NA HAJI NASSOR, PEMBA::
CHAMA cha Mapinduzi CCM wilaya ya
Mkoani Pemba, kimeitaka familia ya mwanachama wao Omar Mohamed Hamad wa
Chumbageni Wilayani humo, kuwa na moyo wa subra katika kipindi hiki kigumu.
Kauli hiyo
imetolewa na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Ali Juma Nassor, wakati
akizungumza na wanafamilia hao, kufuatia kifo cha mwanachama wao.
Alisema, jambo
hilo ni maandiko ya Muumba, hivyo ni vyema wawe wastahamilivu katika kipindi
hiki kigumu, kwani suala la kuondokewa sio jambo jepesi.
Aidha Katibu
huyo alisema enzi za uhai wake, marehemu alikuwa mstari wa mbele katika ujenzi
wa chama, hivyo mchango wake hautosahaulika daima.
Alieleza kuwa,
marehemu alikuwa karibu mno na chama, na maisha alikuwa hachoki kuendeleza
mikakati na maono ya chama ili kuhakikisha kinasonga mbele.
‘’Kwanza tunawapa
pole wanafamilia kwa kuondokewa na ndugu yenu ambae ni mwanachama wetu wa chama
cha Mapinduzi, na endeleeni kumuombea,’’alishauri
Katibu wa
CCM jimbo la Chambani Amour Kheir Vuai, akizungumza kwa niaba ya Mbunge na
Mwakilishi wa jimbo hilo, alisema viongozi wao wameitaka familia kujenga moyo
wa subra.
Alisema
viongozi hao, wamepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa, na hasa
kutokana na umahiri na utendaji wa kazi ndani ya chama.
‘’Viongozi
wetu pamoja na wanachama wa Jimbo lote la Chambani, wameupokea msiba wa
mwanachama Omar Mohamed Hamad kwa mshituko mkubwa,’’alieleza Katibu huyo.
Kwa upande
wake Diwani wadi wa Ngachani Mohamed Said Ali alisema kilichobakia kwa upande
wa chama na familia, ni kumuombea dua marehemu huyo, ili asilimike na adhabu ya
Muumba.
Alieleza
kuwa, moja katia ya mambo matatu ambayo marehemu yanaweza kumsaidia ni dua
kutoka kwa wenzake, hivyo ni vyema hilo likadumishwa.
‘’Sisi chama
cha Mapinduzi pamoja na utamaduni wetu huu wa kuwafariji walioondokewa na ndugu
yao, lakini wakati mwengine huandaa dua ya pamoja na wengine,’’alieleza.
Mapema
akizungumza na kwa niaba ya familia hiyo, Ramha Omar Mohamed, alisema
wamefurahishwa mno na uongozi wa CCM wilaya ya Mkoani kwa kuwafariji.
‘’Hili kwetu
sisi kama familia sio jambo dogo lililofanywa na chama cha Mapinduzi la kufika
nyumbani kuonana na kutuombea dua la baba yetu aliyefariki,’’alieleza.
Hata hivyo
ameushauri uongozi huo wa CCM kuanzia ngazi ya shina hadi taifa, kuendeleza
utamaduni wa kuwafariji wanachama wenzao waliofariki na wagonjwa popote walipo.
Marehemu
Omar Mohamed Hamad ambae alianza kuumwa tokea mwanzoni mwa mwaka jana na
alifariki Oktoba 23, mwaka huu, ambapo ameacha mke mmoja na watoto wanne.
Katika uhai
wake marehemu, alikuwa mwanachama kamili wa CCM na mjumbe wa kamati ya siasa ya
tawi la CCM Chumbageni Jimbo la Chambani.
Mwisho
Comments
Post a Comment