NA
HAJI NASSOR, PEMBA::
WANANCHI
wa shehia za Tumbe Magharibi na Mashariki wilaya ya Micheweni Pemba, wamesema
wameshakata tamaa, juu ya kulipwa fidia za vipando vyao, vilivyoharibiwa na
Shirika la Umeme la Zanzibar ‘ZECO’ wakati lilipokuwa likipelekea huduma ya
umeme soko la samaki Tumbe.
Walisema uharivu huo ambao
umefanywa tokea mwaka juzi, na kufanyia uhakiki mara mbili, lakini kutokana na
muda kuwa mrefu, hawana tena tamaa juu ya kulipwa fidia zao.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi kwa nyakati tofuati, walisema wamekuwa wakipewa ahadi
zisizotekeleza na mlipaji, ambae ni wizara ya Uchumi wa Buluu zaidia ya mwaka
mmoja na nusu sasa.
Mmoja kati ya wananchi hao
Halima Haji Khalid (90), alisema aliharibiwa Miembe, Mibirimbi, Mifenesi,
mihogo na migomba ingawa hadi sasa alichopewa ni ahadi.
‘’Mimi mmoja kati ya
waathirika wa kuharibiwa vipando vyangu, wakati ZECO linasafisha njia kwa ajili
ya kupeleka huduma ya umeme soko la samaki Tumbe, lakini hadi leo
sijalipwa.’’alieleza.
Nae Ali Kale alisema, pamoja
na kuharibiwa kwa vipando vyake alivyokuwa akivitegemea mfano minazi na
mifenesi, lakini hadi sasa hajapata fidia zake.
Nae Khadija Makame Shamata, alisema
haamini tena kuwa kuna siku atalipwa fidia yake, kutokana na kupewa ahadi hewa
kila muda kutoka wizara ya Uchumi wa buluu.
‘’Tupo zaidi ya wananchi 35
ambao tuliharibiwa vipando vyetu vichanga wakati ZECO inapeleka huduma ya umeme
soko la samaki Tumbe, lakini hadi sasa hatujalipwa,’’alieleza.
Kwa upande wake Aisha Issa
Mjaka, alisema alielezwa kuwa watalipwa fidia zao wakati wowote, ingawa
kutokana na muda kuwa mkubwa, kwa sasa hana tena tamaa.
Kaimu sheha wa shehia ya
Tumbe Mashariki Omar Ali Omar alikiri kuwepo kwa shida hiyo, na kusema mara ya
mwisho uongozi wa uchumi wa Buluu Zanzibar uliwaahidi kuwalipa fidia wananchi
hao mwezi Mei mwaka huu.
‘’Kikao cha mwisho kilifanyika
mwezi Aprili mwaka huu, ndani ya soko la samaki la Tumbe, baina ya waathirika
na uongozi wa wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, na ahadi ikatolewa kuwa mwezi
Mei watalipwa, lakini hadi sasa bado,’’alieleza.
Alisema taarifa za kuwa
wananchi wa shehua yake hawajalipwa fididi hizo ameshazifikisha kwa uongozi wa
wilaya ya Micheweni, kwa muda mrefu sasa.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni
Mgeni Khatib Yahya, alikiri kuwepo kwa taarifa hiyo, na kusema tayari ameifikisha
shirika la umeme la Zanzibar ‘ZECO’ ofisi ya Pemba.
Alisema, mara ya mwisho aliahidiwa
kuwa, mpango wa kulipwa kwa fidia hizo umeshawekwa sawa na wakati wowote
wananchi hao watalipwa.
‘’Ni kweli wananchi wa
shehia za Tumbe Mashariki na Magharibi walioharibiwa vipando vyao, wakati wa
upelekaji umeme soko la samaki Tumbe hawajalipwa, na taarifa hizi nshazifikisha
ZECO,’’alieleza.
Meneja wa shirika la Umeme
la Zanzibar ZECO tawi la Pemba Mohamed Juma, alikiri kuwa deni hilo kwa wananchi
hao halijalipwa, ingawa wao sio wahusika.
‘’Sisi ZECO tulipewa kazi ya
kufikisha huduma ya umeme soko la samakini Tumbe na wizara ya Uchumi wa Buluu
na Uvuvi, na hao ndio tuliokubaliana kuwa walipe fidia,’’alieleza.
Meneja huyo alieleza kuwa
hata wananchi wanalijua hilo, kuwa walipaji sio ‘ZECO ‘bali na wizara ya Uchumi
wa Buluu na Uvuvi, kama makubaliano yalivyofikiwa.
Afisa Mdhamini wizara ya
Uchumi wa Buluu Pemba Dk. Salum Mohamed Hamza, alikiri kuwa hadi sasa fidia
hiyo haijalipwa, ingawa nia bado ipo.
Alisema kwa sasa wanaisubiri
wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, maana ndio walipaji wakuu wa madeni yote
ya serikali, kwa mujibu wa maelekezo ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa
hesabu za serikali.
‘’Sisi tunaisubiri wizara ya
fedha, baada ya kumaliza taratibu zao, kama watutingizia sisi fedha tutawalipa
fidia zao wananchi, na kama watalipa wenyewe pia sawa,’’alieleza.
Aidha alieleza kuwa, wastani
wa shilingi milioni 60 hadi 70 ndio ambazo zikadiriwa kulipwa na hasa baada ya
kufanya tathmini ya mara ya pili, ambayo ya mara kwanza ilikuwa na makosa
kadhaa.
‘’Wamo baadhi ya wananchi
watalipwa katia ya shilingi milioni 4, wengine hadi 6, na hii itawashangaaza
wananchi, maana wao walitarajia kupata kidogo, lakini kwa tathimini ya mtathimini
mkuu kutoka wizara ya Ardhi fidia zimeongezeka,’’alieleza.
Sehemu eneo la kuuzia
samaki la soko hilo lilifunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi Julai 26, mwaka huu.
Mwisho
Comments
Post a Comment