto wa kike
aliyeondoshewa utu wake, walau fidia ianzie shiligi milioni 100, lakini sio
jambo la shilingi mioni 1 au shilingi 500,000 kama ilivyo sasa,’’alieleza.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said, alisema kinachosikitisha hata hiyo fidia
ndogo inayotangaazwa mahakamani, waathirika haiwafikii.
Alifafanua kuwa, zipo
hukumu kadhaa ambazo, mahakama imemkuta na hatia mshitakiwa, na hutakiwa
kumlipa fidia mutahirika, lakini hatimae hakuna malipo.
‘’Ni kweli wakati umefika
sasa kwa kuwepo kwa kifungu kipana cha sheria, kinachofafanua aina ya fidia,
njia za kulipwa kwa haraka na isiwe kama ilivyo sasa, kuishia kwenye
maandishi,’’alieleza.
Mama wa mtoto aliyebakwa
mwaka 2022 na kisha kesi yake kutolewa hukumu mwezi Januari mwaka huu, alisema
sasa ni miezi mitano, hajapokea fidia ya shilingi milioni 1.
‘’Niliambiwa kuwa, pamoja
na mshtakiwa kufungwa miaka 20, alitakiwa anilipe fidia, lakini hadi sasa
mwanangu anaendelea kuuguza maumivu, sijaona jambo lolote,’’alieleza.
Mzazi mwengine wa Mchanga
mdogo, alisema katika kesi ya mtoto wake yenye namba 36/2022 ilihusisha kosa la
kubaka, mshitakiwa ni Ali Hassan Hamad, alifungwa miaka 30 na kutakiwa kumlipa fidia
ya shilingi 2,000,000, ingawa hadi sasa hajapokea.
‘’Ni kweli kama kunataka
kufanyiwa marekebisho ya kifungu cha sheria, ni sawa maana, watoto wetu
wanadhalilika mara mbili, ikiwemo kukosa fidia,’’alilalamika.
Aidha baba wa mtoto wa
miaka 9, wa mkoa wa kusini Pemba, ambae alikuwa na kesi yenye namba 37/2022, kwenye
kosa la kulawiti, mshitakiwa Masoud Khamis Mussa, alifungwa miaka 20 na kutakiwa
kulipa fidia ya 1,000,000 ingawa naye, hajalipwa.
Wahanga hao walisema, adhabu
inayotolewa kwenye mahakamani, zimekua haziwasaidii waathirika, bali huwaacha
na maumivu, mara baada ya kesi kumalizika.
Mwanasheria wa serikali
Mohamed Ali Juma, alisema bado kunachangamoto katika sheria zinazosimamia
jinai, na kama hazikuangaliwa, zinaweza kuongeza changamoto.
‘’Kama mtoto
ameshadhalilishwa, kisha kuna fidi hata hiyo ndogo haitoki, inakuwa ni shida,
lazima sheria zibadilishwe na kuwe na fidia kubwa inayotolewa.
Naibu Mrajis wa Mahakama
Kuu Pemba Faraji Shomar Juma, alisema ni wakati sasa, kuanzishwe kwa vifungu
maalum vya kisheria, vitakavyoanzisha mfuko maalum wa wahanga wavitendo vya
udhalilishaji.
Katibu wa Tume ya
Kurekebisha sheria Zanzibar Mussa Kombo, alisema kwa sasa, maeneo hayo ndio
wanayoyafanyiwa kazi, ili kuona kunakuwepo sheria maalum, ambayo itawasaidia
waathirika wa vitendo vya udhalilishaji kupata haki zao.
“Maeneo hayo ndio tunayoyafanyia
kazi na tunampango kazi wakukutana na wadau mbali mbali, ili tuone kasoro iko
wapi na waathirika waweze kupata fidia zao,” alisema.
Uchunguzu imebaini kuwa, kwa upande wa
Mahakama mkoa wa Kaskazini Pemba, zipo kesi 11 zilitolewa hukumu, 10 zilitakiwa
kulipwa fidia na zote hazijalipwa.
Wakati hayo yakifanyika,
sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, kifungu cha 109 (1) cha sheria hiyo, kimebainisha
kuwa, mshitakiwa akitiwa hatiani pamoja na adhabu atakayopewa, pia mahakama
imtake alipe fidia kwa kiwango ambacho, mahakama itaona inafaa.
Kifungu cha 313 (1) (2)
na kifungu cha 314 vya sheria ya mwaka 2018 sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai, kinailazimisha mahakama itoze fidia kwa muathiriwa, baada ya kuombwa au
bila ya kombwa na Mwendesha Mashtaka.
MWISHO.
Comments
Post a Comment