NA SALMA LUSANGI::
KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini ( WMNM) Joseph Kilangi amesema Wizara yake ipo katika mchakato wa kuifanyia marekebisho sera ya maji ili iendane na wakati uliyopo sasa.
Akizungumza katika kikao cha pamoja nilichofanyika jana katika ofisi ya Mamlaka ya Maji safi na Mazingira Dodoma (DUWASA) ambapo kikao hicho amekusudia kujitambulisha kwa viongozi wa Wizara ya Maji ya SMT baada ya uteuzi wa makatibu wa wakuu uliyofanyika June 30, 2022 .
Alisema wizara ya MNM inaendelea na kazi ya kupitia sera ya maji ili Sekta ya maji iweze kuleta tija kwa Serikali angalau wananchi wachangie huduma ya maji.
Alifahamisha kwamba lengo kuu, la wizara yake kuwataka wananchi wachangie maji ni kuipunguzia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ( SMZ) mzigo mkubwa wa kuendesha bure sekta hiyo kutokana gharama ziliyopo.
Katibu mkuu huyo alifafanua kwamba gharama za kuendesha huduma ya maji ni kubwa ikiwemo, uchimbaji wa visima, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa matangi pamoja na huduma ya umeme hivyo uchangiaji wa wananchi utasaidia kuleta ufanisi katika kuendesha huduma hiyo.
Alisema hata hivyo SMZ bado inaendesha huduma zingene bure, ikiwemo afya na elimu hivyo amewaomba wananchi wa Zanzibar kuunga mkono katika kuchangia huduma ya maji.
Aidha katibu Mkuu Kilangi aliwashukuru viongozi wa Wizara ya Maji ya SMT kwa mapokezi mazuri pamoja na kuendeleza mashirikiano kupitia sekta hiyo. Alisema vikao vya pamoja vinaonesha inshara njema katika kulipatia ufumbuzi tatizo la maji Zanzibar.
" Najua vikao vingi, vimefanyika, hadi tumepata fedha za Uviko 19, zimetusaidia katika uchimbaji wa visima, mmetupa mtaalamu Dkt Subira ameweza kutusaidia kuhusu Groundwater, Naibu Katibu Mkuu msituache mkono, kwani tukiendeleza mashirikiano, Muungano tutakua tumeutendea haki" Alisema Kilangi.
Naye Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maji ( SMT) Nadhifa Kemikimba alimshukuru Katibu Mkuu Kilangi kwa uamuzi wake huo wa kufunga safari ya kutoka Zanzibar na kwenda Dodoma kwaajili ya kujitambulisha kwa lengo la kuendeleza mashirikiano baina Wizara bili hizo.
Aidha alishauri kwamba kupitia vikao vyao vya mashirikiano wawe na jitathimini kwa kulinganisha kabla ya masharikiano walikuaje na baada ya mashirikiano ufanisi umeongezeka kwa kiasi gani! ili hata wakiandika ripoti kwa viongozi wa juu ioneshe uhalisia .
Kwa upande wa wakurugenzi wamependekeza katika vikao vya pamoja kuwe na utaratibu wa kuwaalika maafisa manunuzi wa pande zote mbili ( SMZ na SMT) ili waweze kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika vitengo hivyo. Alisema kwani bado kuna changamoto kwa upande wa manunuzi na zinahitaji kupatiwa ufumbuzi.
Katibu Mkuu WMNM Joseph Kilangi katika safari yake hiyo aliambatana na watendaji wake akiwemo Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti Dkt Maryam Issa, Afisa, Mipango, Afisa Utumishi na Afisa Uhusiano, na alikaribishwa na Naibu Katibu Mkuu, Mhandishi Nadhifa, wakurugenzi na maafisa wengine wa wizara ya Maji ( SMT).
MWISHO
Comments
Post a Comment